1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Nicaragua-Daniel Ortega anarejea

P.Martin7 Novemba 2006

Uwezekano wa Daniel Ortega kushinda uchaguzi wa rais nchini Nicaragua,ni pigo jipya kwa Marekani inayoona ushawishi wake ukimungúnyika katika nchi za Amerika ya Kusini,kwa sababu ya ushindi wa vyama vya mrengo wa kushoto katika chaguzi za hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/CHLE

Baada ya kuhesabiwa asili mia 62 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa rais wa siku ya Jumapili nchini Nicaragua,matokeo ya mwanzo yanaonyesha kuwa Daniel Ortega amejinyakulia asili mia 38.6 ya kura hizo na anaongoza kwa takriban pointi nane kulinganishwa na mhasimu wake aliezuia nafasi ya pili.

Mgombea uchaguzi anahitaji kushinda asili mia 35 ya kura na aongoze kwa pointi tano kulinganishwa na mshindani mwenzake ili aweze kushinda moja kwa moja na hivyo kujiepusha na duru ya pili ya uchaguzi.

Wapinzani wake wa kihafidhina,Eduardo Montealegre na Jose Rizo wamepata asilimia 30.9 na 22.9. Serikali ya Marekani na hasa balozi wake mjini Managua,aliwahimiza wananchi wa Nicaragua waungane kumshinda Ortega.Kwani hata miaka 16 baada ya kumalizika vita kati ya serikali ya Sandinista iliyoungwa mkono wakati huo na Soviet Union ya zamani na waasi wa Contra waliopewa mafunzo na Marekani,bado Marekani humtazama Ortega kama ni mshirika hatari wa mrengo wa kushoto wa rais Hugo Chavez wa Venezuela.Hata kabla ya kufanywa uchaguzi wa siku ya Jumapili Marekani ilionya kuwa itafikiria upya uhusiano wa pande mbili kama Ortega atachaguliwa kuwa rais mpya.

Ortega wakati wa kampeni zake za uchaguzi, alijiepusha kumkosoa vikali rais Bush.Si hilo tu bali chama cha Sandinista pia kinaunga mkono mkataba wa biashara huru uliotiwa saini mapema mwaka huu kati ya nchi za Amerika ya Kati na Marekani.Ortega amesema anataka kuendeleza uhusiano uliopo kati ya nchi hiyo masikini na Marekani.

Wakati huo huo rais wa Venezuela Hugo Chavez anaejulikana kama mhasimu wa rais wa Marekani George W.Bush,amemuunga mkono Ortega na amejitolea kuiuzia Nicaragua mafuta kwa bei ya chini,ikiwa Ortega atashinda uchaguzi.