1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa Magazeti ya Ujerumani

P.Martin8 Oktoba 2007

Magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu hasa yameshughulikia mvutano uliozuka kuhusu malipo ya ukosefu wa ajira,kwa watu wazima.

https://p.dw.com/p/C7lU

Wakati kiongozi wa chama cha SPD,Kurt Beck akipendekeza kuwa watu wazima wasio na ajira walipwe pesa kwa muda mrefu zaidi,waziri wa ajira Franz Münterfering ambae pia ni Naibu Kansela,kwa mara nyingine tena amelipinga pendekezo hilo.

Tuataanza na NÜRNBERGER NACHRICHTEN linalomlaumu Beck kuwa anarejea kwenye makosa ya zamani:Linasema;

Ndio kwanza uchumi wa nchi umeanza kustawi na yeye tayari anataka kugawa pesa.Badala ya kueleza mafanikio ya mageuzi yaliyofanywa na serikali iliyopita ya SPD na chama cha Kijani na hivyo kushikilia kuendelea na mwendo huo,yeye anataka kujitenga na mageuzi yaliyoanzishwa na kansela wa zamani Schroeder na Münterfering.Mageuzi hayo yanayojulikana kama Ajenda 2010 yanaungwa mkono hata na waziri wa fedha Peer Steinbrück na waziri wa nje Frank-Walter Steinmeier.

Hata gazeti la MÄRKISCHEN ALLGEMEINE kutoka Potsdam linamuunga mkono Münterfering.Linamtetea Münterfering kwa kusema hivi: Msoshialdemokrat huyo aliebobea,hatetei Ajenda ya Mageuzi kwa sababu anataka kuzuia haki za wakosa ajira,bali kwa vile hiyo ni njia iliyo barabara.

Likiendelea,MÄRKISCHE ALLGEMEINE linasema: Inahamakisha kuona kuwa mawaziri wa nje na wa fedha wanaounga mkono ajenda hiyo hawajitokezi waziwazi kueleza maoni yao.Hata Kansela Angela Merkel katika hotuba yake ya siku ya Jumapili alisifu ujasiri wa serikali iliyopita kufanya mageuzi hayo,lakini amekwepa kueleza msimamo wake kinagaubaga.Linaongezea kuwa katika siasa,kuna wakati ambapo mtu analazimika kusimama wima na kutetea waziwazi kile kinachopaswa kutekelezwa kama afanyavyo Münterfering.

Lakini si magazeti yote yanayomuunga mkono Münterfering kwani kwa maoni ya BERLINER ZEITUNG, mwanasiasa huyo hajiichimbii tu kaburi lake,bali atasababisha chama chake kuangukia upande wa upinzani.BERLINER ZEITUNG linaonya,chama cha SPD kinapaswa kuwa na tahadhari ili kisije kuzama katika mivutano ya madaraka na kulaumiana.Au sivyo,chama cha CDU kwa haki kitakitazama chama cha SPD kama mshirika asieweza kutegemewa. Likiendelea BERLINER ZEITUNG linasema,

„Daima Münterfering amesisitiza kuwa SPD lazima kihifadhi uwezo wake wa kufanya marekebisho. Lakini sasa yadhihirika kuwa yeye ndio anaehatarisha kukisambaratisha chama hicho.Na Kurt Beck nae anazidi kuchochea moto.

Hata gazeti la HANDELSBLATT kutoka Düsseldorf linaamini kuwa uwezo wa kuongoza wa chama cha SPD upo hatarini.Kwa maoni ya gazeti hilo,chama cha SPD kipo mbioni kukanusha siasa zake zenyewe.Kiongozi wa chama hicho,Kurt Beck katika jitahada ya kuwavutia tena wapiga kura waliokimbilia chama cha Linkspartei,hatilii maanani uwezo wa chama chake kushiriki serikalini,seuze kumfikiria makamu wa Kansela Münterfering.