Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 06.11.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

Mada kuu iliyoshughulikiwa na magazeti mengi ya Ujerumani leo hii ni adhabu ya kifo iliyotolewa kwa kiongozi wa zamani wa Irak Saddam Hussein, kuhusika na mauaji ya Washia katika mwaka 1982.

Kwa maoni ya HEILBRONNER STIMME,Saddam Hussein hastahili kuonewa huruma.Likiendelea linasema, kilicho dhahiri kwa wote,yaani wale wanaopinga na wanaounga mkono adhabu ya kifo ni kwamba dikteta wa zamani wa Irak aliwatesa vibaya mno wananchi wake na hivyo anapaswa kuwajibika kwa kila njia. Juu ya hivyo jumuiya ya kimataifa haina sababu ya kuridhika na adhabu ya kwanza iliyotolewa kwa kiongozi wa zamani wa Irak.Kwa maoni ya Heilbronner Stimme,kutofanikiwa kwa serikali nchini Irak kumedhihirika waziwazi.Lakini hatumo katika hali ya kuwa kama polisi wa kimataifa kukomesha udikteta na kuleta amani ya kudumu.

Na gazeti la HANDELSBLATT kutoka Düsseldorf linasema:

Hilo ni tukio lisiloweza kusadikiwa katika nchi iliyoshuhudia utawala wa kidhalimu kwa karne kadhaa.Saddam ambae hapo zamani alijikweza kwa vitendo vyake,ameonekana akinywea kuwa mtu wa kawaida mbele ya mahakama.Mtu anaweza kusema kuwa hilo peke yake,limeifanya kesi hiyo kuwa na maana.Utaratibu huo lakini,unapaswa kuchukua hatua nyingine tena.Kwani baada ya Washia,sasa Wakurd pia wapewe nafasi ya angalao kufungua kesi kuhusika na uhalifu waliotendewa.

WESTDEUTSCHEN ALLGEMEINEN ZEITUNG kutoka Essen likiendelea na mada ya adhabu iliyotolewa kwa Saddam Hussein linasema:

Ikiwa mtu anaunga mkono au anapinga adhabu ya kifo iliyotolewa kwa Saddam Hussein ni uamuzi wa binafsi.Kilicho hakika ni kuwa Irak imefunga ukurasa mmoja wa kihistoria.Saddam Hussein aliesababisha huzuni na maumivu makubwa nchini mwake sasa amelazimishwa kuwajibika kwa vitendo vyake.Huo ni upande mzuri wa tukio hilo.Mbaya ni kwamba adhabu hiyo haitokomesha wimbi la machafuko na wala haitoleta muungano.Hayo hayakutokea hata Saddam Hussein alipokamatwa au wanae wawili wa kiume walipouawa.”

Sasa hebu tugeukie mada nyingine ilioshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani.Jumamosi jioni katika baadhi ya maeneo nchini Ujerumani na sehemu zingine za Ulaya ya Magharibi,umeme ulikosekana kwa takriban saa moja nzima.Inadhaniwa kuwa tatizo hilo limesababishwa na kinu cha nishati huko Elmsland.Magazeti ya leo yanasema hapa kuna umuhimu wa kufanywa mazungumzo juu ya sera na utekelezaji wa mahitaji ya nishati.

Kwa mfano gazeti la WESTFÄLISCHEN NACHRICHTEN kutoka Münster linaeleza hivi:

Ujerumani inahitaji kuwa na uhakika wa kupata nishati na lazima iweze kutegemea uwezo wa makampuni makubwa ya nishati kama vile Eon,RWE na kadhalika kutekeleza mahitaji ya nchi.Baada ya umeme kukatika katika maeneo mengi,kuna fikra inayowavunja moyo wateja kwamba sekta ya nishati, inashughulika kunufaika kifedha lakini kuna kasoro katika uwekezaji kwenye mfumo wa nishati na teknolojia lamalizia Westfällischen Nachrichten.