1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugomvi wazuka katika klabu ya Bayern

18 Aprili 2015

Pep Guardiola ananyoshewa vidole vya lawama baada ya daktari wa klabu hiyo aliyehudumu kwa karibu miaka 40, Hans-Wilhelm Mueller-Wohlfahrt, kuamua kuondoka klabu ya Bayern Munich

https://p.dw.com/p/1FASR
Bayern München Guardiola und Müller-Wohlfahrt streiten sich
Picha: imago/Ulmer

Hii ni kufuatia kichapo chao cha magoli matatu kwa moja katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Porto.

Daktari huyo mwenye umri wa miaka 72, ambaye amekuwa katika klabu ya Bayern tangu mwaka wa 1977, alijiuzulu Alhamisi usiku pamoja na timu yake ya maafisa wa matibabu akisema wamewajibishwa kutokana na matokeo mabaya ya timu, na kuwa kiwango cha imani kilipungua katika usimamizi wa klabu hiyo.

Kocha Pep Guardiola alionekana kukwepa maswali katika vikao vya waandishi wa habari katika wiki za karibuni akisema na namkuu “muulize daktari”, na huku wachezaji nyota Franck Ribery, Arjen Robben, Philipp Lahm na Bastian Schweinsteiger wote wakiwa mkekani, mvutano kati ya Guardiola na Daktari umefikia kilele. Hapo jana Guardiola alisema anamheshimu sana daktari aliyeondoka na akakataa kumlaumu.

“wakati mchezaji anaumia, siyo makosa ya daktari” aliwaambia wanahabari. Hata hivyo Guardiola hivi karibuni alimpuuza daktari Muller-Wohlfahrt katika kisa cha Thiago Alcantara, ambapo alimtuma mjini Barcelona ili kutibiwa jeraha la muda mrefu.

Mueller-Wohlfahrt, aliyeondoka Bayern kwa muda mfupi mwaka wa 2008 baada ya kutoelewana na kocha wa wakati huo Jurgen Klinsmann lakini akarejeabaada ya kocha huyo kuondoka, aliliambia gazeti la Bild Ijumaa kuwa “atafichua yote, lakini sasa ni mapema mno”.

Bayern ilisema imepokea ombi la kujiuzulu daktari huyo kwa masikitiko na kumshukuru kwa huduma zake bora zaidi wakati wote.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu