1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi wa Afrika bado uko makini

7 Februari 2012

Wakati viongozi wa nchi za Ulaya wanahudhuria mkutano mmoja baada ya mwingine juu ya mgogoro wa kiuchumi unaoikumba Kanda ya Euro, viongozi wa Kiafrika bado wana ahueni kutokana na madhara ya mgogoro huu.

https://p.dw.com/p/13yPV
Viongozi wa kundi la G20
Viongozi wa kundi la G20Picha: dapd

Uchumi wa Afrika unatarajiwa kukua kwa kiwango cha kuridhisha mwaka huu. Lakini hii si sababu ya wao kujisahau kwa sababu endapo mgororo huu utakuwa mbaya zaidi, Afrika pia itaathirika.

Habari njema ni kwamba: Matarajio ya uchumi kwa Afrika yanatia matumaini. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Uchumi wa Afrika utakuwa kwa asilimia tano mwaka huu. Ikilinganishwa na Ulaya: Wakala wa viwango Standard & Poor's unabashiri ukuaji wa ongezeko la asilimia moja katika ukanda wa Euro. Lakini endapo kiwango hicho kitashuka zaidi, Afrika itaumia pia.

"Endapo uchumi wa Ulaya utanywea na kwa sababu moja uwezo wa kununua miongoni mwa mataifa ya OECD kuathiriwa na mgogoro huu, nchi za Afrika zenye uhusiano wa karibu kiuchumi na Ulaya zitaumia zaidi. Kushuka kwa asilimia moja katika ukuaji wa uchumi wa Ulaya kutasababisha kushuka kwa uchumi wa nchi zote za Afrika kwa nusu asilimia". Anasema Desire Vencatachellum Mkurugenzi wa Programu ya Utafiti wa Maendeleo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, mjini Tunis.

Tatizo ni kuwa nchi nyingi za Afrika bado zinategemea uchumi wa kuuza nje mali ghafi kama vile chuma, makaa ya mawe au mafuta. Na bidhaa zao nyingi huuzwa Ulaya na Marekani na endapo mahitaji huko yatapungua kutokana na kushuka kwa uchumi, bei zitashuka pia kwenye soko la dunia.

Viongozi wa mataifa yanayoinukia kiuchumi ya BRICS
Viongozi wa mataifa yanayoinukia kiuchumi ya BRICSPicha: AP

Kwa bahati nzuri, bei hizi hazitarajiwi kushuka kwa kiwango kikubwa kama ilivyotokea huko nyuma kwa sababu kuna wadau zaidi. China na India zinanunua bidhaa za Afrika kwa wingi lakini nazo pia zinaweza kuathiriwa na mgogoro huu.

"Katika kipindi cha muda mrefu, mambo yanaweza kuwa magumu kwa sababu hata China na India nazo zinategemea kukua kwa uchumi wa Ulaya ziweze kuuza bidhaa zake. Kwa hiyo endapo na hizo zitaathirika, soko la bidhaa za Afrika litaathirika pia". Anasema Anver Vasi, Mhariri wa Jarida la Africa Business.

Katika mataifa hayo ya Kanda ya Euro kwa hivi sasa macho yote yako nchini Ugiriki, ambako viongozi wa taifa hilo wanapaswa hadi kufikia wiki ijayo kuamua ikiwa wanasaini makubaliano ya mfuko wa uokozi barani Ulaya ili ijikwamuwe kutoka kwenye madeni yanayoizonga ama ifilisike.

Mwandishi: Daniel Pelz/DW
Tafsiri: Ismail Iddi
Mhariri: Saumu Yusuf