1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa wapewa mapokezi ya kishujaa

Bruce Amani
16 Julai 2018

Mabingwa wa dunia wa kandanda Ufaransa wanawasili nyumbani leo na kupewa mapokezi ya mashujaa baada ya kushinda Kombe la Dunia kwa mara ya pili.

https://p.dw.com/p/31X3A
Frankreich empfängt seine Weltmeister
Picha: Reuters/P. Rossignol

Mashabiki 78,000 walitazama mechi hiyo uwanjani huku mabilioni ya watu wakiifuatilia kote duniani kupitia televisheni. Siku 161 baada ya Didier Deschamps kunyanyua Kombe la Dunia katika anga za Saint-Denis mnamo Julai 12 1998, Kylian Mbappe akazaliwa. Miongo miwili baadaye, Mbappe mwenye umri wa miaka 19, aliifungia Ufaransa bao la nne na kuipa ushindi dhidi ya Croatia katika fainali ya Kombe la Dunia

Na umahiri wake ulitosha kumpa taji la mchezaji bora chipukizi wa mashindano hayo. Msikilize Mbappe "Nna furaha sana. Lakini kama nilivyosema, ni tofauti, mchezo ni tofauti kwa wachezaji wote. Kuna wachezaji ambao wako karibu umri wa miaka 30, ambao wamecheza kwa muda mrefu ili kushinda kombe hili. Kwangumimi, ni mwanzo tu. kwangu ni hatua kubwa, lakini ni hatua ambayo inahitaji kunifikisha mbali zaidi"

Na kwa Deschamps, sasa anakuwa mtu wa tatu pamoja na Mario Zagallo na Franz Beckenbauer kushinda Kombe la Dunia akiwa mchezaji na baadaye kocha.

FIFA Fußball-WM 2018 | Kroatien Vize-Weltmeister | Fans in Zagreb
Mashabiki wa Croatia wanaikaribisha timu yao ZagrebPicha: Reuters/A. Bronic

Rais wa Ufaransa Macron, anaikaribisha timu ya Les Bleus leo mjini Paris na wachezaji watakuwa kwenye basi la wazi likalofanya msafara katika mtaa maarufu wa Champs-Elysees, ambako watalakiwa na mamia kwa maelfu ya watu.

Mashabiki nchini Ufaransa walikesha mitaani wakishangilia ushindi huo isipokuwa katika baadhi ya matukio kulizuka vurugu huku vijana wakijaribu kupora duka hatua iliyowalazimu polisi kufyatua mabomu ya kutoa machozi.

Kwa Croatia, kichapo hicho kilikuwa kichungu lakini timu hiyo inajipa fahari kwa kutinga fainali hiyo kwa mara yao ya kwanza kabisa kama anavyosema nahodha Luka Modric "Tumewaikilisha Croatia katika njia bora Zaidi kwenye fainali hii. Tumehuzunika kiasi bila shaka. Hatuwezi kuwa na furaha lakini baada ya muda, tutambua mafanikio tuliyopata hapa. Bila kujali kuwa tulishindwa leo, tunapaswa kujivunia na hatuna chochote cha kujutia, maana tulijaribu tuwezavyo, na mambo hayakwenda upande wetu. Lakini tuna furaha kwa namna tulivyocheza katika dimba hili lote na kwenye fainali"

Mchezaji kiungo wa Croatia Luka Modric alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo, huku kipa wa Ubelgiji Thibaut Courtois akishinda taji la kipa bora. Harry Kane wa England alipata tuzo ya mfungaji bora baada ya kutikisa nyavu mara sita.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/Reuters
Mhariri: Josephat Charo