1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atamrithi Mwanawasa?

Mtullya, Abdu Said30 Oktoba 2008

Watu wa Zambia leo wanapiga kura kumchagua rais atakaechukua nafasi ya hayati Levy Mwanawasa aliefariki mnamo mwezi agosti.

https://p.dw.com/p/FkLM
Nani ataweza kushughulikia mustakabal wa watoto hao baada ya uchaguzi wa leo nchini Zambia?Picha: DW/Rottscheidt

Watu wa  Zambia  leo wanapiga kura kumchagua rais atakaechukua  nafasi ya hayati Levy Mwanawasa  aliefariki mwezi  agosti  kutokana  na  kiarusi.

Kinyang'anyiro  cha leo ni  baina ya kaimu rais, Rupiah  Banda na kiongozi wa chama  cha  upinzani Michael  Sata.

Watu  wanaendelea kupiga kura na habari zinasema  zoezi hilo linafanyika huku kukiwa na  mvutano.  Vituo kadhaa vilifunguliwa  kwa  kuchelewa mjini Lusaka.  Kiongozi  wa  upinzani  bwana Sata  amedai kuwapo  njama  baina  ya maafisa  wa  tume ya  uchaguzi  na polisi.   

Habari  zinasema   bwana Sata yupo sambamba na kaimu rais Banda katika kinyang'nyiro hicho. Bwana Sata amesema kuwa chama  kinachotawala hakiwezi  kushinda katika uchaguzi wa leo .Amedai kuwa tume  ya uchaguzi na polisi wanakula  njama  za kujaribu kuiba kura.

Rais wa muda bwana Rupiah Banda ameahidi  kuendelea na sera za hayati Mwanawasa aliekuwa maaruf miongoni mwa watu wake.

Bwana Banda mwenye umri wa  miaka 71  anakiongoza chama kinachotawala  -Movement  For Multi Party Democracy. 

Mshindani  wake, kiongozi wa chama cha upinzani- Patriotic Front  bwana Michael Sata  ameahidi kuleta mabadiliko makubwa  mnamo  muda wa siku 90 . Amesema ikiwa atashinda katika uchaguzi, baada ya  muda huo atayalazimisha makampuni ya nje kutoa asilimia  25 ya maslahi yao kwa kampuni za wanananchi wa  Zambia.

Licha ya kuwapo mvutano, watazamaji wa kimataifa kutoka Umoja wa Afrika wamesema uchaguzi  unaenda vizuri na kwamba hakuna dalili za   kuthibitisha wizi wa kura.


Hatahivyo kutokana na  kuhofia  kutokea fujo baada  ya kumalizika zoezi la kipiga kura leo jioni ,polisi na wanajeshi wamewekwa katika hali ya tahadhari.

Wagombea wengine katika  uchaguzi wa  leo ni   kiongozi wa chama cha UPND bwana  Hakainde Hichilema na aliekuwa makamu wa rais,  Godfrey Miyanda  wa chama cha Heritage. Matokeo ya kwanza yanatarajiwa kufahamika baadae leo.