1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa na Uingereza zaumana leo robo fainali

9 Julai 2011

Fainali za kombe la dunia kwa wanawake zimeendelea hapa nchini Ujerumani katika robo fainali. Mahasimu wa jadi katika soka Ufaransa wanaonyeshana kazi na Uingereza ambapo wenyeji Ujerumani inakibarua na Japan.

https://p.dw.com/p/11sKl
Wanawake wa Ufaransa wakishangiria bao wakati matokeo yakiwa 1-1 dhidi ya Uingereza.Picha: picture-alliance/dpa

Fainali za kombe la dunia kwa wanawake zinaendelea hapa nchini Ujerumani ambapo michuano hiyo sasa inaingia katika duru ya robo fainali. Mahasimu wa jadi katika soka, Ufaransa na Uingereza , wanatiana kifuani katika mchezo muhimu leo jioni kuwania tikiti ya nusu fainali. Na kombe la Copa America, kombe la mataifa ya kusini mwa bara la Amerika, Brazil baada ya kuanza kwa kusuasua, inakwaana leo na Paraguay, wakati Venezuela ina miadi na Ecuador katika kundi B.

Mahasimu wa jadi katika soka, Ufaransa na Uingereza, wataonyeshana kazi leo jioni katika robo fainali ya michuano ya kombe la dunia kwa wanawake katika mchezo muhimu wa kuwania tikiti ya kucheza katika nusu fainali. Uingereza ilisonga mbele katika fainali hizi ikiwa mshindi katika kundi B, na Ufaransa ikimaliza ya pili katika kundi A, kundi ambalo lilizijumuisha timu za Ujerumani, Nigeria, Ufaransa na Canada. Les Bleus inaonekana kuwa na nguvu zaidi kutokana na kushinda mara tano dhidi ya ushindi mara mbili tu wa Uingereza, huku timu hizo zikitoka sara mara tano , ikiwa ni pamoja na katika michezo yao mitatu ya mwisho. Lakini itakuwa ni mara ya kwanza kukutana katika fainali za kombe la dunia na timu hizo zote zina usongo wa kufanya kweli . Uingereza haijawahi kuishinda Ufaransa kwa zaidi ya miaka 37, ambapo kwa Ufaransa ilikuwa ni Waingereza waliokuwa kizingiti kwa kuingia kwao katika fainali za mwaka 2007. Katika fainali za mwaka 2003 Ufaransa ilifanikiwa kwa mgongo wa Uingereza . Nahodha wa zamani wa Ufaransa, Sandrine Soubeyrand, amesema kuwa watajaribu kuweka kando jazba dhidi ya majirani zao hao.

Nae mshambuliaji wa Japan, Yuki Nagasato, anakataa kukatishwa tamaa na mchezo wa robo fainali kati ya timu yake na wenyeji, Ujerumani. ambao ni mabingwa watetezi leo jioni. Ujerumani inawania kulinyakua tena kombe hilo kwa mara ya tatu na wanakumbana na Japan ili kuwania tikiti ya kuingia katika nusu fainali mjini Wolfsburg, wakati mashabiki wengi watakuwa wakiishangilia timu hiyo ya nyumbani. "Nina shauku kubwa kupambana na Wajerumani . Nawafahamu vilivyo wachezaji wa Ujerumani, na ndivyo nitakavyoweza kuisaidia timu yangu kujitayarisha vizuri. Ujerumani ni timu kubwa na ngumu, lakini hiyo haina maana kuwa hawashindiki. Japan ilifanya vizuri katika kundi B na kupata ushindi dhidi ya New Zealand na Mexico kabla ya kubwagwa kwa mabao 2-1 dhidi ya Uingereza."

Lakini golikipa wa muda mrefu katika kikosi cha Ujerumani, Nadine Angerer, anafikiria kuwa utapatikana ushindi tu dhidi ya Japan, lakini ameonya dhidi ya kubweteka. Kocha wa Ujerumani, Silvia Neid, amemuweka kando nahodha Birgit Prinz katika ushindi wao wa mabao 4-2 dhidi ya Ufaransa katika mchezo wao wa mwisho wa kundi A baada ya kucheza chini ya kiwango katika michezo miwili. Lakini mchezaji huyo, mwenye umri wa miaka 33 ambaye atastaafu baada ya fainali hizi, amesema kuwa ana matumaini ya kurejea katika kikosi hicho.

"Wakati mwingine ni muhimu kufanya uamuzi, ambapo kwangu mimi pia si rahisi. Ukweli ni kwamba unakuja wakati unasema nafikiri sina uwezo tena, na pia hilo si rahisi kulifanyia uamuzi.",

Frauenfußball WM 2011 Deutschland vs Nigeria
Mchezaji wa Ujerumani Birgit Prinz akifumua mkwaju mbele ya wachezaji wa Nigeria katika mchezo wa kundi A .Birgit anamatumani ya kurejea uwanjani baada ya kukaa benchi kwa muda.Picha: AP

Na katika fainali za kombe la mataifa ya Amerika ya kusini ,Copa America Brazil ambayo iliyaanza mashindano hayo kwa sare ya bila kufungana na Venezuela, itajitupa tena uwanjani kumfukuza bundi aliyekaa katika paa lake, mara hii wakitiana kifuani na Paraguay. Katika mchezo mwingine Venezuela inaonyeshana kazi na Ecuador.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri : Othman Miraji