1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

UEFA-EURO 2012

Ujerumani kuumana na Ureno katika mechi ya kwamza ya fainali za kombe la mataifa ya Ulaya .

Kikosi cha Ujerumani

Kikosi cha Ujerumani

Mashindano ya kombe la mataifa ya Ulaya -UEFA EURO 2012 yalioanza rasmi Ijumaa (08.09) yanaingia siku ya pili Jumamosi kwa pambano kati ya Uholanzi na Denmark. Uholanzi ina kiu cha kutawazwa tena mabingwa tangu ushindi wao wa 1988.Pambano hilo litafuatiwa na lile kati ya Ujerumani na Ureno baadae usiku. Timu hizo ziko katika kundi B ambalo linatajwa kuwa gumu.

Itakumbukwa baada ya mechi mbili za kujipima nguvu kabla ya mashindano haya , ile dhidi ya Uswisi ambapo kikosi cha majaribio cha Ujerumani kilitandikwa mabao 5-3 mjini Basel kabla ya kushinda pambano la pili la kirafiki la kujipima nguvu dhidi ya Israel 2-0, Kocha Joachim Loew aliungama kwamba kunahitajika marekebisho katika kikosi chake, licha ya kwamba pambano dhidi ya Uswisi liliwakosa wachezaji wanane nyota kutoka kilabu ya Bayern Munich waliokuwa mapumzikoni .

Loew amesema lengo lao ni kufika fainali na kunyakua ubingwa mjini Kiev Julai mosi ,baada ya kuukosa chupuchupu 2008 na 2011. Mara ya mwisho kulitwaa kombe hilo ilikuwa miaka 16 iliopita wakati mashindano hayo yalipofanyika England.

Pamoja na matumaini yake Kocha wa Ujerumani ambaye anawania kulitwaa taji lake la kwanza na timu ya taifa anakiri kwamba kundi lao zikiwemo Ureno, Denmark na Uholanzi ni gumu, Kikosi chake safari hii kina wachezaji vijana kabisa kuwahi kuonekana katika mashindano ya Kombe la mataifa ya Ulaya kwa miaka 16 iliopita. Kwa mfano Sami Kader anayelisakata dimba katika kilabu ya Real Madrid ya Uhispania ana miaka 24 tu na ni mchezaji mwenye umri mdogo katika timu hiyo ya Ujerumani.

Kader ataungana na mchezaji mwenzake wa Real, Mesut Özil na mchanganyiko wa wachezaji nyota wa Bayern Munich na mabingwa wa soka nchini Borussia Dortmund. Kwa jumla Loew anasema vijana wake wamejiandaa vizuri. Ujerumani imeweka rekodi ya kulitwaa kombe la mataifa ya Ulaya mara tatu, 1972, 1980 na 1996 .

Matumaini ya Ureno:

Kwa upande wa timu ya Ureno, mahasimu wa Ujerumani leo usiku, Kocha Paulo Bento anatarajiwa kuhakikisha ngome yake ya ulinzi inakuwa makini mbele ya Ujerumani na pia Uholanzi na Denmark. Katika kikosi chake wamo kina Cristiano Ronaldo, Fabio Coentrao, Pepe na Miguel Lopes.

Bento anajuwa anakibarua kigumu hasa baada ya kufungwa Uturuki wiki iliopita katika mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu mabao 3-1 .

Timu ya Ureno EURO-2012

Timu ya Ureno EURO-2012

Ureno bado ina kiwewe cha kushindwa nyumbani mjini Lisbon na Ugiriki katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya 2004 na Ugiriki kutawazwa mabingwa . Katika matukio na viroja vya kabla ya mashindano haya kuanza jana, shabiki mmoja wa soka kutoka Ureno aliwasili Poland kwa baiskeli akiwa amesafiri kilomita 3,600, kuonyesha mshikamano na timu yake ya nyumbani .Bila shaka shabiki huyo Jorge Franco aliyesafiri kutoka Palmela karibu na mji mkuu wa Ureno Lisbon wiki saba zilizopita, analisubiri kawa hamu pambano la leo dhidi ya Ujerumani .

Kundi C:

Jumapili katika kundi C, Uhispania mabingwa wa dunia wataumana na Italia , wakati Ireland itatoana jasho na Kroatia. Kroatia iliwasili Poland bila ya mshambuliaji wake Ivica Olic ambaye ameumia. Akiulizwa timu yake itakuwaje bila ya Olic, kocha Slaven Bilic alisema ni vigumu kumpata mchezaji kama yeye ni sio tu nchini Kroatia, lakini alirejea tena , “ kama nilivyowaeleza wachezaji wangu, lengo letu linabakia lile lile , nalo ni ushindi.” Alisema kocha huyo.

Taarifa nyengine :

Tukiondoka katika fainali hizo za kombe la mataifa ya Ulaya, UEFA -Euro 2012- tuzigeukie taarifa nyengine. Kilabu ya Real Zaragoza ya Uhispania imemtunukia kocha wake Manolo Jimenez mkataba mwengine wa miaka mitatu, baada ya kunusurika kushuka daraja msimu uliopita. Taarifa ya kilabu hiyo ya ligi kuu ya Uhispania-La Liga, imesema uamuzi huo unatokana na mafanikio yaliopatikana baada ya Jimenez kushika uongozi kutoka kwa kocha aliyemtangulia Javier Aguire kutoka Mexico mwezi Desemba na kuweza kuwaondoa katika janga la kushuka daraja la pili. Jimenez ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Uhispania na aliwahi kuwa mchezaji na Kocha katika kilabu ya Sevilla, ambako baadae alipandishwa kuchukuwa nafasi ya Juande Ramos mwaka 2007. Mwaka jana 2011 aliiongoza AEK Athens ya Ugiriki kulitwaa kombe la taifa la nchi hiyo.

Afrika na kombe la dunia 2014:

Barani Afrika, timu ya taifa ya Afrika kusini Bafana Bafana , imemfukuza kocha wake Pitso Mosimane, baada ya kuanza vibaya katika kinyan'ganyiro cha kutafuta nafasi ya kushiriki katika fainali za kombe la dunia , ilipotoka sare nyumbani dhidi ya Ethiopia bao 1-1 mwishoni mwa juma lililopita. Uamuzi wa kumfukuza Mosimane ambaye ni kocha wa kwanza kufikwa na masahibu hayo barani Afrika katika kampeni ya kuelekea fainali za kombe la dunia Brazil, ulitolewa Jumanne na chama cha kandanda mjini Johannesburg. Nafasi ya Mosimane sasa itajazwa na naibu wake Steve Komphela, Afrika Kusini inateremka uwanjani Jumamosi hii kwa pambano la pili la kinyan'ganyiro hicho dhidi ya jirani yake Botswana. Afrika Kusini itasherehekea miaka 20 ya kurudi tena katika kandanda la kimataifa hapo mwezi ujao ambapo katika kipindi hicho, imekuwa na makocha 15 .

Zambia nayo itacheza nyumbani dhidi ya Ghana katika kinyan'ganyiro cha kuwania nafasi ya fainali za kombe la dunia 2014. Mwishoni mwa juma lililopita timu hiyo ya taifa ya Zambia Chipolopolo ambao ni mabingwa wa Afrika ilianza kwa mkosi ilipojikuta ikifungwa na Sudan mabao 2-0. Ghana nayo ikaiadhibu vibaya Lesotho mabao 7-0 mjini Maseru, pambano lilikumbwa na matatizo ya kuzimika kwa taa uwanjani. Jumapili June 10 Tanzania nayo itaumana na Gambia, ikiwa na kibarua kigumu baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Cote d´Ivoire wiki moja iliopita mabao 2-0 .

Kagawa asajiliwa Uingereza:

Mshambuliaji wa kimataifa wa Japan Shinji Kagawa anajiandaa kujiunga na Manchester United ya Uingereza baada ya kusaini mkataba na miamba hiyo wiki hii. Maafisa wa Manchester United au MANU kama wanavyojulikana wamethibitisha kwamba, yamefikiwa makubaliano na mabingwa wa Ujerumani Borussia Dortmund na kwamba taratibu zitakazofuata ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa afya zinatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.

Kagawa akifurahi bao

Kagawa akifurahi bao

Kagawa mwenye umri wa miaka 23 ni mchezaji wa kiungo mshambuliaji, na aligharimu euro 350.000 tu alipojiunga na Dortmund kutoka kilabu ya ligi ya Japan ya Cerezo ya mjini Osaka mwaka 2010. Amefunga mabao 21 katika mechi 49 za Bundesliga alizocheza akiwa na Borussia na kuchangia katika kuyatwaa mataji mawili ya Ujerumani mwaka huu- Ubingwa wa ligi kuu na kombe la taifa la shirikisho la kandanda la Ujerumani –DFB.

Mwandishi : Mohammed Abdul-Rahman/afp,rtr,dpa

Mhariri: Mohamed Dahman

 • Tarehe 09.06.2012
 • Mwandishi Mohamed Abdulrahman
 • Maneno muhimu UEFA-EURO 2012
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/15BJI
 • Tarehe 09.06.2012
 • Mwandishi Mohamed Abdulrahman
 • Maneno muhimu UEFA-EURO 2012
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/15BJI