1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Sierra Leone kufanyika siku ya Jumamosi

9 Agosti 2007

Licha ya kufutiwa madeni na kupokea msaada wa mabilioni ya dola, raia wengi nchini Sierra Leone wanakabiliwa na hali ya umasikini mkubwa. Wengi wao wanatarajia kuwa baada ya uchaguzi uliopangiwa kufanyika mwishoni mwa wiki kumalizika, huenda ukawa ndio sababu ya kuboresha hali ya maisha yao.

https://p.dw.com/p/CH9s
Rais Ahmad Tejan Kabbah wa Sierra Leone
Rais Ahmad Tejan Kabbah wa Sierra LeonePicha: dpa

Sierra Leone taifa dogo katika eneo la Afrika ya Magharibi ambalo bado limo katika hali tete lilikumbwa na muongo mmoja wa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyomalizika miaka sita tu iliyopita linatarajiwa kufanya uchaguzi wa urais na bunge siku ya jumamosi.

Takriban aslimia 70 ya wananchi wanaishi katika kiwango cha chini ya dola moja ya Marekani kwa siku licha ya kwamba nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa mali asili.

Mashirika ya kifedha yamekuwa na imani kubwa katika utendaji kazi wa serikali ya sasa ya nchi hiyo hali ambayo ilisababisha kufutiwa madeni ya zaidi ya dola bilioni moja nukta tano.

Mwaka 2006 shirika la fedha duniani IMF na benki ya dunia yalifuta madeni ya kisasi cha dola bilioni moja nukta sita. Pia Marekani na kundi la Paris la wafadhili limesamehe baadhi ya fedha zilizokuwa zikiidai Sierra Leone.

Nchi hiyo ya Kiafrika imepokea sifa nyingi kutoka kwa wafadhili wa kimataifa hasa kutokana na ufanisi mkubwa katika utendaji kazi wa serikali na vile vile matumizi mazuri ya fedha za misaada wakati ambapo taifa hilo linajikwamua taratibu kutoka kwenye kishindo cha vita vya mwaka1991hadi 2001.

Uchumi wa nchi hiyo unaonyesha muelekeo mzuri mwaka uliopita kiwango cha uchumi kiliongezeka kwa asilimia 7.5 na mfumuko wa gharama za maisha kufikia asilimia11,lakini raia wa kawaida nchini Sierra Leone wengi wao bado hali yao ya maisha ni duni na bado hawaelewi nini hasa maana ya kukua kwa uchumi wa nchi yao.

Watalaam wanasema lazima zifanyike jitihada za kutafuta mkakati wa kupambana na umasikini utakao lenga kuboresha hali ya maisha ya raia wa kawaida nchini Sierra Leone.

Muwakilihsi wa benki ya dunia nchini humo Engilbert Gudmundsson amesema hali ya usalama nchini humo imeimarika uzalishaji unakuwa kwa kiwango cha kuridhisha na hali ya kupatikana bidhaa pia inaimarika lakini hali ya maisha ya mwanachi wa kawaida ni ngumu mno.

Kundi linalo shughulikia mizozo ya kimataifa ICG lenye makao yake mjini Brussels nchini Ubelgiji limesema katika ripoti yake kwamba uchumi wa Sierra Leone una nafasi nzuri katika sekta za kilimo na migodi ambazo zikikuzwa vyema zitatosheleza kupunguza kiwango cha umasikini nchini humo. Kinachohitajika kwa sasa ni uchaguzi utakao waweka pamoja Wasierra Leone na wala sio kuwatenganisha.

Wachambuzi wanasema kwamba serikali mpya itahitajika kufikiria namna ya kuimarisha hali ya maisha ya kila siku kwa raia wake.

Waziri wa Fedha John Benjamin amesema mjini Free Town kwamba serikali ya sasa inahitaji muda zaidi ili kuuendelezaza msingi imara iliouanzisha na kwamba iwapo wanachi wataichagua tena serikali ya sasa basi bila shaka swala la kuupunguza umasikini lifanikiwa.