Uchambuzi wa Magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 24.10.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Uchambuzi wa Magazeti ya Ujerumani

Mada kuu iliyoshughulikiwa hii leo ni uamuzi wa Mahakama ya Umoja wa Ulaya kuondosha sheria iliyoipa serikali ya jimbo la Niedersachsen haki maalum kama mmiliki hisa katika kampuni ya Volkswagen.

Sasa,kampuni ya Porsche inayotengeneza magari ya spoti,itakuwa na usemi zaidi kama mmiliki mkubwa wa hisa za Volkswagen.Gazeti la Die Welt linasema:“Hakuna tena vikwazo dhidi ya Porsche“Halafu linaeleza hivi:

Sasa sheria ya VW ni jambo la kale.Juu ya hivyo,hakuna mengi yatakayobadilika katika kampuni hiyo.Badala ya sheria iliyokuwa ikitetea maslahi ya VW,sasa mshindani wa awali Porsche, ndio itakayokuwa ikifanya bidii,kuhakikisha kuwa kampuni ya VW itaendelea kuwa nambari moja nchini Ujerumani.Porsche inayomiliki asilimia 50 ya hisa za VW,bila ya shaka sasa itaongeza idadi hiyo.Hapo basi jimbo la Niedersachsen litapaswa kujiuliza kuna maana gani tena kubakia katika kampuni hiyo.

Lakini gazeti la mjini Berlin DIE TAGESZEITUNG linasema:

Kwa maoni ya vyama vya wafanyakazi,maslahi ya masoko ya hisa yatapewa umuhimu zaidi kuliko yale ya wafanyakazi wanaotaka uhakika wa ajira na mishahara.Likiendelea linasema,Umoja wa Ulaya kwa kuipeleka Ujerumani mahakamani imeingilia kati utaratibu wa nchi mwanachama kuwa na uhuru katika siasa za kiuchumi.

Lakini gazeti la Düsseldorf,HANDELSBLATT linasema:

Kwa jumla,hukubaliwa kuwa serikali inapaswa kuwa na udhibiti fulani,ikiwa ni katika mawasiliano ya simu,ulinzi,nishati au usafiri na karibuni hata katika makampuni yanayohusika na teknlojia ya kisasa.Lakini ile sheria maalum kuhusu VW inapaswa kuwa somo kwa sote.Kwani,sheria hiyo haikuweza kuzuia kampuni ya VW kukaribia kufilisika.Wala haikuisaidia VW kuongoza katika masoko ya magari duniani.VW ipo katikati tu.Kwa maoni ya Handelsblatt hali hiyo itaweza kubadilika chini ya uongozi wa Porsche tu.

Lakini TAGESSPIEGEL naona kuwa lina shaka zake.Kwani linasema:

Ye yote anaefurahia kuwa Volkswagen kama sehemu ya Porsche mara itabadilika kuwa na muundo mwingine kabisa na kumimina pesa basi huyo amekosea.Kwani VW ni kampuni kubwa mno na pili asilimi 95 ya waajiriwa wa VW ni wanachama katika shirika la wafanyakazi wa viwandani IG-Metall. Vile vile uhusiano maalum uliopo kati ya waajiriwa na waajiri hautobadilika:uhusiano unaokutikana katika viwanda vyote vya kutengeneza magari.

Kwa kumalizia MÄRKISCHE ODERZEITUNG linasema:

Licha ya kulalamika kote kwa mabaraza ya wafanyakazi,kwa hofu ya kudhibitiwa na Porsche, hatimae kilicho muhimu kwa waajiriwa wa VW nchini Ujerumani,wapatao 180,000 ni idadi ya magari yatakayoweza kutengenezwa na kuuzwa kwa bei za kuweza kushindana katika masoko ya dunia.