1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa uchaguzi wa Ujerumani

Zainab Aziz
23 Septemba 2017

Septemba 24 mwaka huu macho yote yataiangalia Ujerumani katika uchaguzi wake mkuu ambapo panda shuka zimekuwa nyingi kuliko kawaida. DW inaangazia mchakato mzima wa uchaguzi wa bunge (Bundestag).

https://p.dw.com/p/2kZX0
Bayrischzell Wahllokal zur Bundestagswahl
Picha: Getty Images/L. Preiss

Ujerumani ina mfumo tata wa kupiga kura katika kulichagua  bunge lake "Bundestag”. Mfumo huo unajumuisha kuchaguliwa wajumbe moja kwa moja kutoka kwenye maeneo yao pamoja na kuvichagua vyama ambavyo vinawakilisha uwiano na wakati huo huo kuwa makini juu ya kutorudia makosa ya uchaguzi yaliyofanyika zamani hapa nchini Ujerumani, ambayo yalisababisha mgawanyiko wa kisiasa wakati wa Jamhuri ya Weimar kati ya vita vya kwanza na vya pili vya dunia. Zainab Aziz anatusomea ripoti ya Rebecca Staudenmaier.

Nani anaweza kupiga kura?

Uchaguzi wa bunge wa mwaka 2009 na 2013 ulikumbwa na kushuka kwa kiasi kikubwa cha wapiga kura hadi asilimia 70, lakini uchaguzi huo uligubikwa na ongezeko la harakati za makundi yanayolemea siasa za mrengo mkali wa kulia ambayo hupata ushawishi mkubwa wa watu ambao kwa kawaida huwa hawapigi kura katika majimbo yote. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa katika uchaguzi wa mwaka huu.

Kulingana na takwimu za Idara ya takwimu ya Ujerumani, mwaka huu, watu milioni 61.5 wenye umri wa miaka 18 na zaidi watashiriki katika zoezi la kupiga kura kwenye uchaguzi wa kitaifa.

Deutschland Bundestagswahl Angela Merkel in Freiburg
Kansela Angela Merkel anatafuta muhula wa nne madarakani.Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Kati ya hao, wanawake ni milioni 31.7 na milioni 29.8 ni wanaume. Takriban watu milioni 3 wanatarajiwa kupiga kura kwa mara ya kwanza. Vile vile zaidi ya theluthi tatu ya wapiga kura wa Ujerumani milioni 22  wana umri wa miaka 60 na zaidi hii ikiwa na maana kwamba kizazi cha wazee mara nyingi kina usemi mkubwa katika matokeo ya uchaguzi.

Idadi kubwa ya wapiga kura wanaishi katika jimbo la magharibi la North Rhine Westphalia jimbo hilo lina takriban wapiga kura milioni 13.2 likifuatiwa na jimbo la kusini la Bavaria lenye wapiga kura milioni 9.5 halafu jimbo la Baden-Württemberg lililo na wapiga kura milioni 7.8. Mpiga kura anastahili kuwachagua wagombea wawili katika zoezi la kura nchini Ujerumani. Uchaguzi umegawanywa katika mafungu mawili. Sanduku la kupigia kura la kwanza ni jeusi na sanduku la pili ni la rangi ya bluu. Kila sanduku linawakilisha kura moja kwa mgombea au kwa chama cha siasa. Mpiga kura anapiga kura mbili, moja kwa mgombea na moja kwa ajili ya chama.

Kugawanya kura

Wakati Wajerumani watakapokuwa wanapiga kura kwenye uchaguzi wa tarehe 24 mwezi wa Septemba, kila mpiga kura atachagua mara mbili, yaani kura moja ya mwakilishi wa wilaya na moja kwa ajili ya chama.

Vita ya kwanza ya mwakilishi wa wilaya, inafuata mfumo wa kwanza wa uchaguzi kama ule wa Marekani. Mpiga kura huchagua mgombea wake anayependa ambaye ataiwakilisha wilaya yao katika bunge. Kila mgombea ambaye atafanikiwa kushinda katika mojawapo ya majimbo 299 ya Ujerumani atakuwa na uhakika wa kupata kiti hicho cha uwakilishi bungeni ambao unagawanywa kwa kila wakazi 250,000.

Merkel aliteuliwa kuwa mgombea wa moja kwa moja

Ili kujaza nusu nyingine ya viti 598 katika bunge la Ujerumani "Bundestag”, wapiga kura watapiga kura zao katika kura ya pili na kura hii ni ya kuchagua chama cha siasa badala ya mgombea mmoja pia huamua kila chama cha siasa kinapata asilimia ngapi katika bunge. Majimbo ya Ujerumani yenye idadi kubwa ya watu bila shaka huwa na nafasi nzuri ya kuwapeleka wawakilishi zaidi bungeni.

Bundestagswahl 2017 | SPD - Martin Schulz, Kanzlerkandidat
Mpinzani mkuu wa Merkel katika uchaguzi wa mwaka huu Martin Schulz.Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/TF-Images

Kwa nini uchaguzi wa nchini Ujerumani huvutia?  Ni kwa sababu wapiga kura wanaruhusiwa kugawa kura zao wanavyopenda wao kati ya vyama, kwa mfano kumpigia kura ya kwanza mgombea wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, wa ndani katika kura ya kwanza, lakini akampigia kura mgomea wa chama cha FDP katika kura ya pili kwa ajili ya kukisaidia chama kidogo mshirika wa jadi wa chama cha CDU ili kiweze kuingia bungeni.

'Viti vya ziada'

Wakati mwingine, chama kinapata viti vya ziada vya bunge moja kwa moja katika kura ya kwanza na inapotokea hivyo basi chama kinafaidika kwa ziada hiyo ambayo hatimaye hufanya bunge kuwa kubwa zaidi kuliko viti vyake vya msingi ambavyo ni 598 na kutokana na hili, ndio maana kwa sasa kuna viti 630 katika bunge la Ujerumani.

'Kizuizi cha asilimia 5'

Ili chama kiweze kuingia bungeni, kinapaswa kupata angalau asilimia 5 ya kura ya pili. Mfumo huu uliwekwa ili kuvizuia vyama vidogo vidogo kuingia katika bunge kama vyama vilivyozuiwa kuingia bungeni chini ya Jamhuri ya Weimar katika miaka ya 1920. Kiunzi cha asilimia tano kimetumika kuviweka kando vyama, kama chama cha NPD chenye mrengo mkali wa kulia pamoja na vyama vingine vyenye mitazamo mikali.

Hivi sasa, kuna vyama vitano vinavyowakilishwa bungeni, Chama cha Kansela Angela Merkel cha CDU na chama ndugu cha Christian Social Union, CSU, Chama cha mrengo wa kushoto, Die Linke, chama Social Democratic, SPD na chama cha Kijani.

Chama kingine cha kuzingatia ni chama cha AfD maarufu kama chama Mbadala kwa Ujerumani kinachopinga wahamiaji. Chama hicho kilishindwa kuingia bungeni katika uchaguzi wa mwaka 2013 lakini tangu wakati huo, chama hicho kimeendelea kupata wafuasi sio tu kwa uwepo wake katika Bunge la Ulaya, lakini pia katika majimbo 13 kati ya majimbo 16 ya Ujerumani.

Kielelezo hiki kinaonyesha matokeo ya uchaguzi ya chama cha AfD kuanzia mwaka wa 2013 hadi 2017. Chama cha AfD kiliweza kupata kura nyingi katika jimbo la Saxony-Anhalt mwaka 2016 ambapo kilipata asilimia 24.3.  Na katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2017 huenda chama hicho kikapata kati ya asilimia 4 hadi 20 kote katika majimbo yote ya Ujerumani.

DW Pan-Africa “Germany Decides”
Timu ya waandishi wa maripota wa idhaa za Kiafrika iliofuatilia kampeni za uchaguzi katika eneo la mashariki mwa Ujerumani.Picha: DW/U. Shehu

"Kansela huchaguliwa na nani”?

Tofauti na mfumo wa urais nchini Marekani, wapiga kura nchini Ujerumani hawamchagui kansela moja kwa moja ambaye ndiye mkuu wa serikali. Bunge jipya linapaswa kukutana kwa mara ya kwanza mwezi mmoja baada ya zoezi la kupiga kura kumalizika.

Inawezekana kikao cha bunge kufanyika mapema ikiwa mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano wa vyama yatakuwa yamemalizika haraka. Mgombea mkuu kutoka kwenye chama ambacho kimefanikiwa kupata kura nyingi ndiye huwa na jukumu la kuunda muungano huo wa vyama katika kuunda serikali. Rais, ambaye ni mkuu wa serikali na ana jukumu kubwa la kiutendaji atampendekeza mshindi huyo kuwa mgombea wa ukansela, ambaye atapigiwa kura bungeni na wawakilishi wapya waliochaguliwa na hatimaye kuidhinishwa katika kura ya siri.

Ikiwa, kama katika chaguzi tatu ziliopita, chama cha CDU kitafanikiwa kupata kura nyingi basi mgombea wake wa ukansela Angela Merkel, atashika nafasi hiyo kwa miaka minne ijayo. Nchini Ujerumani hakuna kikomo cha mihula ya kansela anayopaswa kuwa madarakani. Lakini hadi sasa hakuna kansela aliyewahi kutumikia zaidi ya miaka 16 tangu wakati wa kansela wa zamani hayati Helmut Kohl.

Mwandishi:Zainab Aziz/Staudenmaier, Rebecca

Mhariri:Josephat Charo