1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugonjwa wa EHEC wazidi kuenea

1 Juni 2011

Kufuatia kusambaa kwa ugonjwa unaosababishwa na kimelea cha E.Coli hapa Ujerumani, hivi leo serikali imewaomba watu wachangie damu kuwasaidia wagonjwa waliolazwa hospitalini kutokana na ugonjwa huo.

https://p.dw.com/p/11Sai
Inaaminika kuwa ugonjwa wa EHEC unatokana na vitango
Inaaminika kuwa ugonjwa wa EHEC unatokana na vitangoPicha: picture alliance/dpa

Mji wa Hamburg umethibitisha visa 200 vya watu ambao ama wamedhurika moja kwa moja au wanahofiwa kupatwa na maradhi hayo yanayotokana na kula vitango vibichi. Maradhi hayo yanayojuilikana kwa ufupi kama EHEC, hulifanya figo kushindwa kufanya kazi na hivyo kupelekea kifo.

Darizeni kadhaa za wagonjwa wanaripotiwa kuwa katika hali mbaya na wanahitaji kuwekwa damu haraka kunusuru maisha yao.

Viongozi wa mji wa Hamburg wanasema kwamba, kwa sasa hospitali mjini humo zina damu ya kutosha, lakini watalazimika kuirudisha damu inayotumiwa hivi sasa kwenye benki ya akiba ya damu.

Viongozi hao wanasema itachukuwa muda kwa akiba iliyopo kukauka, lakini ni lazima juhudi za kuzuia hilo zifanyike sasa.

Hadi sasa watu 16 wameshafariki dunia kutokana na maambukizi ya EHEC, 15 kati yao wakiwa ni hapa Ujerumani.

Uchunguzi wa maradhi ya EHEC katika maabara
Uchunguzi wa maradhi ya EHEC katika maabaraPicha: dapd

Kwa ujumla, hadi sasa watu wapatao 1,000 wameripotiwa kupatwa na ugonjwa huu katika maeneo nchini Ujerumani, lakini wengi wao maambukizi yameishia kwenye kuumwa na tumbo, kuharisha na kutokwa na damu.

Katika jimbo la Lower Saxony pekee, maafisa wanasema kwamba idadi ya watu wanaoshukiwa kupatwa na ugonjwa huu imepanda hivi leo kutoka 84 hadi 344, huku 64 kati yao wakihitaji huduma za haraka za matibabu. Majimbo mengine ya karibu yana idadi inayokaribiana na hii.

Serikali ya jimbo la Hamburg inasema kwamba dalili zote zinaonesha kuwa wagonjwa wengi ni wale walikula vitango, lakini imelikanusha lile dai la kwanza kwamba vitango hivyo vilitoka Hispania.

Waziri wa Ujerumani anayeshughulikia haki za walaji, Ilse Aigner, amesema kwamba bado hali haijawa ya kuridhisha.

"Tunakabiliwa na changamoto kubwa sana hivi sasa. Tunapaswa kukusanya ushahidi wa mamia kwa maelfu ya sampuli kuziweka pamoja na baadaye kufanya uchunguzi kupata jawabu sahihi la sababu ya maambukizi haya." Amesema Aigner.

Sasa kuna kila dalili kwamba huenda Hispania ikidai fidia kwa onyo lilitolewa wiki iliyopita dhidi ya vitango vyake. Naibu Waziri Mkuu wa Hispania, Alfredo Perez Rubalcaba, amesema kwamba nchi yake huenda ikachukua hatua za kisheria dhidi ya jimbo la Hamburg.

Rais wa Baraza la Afya la Mkoa wa Kaskazini wa Ujerumani, Mathhias Pulz
Rais wa Baraza la Afya la Mkoa wa Kaskazini wa Ujerumani, Mathhias PulzPicha: picture-alliance/dpa

Hispania inasema kwamba, wakulima wa mbogamboga katika nchi hiyo wamepoteza kiasi ya euro milioni 200 kwa kipindi cha wiki moja tangu vitango vyao vishukiwe kusababisha maradhi ya EHEC.

Rubalcaba amesema kwamba anatarajia kuwa vikwazo dhidi ya vitango vya nchi yake katika soko la Ulaya, vitaondoshwa leo hii, huku akitaka kuwepo kampeni ya kurudisha taswira nzuri ya mazao ya kilimo kutoka Hispania.

Msemaji wa chama cha upinzani cha kihafidhina nchini Hispnia, Soraya Saenz de Santamaria, ameuita uamuzi wa awali wa Waziri wa Afya wa jimbo la Hamburg,Cornelia Pruefer-Storcks, kuyahusisha maradhi ya EHEC na vitango vya Hispania kuwa "haukuwa wa kiuwajibakaji kabisa."

Hata hivyo Waziri Aigner amekiambia kituo cha televisheni cha ZDF cha hapa Ujerumani, kwamba serikali ya jimbo la Hamburg ilitekeleza vyema wajibu wake kwa mujibu wa sheria za Umoja wa Ulaya, kwa kutoka onyo baada ya vimelea vya E.Coli kugundulika kwenye vitango vya Hispania.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPAE/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman