1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Marekani, Wa-Republican wahoi

Othman, Miraji21 Mei 2008

Urithi wa rais wa Marekani, Geoge Bush, usiopendwa na watu wengi, ni kama wingu lililoyagubika matarajio ya Chama cha Republican katika uchaguzi ujao wa mwezi Novemba.

https://p.dw.com/p/E3sV
Mtetezi wa Chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa Marekani.Picha: AP

Kuna hofu kwamba chama cha Democratic kitajizolea ushindi mkubwa katika uchaguzi huo.

Matatizo ya uchumi, vita vya Iraq visivopendwa na watu na ambavyo vimesimamiwa vibaya na wingi mkubwa wa watu waliojichomoza kupiga kura katika chaguzi za mchujo za Chama cha Democratic, mambo yote hayo yanawafanya watetezi wa Chama cha Republican kutafuta mkakati mpya ambao wanatarajia, angalau, utazuwia kile kinachoonekana kuwa utakuwa ushindi mkubwa wa Chama cha Democratic katika mabaraza yote mawili ya Bunge, yaani Baraza la Wawakilishi na lile la Senate.


Majabali ya mwanzo yalianza kuanguka pale Chama cha Democratic kilipovinyakua viti vitatu vya Baraza la wawakilishi kwenye uchaguzi maalum mnamo miezi mitatu iliopita; viti hivyo vyote vitatu vilikuwa katika maeneo yalio na ushabiki mkubwa wa Chama cha Republican.


Watu wanasema kwamba ikiwa Chama cha Republican kimeweza kushindwa katika wilaya hizo, basi kinaweza kushinda kokote kwengine. Hivyo, Wa-Republican wanahitaji kuzichunguza nyoyo zao na kutafakari juu ya nini kilichokwenda kombo ndani ya chama chao.


Miaka minanne tu iliopita, pale George Bush alipochaguliwa tena, na Chama cha Republican kikawa na wingi wa viti katika mabaraza yote mawili ya Bunge, chama hicho kilitamba. Lakini watu walianza kuvunjwa moyo pale Rais Bush aliposhikilia kwamba atain'gan'gania siasa yake kuhusu vita vya Iraq na pia kuhusu kashfa kadhaa zilizoharibu majina ya vigogo wa Chama cha Republican. Chama cha Democratic miaka miwili baadae kiliweza kupata wingi, japokuwa wa chupu chupu, katika mabaraza hayo ya Bunge, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 994.


Na licha ya kwamba Chama cha Democratic tangu wakati huo hakijaweza kuutumia wingi wao bungeni kuanza kuyaondoa majeshi ya Kimarekani kutoka Iraq, au kupeleka mbele yale mambo wanayoyaona kwao kuwa ni muhimu, hata hivyo, chama cha Republican nacho hakichasonga mbele katika kuisafisha sura yake iliochafuka.


Chama cha Republican kinafikiri kwamba kinaweza kunusuru kile kinachoweza kunusurika katika uchaguzi wa Novemba, hasa kikiwa na mtetezi wa urais John McCain, ambaye ukakamavu wake unaweza kuzivutia kura za wale watu wanaojiita kuwa ni wenye kujitegemea. Hicho kitakuwa kibarua kikubwa, kila mmoja anakiri. Rais, ambaye ni alama ya kuwa mkuu wa chama, hakubaliwi na watu wengi, hivyo anaweza kuwa mwiba wa mchongoma kwa watetezi wengi wa chama chake watakaowania ubunge katika uchaguzi ujao. Kura ya uchunguzi wa maoni iliofanywa baina ya Mei 8 na 12 ilisema ni asilimia 28 tu ya wananchi wanaomuunga mkono George Bush, huku asilimia 67 wakimpinga.


Lakini licha ya matatizo hayo yote ya Chama cha Republican, Seneta John McCaine wa chama hicho, bado anaweza kuchaguliwa kuwa rais.


Karibu thuluthi mbili ya Wa-Republican wanaojuwa nini kinafanyika ndani ya bunge, walipoulizwa, walisema wanaamini Chama cha Democratic huenda kikashinda kiti kimoja hadi 19 zaidi katika Baraza la wawakilishi lenye wajumbe 435. Ikiwa ni hivyo, basi Chama cha Republican kitabakia katika kiza, kama kilivokuwa katika miaka ya sitini na sabini. Katika baraza la Senate, Chama cha Democratic kinaweza kushinda hadi viti saba zaidi, hivyo kukaribia kuwa na viti 60 katika baraza hilo.


Pia inafikiriwa kwamba uhasama wa sasa baina ya watetezi wawili wa urais wa Chama cha Democratic, Barack Obama na Bibi Hilary Clinton hautadumu hadi hadi Novemba. Jambo jingine ni kwamba Chama cha Republican hakina fedha nyingi za kampeni ya uchaguzi kama kilivyo Chama cha Democratic, na Barack Obama, pindi atashinda kuteuliwa na chama hicho, basi atakuwa amekusanya fedha nyingi za kampeni, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa na mtu yeyote mwengine hapo kabla. Na kumbuka kwamba wafadhili hawataki kuchangia kwa ajili ya mtu wanayehisi atashindwa.