1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yawasilisha orodha ya mageuzi.

24 Februari 2015

Ugiriki imeiwasilisha orodha ya mapendekezo ya mageuzi inayozingatiwa kuwa msingi mzuri wa kuiwezesha nchi hiyo kuendelea kupatiwa mkopo.Wakati huo huo Ujerumani imeashiria uwezekeno wa kuyakubali maombi ya Ugiriki

https://p.dw.com/p/1EgR8
Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis
Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis VaroufakisPicha: Reuters/E.Vidal

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imearifu leo kwamba mapendekeo ya Ugiriki juu ya kuzitekeleza hatua za mageuzi yameshawasilishwa kwenye taasisi Halmashauri hiyo. Taasisi hiyo imesema orodha hiyo ya mapendekezo ni msingi sahihi wa kutafakari kuendelea kuisaidia Ugiriki kwa muda wa miezi minne.

Wasiwasi juu ya kuishiwa fedha

Pana wasi wasi mkubwa ,huenda Ugiriki ikaishiwa fedha kabisa na hivyo kulazimika kuondoka kwenye Umoja wa sarafu ya Euro ikiwa Umoja wa Ulaya hautaendelea kutoa sehemu yake ya mkopo kwa Ugiriki. Muda wa mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuisaidia Ugiriki unamalizika hapo Jumamosi.

Ahadi ya kuendelea kuyatekeleza mageuzi ni sharti la msingi kwa Ugiriki kueongezewa muda wa kuendelea kupatiwa mikopo. Msemaji wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya ameeleza kwamba mapendekezo ya Ugiriki yamewasilishwa wakati mwafaka na kwamba yanaweza kuwa msingi wa kuyatafakari kwa mafanikio. Msemaji huyo ameeleza kuwa mapendekezo hayo ni kamilifu na yanaonyesha kuwa Ugiriki itauzingatia wajibu wake.

Vita dhidi ya wanaokwepa kulipa kodi

Mapendekezo ya Ugiriki ni pamoja na kuwapiga vita wanaokwepa kulipa kodi na wale wanaohujumu uchumi wa nchi na pia yanaekelezwa katika kupambana na rushwa . Mkutano wa nchi za ukanda wa sarafu ya Euro kwa njia ya simu unatarajiwa kufanyika baadae leo ambapo mapendekezo ya Ugiriki yatajadiliwa.

Wakati huo huo Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble amewasilisha maombi ya kupigwa kura bungeni juu ya mapendekezo yaliyowasilishwa na Ugiriki kwa Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya , ECB na Shrika la Fedha la Kimataifa IMF. Kura hiyo itakuwa juu ya kuamua kuyakubali maombi ya Ugiriki.

Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis amesema anatumai mapendekezo yaliyowasilishwa na nchi yake yatapitishwa na Umoja Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na Shrika la Fedha la Kimataifa . Ikiwa mawaziri wa umoja wa sarafu ya Euro leo watayakubali maombi ya Ugiriki,watakuwa na muda wa wiki nzima wa kufanya matayarisho ya kuupitisha rasmi mpango wa kuendelea kuisaidia Ugiriki.

Mwandishi;Mtullya Abdu.dpa,afp.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman