1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhariri wa leo.

30 Oktoba 2009

Je kuna Demokrasia ya Kweli nchini Msumbiji?

https://p.dw.com/p/KJ8E
Rais Armando Guebuza anaongoza katika uchaguzi wa rais pamoja na chama chake cha Frelimo katika uchaguzi wa bungePicha: AP

Nchini Msumbiji chama tawala kimepata ushindi kwa mara nyingine kwa njia isiyokuwa ya kidemokrasia.Ujerumani kama nchi mshirika wake wa kimaendeleo inabidi kuitathmini hali hii.

Tarehe 28 mwezi wa Oktoba raia wa Msumbiji walijitokeza kupiga kura kuchagua bunge jipya na rais. Dalili zote zilionyesha kwamba chama tawala cha Frelimo ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1975 nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake kitashinda katika chaguzi zote mbili.

Msumbiji inaangaliwa kama ni lulu katika ushirikiano wa kimaendeleo kwenye eneo la bahari ya Hindi,nchi inayozungumzwa panapohusika na zoezi la demokrasia barani Afrika. Uongozi bora na demokrasia nchini humo ni mambo ambayo siku za nyuma hayakukosa kuzungumzwa iwe na Benki ya dunia,Umoja wa Ulaya au serikali ya Ujerumani.

Lakini katika uchaguzi wa tarehe 28 mwezi huu sifa hizo zimetoweka kutoka kila upande.Ingawa zoezi zima la uchaguzi lilifanyika kwa njia barbara na uchaguzi wenyewe kufanyika bila matatizo lakini ni lazima kuweka wazi kwamba kumekuweko dosari chungumnzima zilizougubika uchaguzi huo.

Wahlen in Mosambik: Anhänger von Präsident Armando Guebuza
Wafuasi wa chama tawala cha FrelimoPicha: AP

Kosa kubwa kabisa lililojitokeza katika uchaguzi huo ni hatua ya tume ya uchaguzi kukizuia chama cha upinzani cha Mozambique Movement for Demokrasi MDM kutogombea katika majimbo 9 kati ya majimbo 13 ya uchaguzi. Hali hiyo moja kwa moja,tangu mwanzo ilikifungia nafasi chama hicho kushinda katika uchaguzi huo.

Kuna pia vyama vingine vidogo vidogo ambavyo vilinyimwa nafasi hiyo ya kushiriki katika uchaguzi.Hata hivyo tume ya uchaguzi ilijitetea katika uamuzi wake huo na kusema kwamba vyama hivyo vimekosa kuwasilisha stakabadhi zinazohitajika kuwasimamisha wagombea wake katika uchaguzi huo.

Katika uamuzi wake dhidi ya chama cha MDM tume hiyo ya uchaguzi ilisisitiza kwamba sheria lazima zizingatiwe na sio pendekezo lake kukizuia chama hicho.Hata hivyo kwa upande mwingine tume hiyo ya uchaguzi ilikiri kwamba chama cha upinzani cha MDM hakikupewa muda wa mwisho wa kuwasilisha stakabadhi zake za wagombea watakaosimama katika uchaguzi huo, wala kusimamisha wagombea mbadala, hatua ambayo bila shaka inaonyesha kwamba tume hiyo ilikiuka sheria.Tume hiyo haijatoa maelezo kwanini ikachukua uamuzi huo na wala stakabadhi hizo muhimu hadi hii leo hazijaweza kuchunguzwa ipasavyo.

Sio tu kwamba uchaguzi haujafanyika kwa njia ya haki lakini pia wagombea wa chama tawala cha Frelimo walifanya kampeini kwa kutumia mali ya serikali ikiwemo magari ya serikali ambayo yalikuwa yakionekana yakizunguka kuwapigia debe wagombea kadhaa wa chama hicho.

Sio jambo geni kwa chama hicho kutumia mali ya serikali katika uchaguzi tangu kuanza muhula wa kwanza wa rais Amando Guebuza mwaka 2004 maafisa wengi wa serikali wamekuwa wakishinikizwa kuunga mkono chama hicho cha Frelimo. Nafasi muhimu zote zimekuwa zikipewa wafuasi wa chama tawala na wasiokuwa wafuasi huambulia patupu.

Kutokana na hali kama hii umefika wakati kwa nchi fadhili kuzungumzia wazi juu ya suala la Demokrasia nchini Msumbiji na kutoa ujumbe kwa serikali ya nchi hiyo.Serikali ya Ujerumani kama mshirika wa moja kwa moja wa kimaendeleo nchini humo inabidi kutafakari upya na kuangalia iwapo inalazimika msaada wake wa kusaidia bajeti ya nchi hiyo.

Mwandishi:Beck Johannes/Saumu Mwasimba

Mhariri Abdul Rahman