1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi kuimarishwa kati ya Arabuni na Afrika

18 Novemba 2013

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu na za Kiafrika wamekutana Kuwait Jumapili (17.11.2013) kuharakisha mkakati wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi,uwekezaji na biashara kabla ya kuanza kwa mkutano wa kilele.

https://p.dw.com/p/1AJNn
Bendera za nchi za Kiafrika.
Bendera za nchi za Kiafrika.Picha: AP

Mkutano wa Tatu wa Kilele wa viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiafrika hapo Jumanne na Jumatano utakuwa mkutano wa kwanza wa aina yake kufanyika tokea mwaka 2010 ambapo viongozi hao walikutana nchini Libya kabla ya kuzuka kwa vuguvugu la uasi wa majira ya machipuko katika nchi za Kiarabu lililopinduwa tawala za kidikteta zilizokuwa zimedumu kwa muda mrefu huko Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati.

Mkutano huo wa siku moja ulikuwa umepangwa kuandaa agenda ya mkutano huo wa kilele ambapo viongozi wanatarajiwa kuidhinisha hatua mpya kadhaa za kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya kanda hizo mbili ikiwa ni pamoja na eneo la Ghuba lenye utajiri wa mafuta na eneo la kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika.

Wakati umefika kwa utekelezaji

Waziri wa mambo ya nje wa Kuwait Sheikh Sabah Khaled Al-Sabah amekiambia kikao cha ufunguzi kwamba wakati umefika wa kuimarisha na kutekeleza mradi wa pamoja kati ya Arabuni na Afrika kuwahudumia watu wa kanda hizo mbili.Sheikh Khaled amewaambia waandishi wa habari kwamba mkutano huo utakaofanyika chini ya jina la "Washirika katika Maendeleo na Uwekezaji" unatarajiwa kujadili uwezekano wa kuanzisha soko la pamoja kati ya Arabuni na Afrika.

Amir wa Kuwait Amir Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah ambaye nchi yake ni mwenyeji wa mkutano wa Kilele wa Arabuni na Afrika.
Amir wa Kuwait Amir Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah ambaye nchi yake ni mwenyeji wa mkutano wa Kilele wa Arabuni na Afrika.Picha: Getty Images

Wakuu wa nchi thelathini na nne, makamo wa rais saba na viongozi watatu wa serikali wamethibitisha kushiriki mkutano huo wa kilele ambao utazijumuisha nchi 71 na mashirika.

Machafuko yaathiri utekelezaji

Mkutano wa pili wa kilele uliofanyika nchini Libya miaka mitatu iliopita uliidhinisha Mkakati wa Ushirikiano kati ya Arabuni na Afrika na Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji kwa mwaka 2011 hadi 2016 wa kuongeza uwekezaji, biashara na miradi mengine ya kiuchumi kati ya kanda hizo mbili.

Aliekuwa kiongozi wa Libya Moamer Gaddafi (kushoto) na aliekuwa Rais wa Tunisia Zine el-Abidin Bin Ali ambao wote wameangushwa madarakani wakati wa vuguvugu la machipuko la Kiarabu.
Aliekuwa kiongozi wa Libya Moamer Kadhafi (kushoto) na aliekuwa Rais wa Tunisia Zine el-Abidin Bin Ali ambao wote wameangushwa madarakani wakati wa vuguvugu la machipuko la Kiarabu.Picha: M. Naamani/AFP/Getty Images

Lakini utekelezaji ulikuwa ukisua sua kwa kiasi fulani kutokana na machafuko yaliozuka katika eneo zima la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kufuatia vuguvugu la Kiarabu la majira ya machipuko hapo mwaka 2011 ambalo limesababisha kuangushwa kwa viongozi wa Tunisia,Libya,Misri na Yemen kutokana na maandamano makubwa ya umma na kuzuka kwa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi za Kiarabu na Afrika pia waliangalia upya pendekezo la Utaratibu wa Pamoja wa Kifedha kati ya Arabuni na Afrika kufunguwa njia zinazohitajika katika utekelezaji wa miradi na kushajiisha uwekezaji.Pia watajadili kuanzishwa kwa Kamati ya Ufundi na Uratibu kuhusu Uhamiaji kati ya Arabuni na Afrika ili kusaidia kuwalinda wafanyakazi wahamiaji.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Yusuf Saumu