1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa iko vitani - Hollande

Mohammed Khelef17 Novemba 2015

Rais Francoise Hollande wa Ufaransa ametangaza kwamba nchi yake iko kwenye vita dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu kufuatia mashambulizi mjini Paris siku ya Ijumaa na kuapa kulishinda kundi hilo.

https://p.dw.com/p/1H6uH
Rais Francoise Hollande akihutubia mabaraza mawili ya bunge la Ufaransa siku ya Jumatatu (16 Novemba 2015).
Rais Francoise Hollande akihutubia mabaraza mawili ya bunge la Ufaransa siku ya Jumatatu (16 Novemba 2015).Picha: Reuters/Philippe Wojazer

Akihutubia mabaraza mawili ya bunge hapo Jumatatu jioni, Hollande alisema vikosi vya ulinzi vitaimarishwa na kutaundwa muungano wa kimataifa kudhibiti mipaka.

"Leo kuna haja ya kufanyika mashambulizi zaidi, na hicho ndicho hasa tunachokifanya. Tunatoa msaada zaidi kwa wale wanaopambana dhidi ya Daesh. Lakini tunahitaji kukusanya vikosi vyote ambavyo vinaweza kupigana kikwelikweli dhidi ya jeshi hili la magaidi, kwenye muungano mpana na wa kipekee, na hilo ndilo tunalodhamiria. Ni kutokana na hilo ndio maana siku za hivi karibuni nitakutana na Rais Obama na Rais Putin, kuunganisha nguvu na hivyo kufikia matokeo ambayo yalikuwa daima yakiakhirishwa."

Hii ni mara ya kwanza ndani ya miaka sita kwa mabaraza mawili ya bunge kuhutubiwa na rais kwa wakati mmoja na Hollande alisema Ufaransa imewahi kukumbwa na misukosuko mingi huko nyuma, na kwamba itasimama imara baada ya mashambulizi ya Paris.

Alitumia hotuba hiyo pia kutangaza kuongezeka kwa operesheni ya kijeshi nchini Syria, na pia pendekezo la kuongeza muda wa hali ya hatari kwa miezi mitatu zaidi, na mabadiliko ya katiba.

Hotuba ya Hollande ambayo ilijaa maneno makali lakini ya tahadhari, ilitaja dhamira ya kiongozi huyo kuwasilisha mswaada wa kurefusha muda wa hali ya dharura, iliyotangazwa mara tu baada ya mashambulizi ya hapo Ijumaa, kwa miezi mitatu zaidi, na pia pendekezo la mabadiliko ya katiba, kwa kile alichosema ni ulazima wa kuwa na nyenzo muafaka za kuzitumia bila ya kutangaza hali ya hatari.

Wakimbizi wasiostahiki wafukuzwe

Akigusia suala la wakimbizi wanaoingia barani Ulaya hivi sasa, suala ambalo limezidisha suintafahamu baada ya mashambulizi haya, Hollande alisema umefika wakati wa bara hili kuwatenganisha wakimbizi wa kweli na wale wasiokuwa na hadhi ya kuomba hifadhi na kuwafukuza, jambo ambalo linahitaji ulinzi madhubuti wa mipakani kwenye mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Ndege ya kijeshi ya Ufaransa ikielekea kwenye mashambulizi dhidi ya IS nchini Syria.
Ndege ya kijeshi ya Ufaransa ikielekea kwenye mashambulizi dhidi ya IS nchini Syria.Picha: picture alliance/dpa/Ecpad Handout

Katika hatua nyengine, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali mashambulizi hayo ya Paris lililoyaita ya "kikatili" na ya "kijoga".

Wajumbe wa Baraza hilo walisimama kwa muda wa dakika moja kuwakumbuka watu 132 waliouawa kwenye mashambulizi hayo ya Ijumaa, na baadaye rais wa sasa baraza hilo, Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa, Peter Wilson, alisoma tamko la pamoja akisema wako tayari kushirikiana na Ufaransa.

"Tuko tayari kuisaidia Ufaransa kwa namna yoyote ambayo nchi hiyo inataka kwa kutumia urais wetu kwenye Baraza la Usalama kuchukua hatua kwa namna ambayo itaisaidia Ufaransa na kuwasaidia wengine ambao ni wahanga wa mashambulizi haya ya kigaidi."

Katika hatua nyengine, Ufaransa imesema inatuma meli yake ya kubebea ndege za kivita kwenye Bahari ya Mediterrania, kuimarisha operesheni yake dhidi ya wapiganaji wa Dola la Kiislamu nchini Syria.

AFP/Reuters