1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yataka mazungumzo na Al-Qaeda

Kabogo Grace Patricia23 Septemba 2010

Mazungumzo hayo ni katika jitihada za kuachiwa huru kwa raia wake watano waliotekwa nyara huko Niger.

https://p.dw.com/p/PL6m
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Herve Morin.Picha: AP

Ufaransa inajaribu kuwasiliana na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda katika jitihada za kufanya nalo mazungumzo ya kuachiwa kwa raia watano wa Ufaransa wanaoshikiliwa mateka kwenye eneo la Sahara, baada ya kundi hilo kuonya dhidi ya majaribio yoyote ya kutaka kuwaokoa mateka hao.

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Herve Morin amekiambia kituo cha redio cha RTL kwamba nchi hiyo inaamini kuwa raia watano wa Ufaransa na Waafrika wawili wanaofanya kazi katika kampuni za Ufaransa wako hai na wanashikiliwa kaskazini mwa Mali, wiki moja baada ya kutekwa huko Niger. Morin alisema wanachozingatia kwa sasa ni uwezekano wa kuwasiliana na al-Qaeda ili kujua matakwa yao, ambayo bado hawajayapokea hadi sasa. Taarifa hiyo inaonyesha kwa mara ya kwanza Ufaransa kukiri kuwa iko tayari kuanzisha mazungumzo.

Katika Ikulu ya nchi hiyo, Rais Nicolas Sarkozy alikutana na baraza lake la mawaziri, maafisa wa ngazi za juu wa jeshi pamoja na wakuu wa ujasusi na polisi kwa ajili ya kujadiliana kuhusu suala hilo. Hata hivyo, Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa ilikataa kuzungumzia moja kwa moja taarifa hiyo ya Morin, ikisema kuwa nchi hiyo inafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa mateka hao wanarejea wakiwa salama. Msemaji wa wizara hiyo, Romain Nadal alisema hawezi kuzungumza zaidi kwa sababu katika matukio kama hayo, busara inahitajika kuhakikisha ufanisi katika utekelezaji wao.

Alhamisi iliyopita watu wenye silaha waliwateka nyara raia watano wa Ufaransa, wakiwemo wanandoa pamoja na raia mmoja wa Togo na Madagascar baada ya kufanyika uvamizi katika nyumba mbili zilizopo kwenye mgodi wa madini ya uranium katika mji wa Arlit, kaskazini mwa Niger. Wengi wa waliotekwa nyara wanafanya kazi katika kampuni ya nishati ya nyuklia inayomilikiwa na Ufaransa ya Areva au katika kampuni yake ndogo ya kandarasi ya Satom. Tangu tukio hili litokee, kampuni hizo zimekuwa zikiwaondoa wafanyakazi wake wa kigeni kutoka kwenye mgodi wa madini ya uranium uliopo Niger.

Wapiganaji wa tawi la al-Qaeda la Afrika Kaskazini-AQIM, wamedai kuhusika na utekaji nyara huo na wameonya kuwa Ufaransa isijaribu kujiingiza katika jaribio lolote la hatari kwa kutumia vikosi vya jeshi kwa lengo la kuwaokoa mateka hao. Ufaransa imesema kitendo cha kundi hilo kukiri kuhusika na utekaji nyara huo ni cha kweli na maafisa wana amini kuwa mateka hao wamepelekwa katika eneo la mbali la milimani la Mali karibu na mpaka wa Algeria. Aidha, Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Herve Morin amesema hawajapokea taarifa yoyote ya uhakika wa mateka hao kuwa hai, lakini wana kila sababu ya kuamini kwamba wako hai.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne na kundi hilo la AQIM kupitia Al-Jazeera na mtandao wa YouTube, imeeleza kuwa wanaiarifu serikali ya Ufaransa kuwa Mujahedeen watatuma madai yao halali baadaye na kuonya dhidi ya hatua zozote zitakazochukuliwa na serikali hiyo. Morin amesema Ufaransa haijapokea taarifa zozote nyingine kutoka kwa watekaji hao. Ufaransa imepeleka timu ya maafisa wa ujasusi nchini Niger ikiwa na ndege za kipelelezi na jana Rais Sarkozy alisema Ufaransa itatumia vyombo vyake vyote vya kiusalama kuhakikisha mateka hao wanaachiwa huru.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman