1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin29 Novemba 2006

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wametupia jicho ziara ya Baba Mtakatifu Benedikt XVI nchini Uturuki.Mkutano mkuu wa chama cha CDU mjini Dresden ni mada nyingine iliyoshughulikiwa.

https://p.dw.com/p/CHUK

Gazeti la HANDELSBLATT la mjini Düsseldorf likiandika juu ya ziara ya Papa Benedikt linasema:

Hatimae,Baba Mtakatifu Benedikt XVI na waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wamepeana mkono.Mkuu wa Wakatoliki duniani na kiongozi wa chama cha kiislamu chenye siasa za wastani wamezungumza kuhusu dini na dunia.Hiyo ni hatua muhimu.Wote wawili wameonyesha ujasiri:kwani Benedikt XVI kufuatia matamshi yake kuhusu Uislamu,yalioeleweka visivyo amekwenda kwa wakosoaji wake.Erdogan nae alikutana na Papa,ingawa hapo awali mkutano huo ulifutwa kwa sababu ya upinzani wa kisiasa uliozuka nchini Uturuki kuhusu ziara ya Papa.Kwa kufanya hivyo ametoa ishara kwa jumuiya ya Kituruki na Ulaya vile vile.

Gazeti la WIESBADENER KURIER likiendelea na mada hiyo linasema:

“Moto usichochewe,lakini ile kasoro ya Uturuki kuwa na ustahmlivu itajwe;huo zaidi ni mwito wa wanadiplomasia kuliko huyo kiongozi wa kanisa. Atakapokutana na Askofu Mkuu Bartholomew wa Wakristo wa Ki-orthodox,Papa Benedikt atakuwa na nafasi ya kushuhudia vipi jamhuri ya Kiislamu ya Uturuki inavyoishi na Wakristo walio wachache na hivyo kulizungumzia wazi wazi jambo hilo.Ikiwa makanisa hayatambuliwi na hakuna mafunzo ya upadri yanayotolewa,hapo mtu hawezi kuzungumzia uhuru wa dini kama Papa Benedikt alivyopendekeza wakati wa siku ya kwanza ya ziara yake.”

Kwa maoni ya gazeti la NEUE WESTFÄLISHE kutoka Bielefeld:

“Papa Benedikt alijitokeza kama mwanadiplomasia na kwa njia hiyo alijua kuwasadikisha wakosoaji wake nchini Uturuki.Papa alisisitiza ujumbe wa dini zote mbili,yaani kuna Mungu mmoja tu.Hilo linafungamanisha mielekeo ya imani za dini hizo mbili dhidi ya wale wasio na dini.”

Sasa ndio tunatupia jicho mada nyingine.Gazeti la ABENDZEITUNG mjini Munich likieleza juu ya mkutano wa chama cha CDU mjini Dresden linasema:

“Merkel asijiachie kubabaika kwa vile amechaguliwa tena kama kiongozi wa chama.Yeye amenufaika kutokana na mivutano ya viongozi wa mikoa walioutumia mkutano wa chama kutoa dukuduku lao.Imedhihirika kuwa Merkel kama Kansela wa serikali ya muungano mkuu,hawezi kuongoza kwa mamlaka.Na kama kiongozi wa chama akifuata mkondo wa kati usioueleweka badala ya kuwa na mkondo dhahiri kama vile Stoiber,ni jambo linalovunja moyo.Chama cha CDU kitakuwa na shida kama kitakuwa sawa na pakacha ambamo kila kitu huweza kutumbukizwa.” Hayo ni maoni ya ABENDZEITUNG kutoka Munich.

Lakini gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE huko Potsdam linaeleza hivi:

“Kinyume ni inavyokosolewa sana,mkondo unaofuatwa na chama cha CDU na Kansela ni wazi;yaani hakuna mabadilisho yatakayofanywa kuhusu malipo yanayotolewa kwa wakosa ajira na pia njia ile ile ya mageuzi iliyokubaliwa katika mkutano wa mwisho wa chama ndio inafuatwa.Matamshi ya Merkel kuhusu uchumi mpya wa kijamii duniani,huonyesha kuwa juhudi za kuzuia hofu na hisia za kujikinga husababisha hali ya kutobainika.Uchumi wa kijamii wa zamani umeongeza mzigo wa taifa la kijamii na mara nyingi hushindwa kuwasaidia wale wanaohitaji kweli kusaidiwa.Na Merkel hajiachili kuingia katika mapambano kwani matokeo yake hayawezi kutabiriwa.Huo ndio ukweli wa hali na hadi hivi sasa amefanikiwa,lamalizia gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE.