1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AfD washinda kwa kishindo

7 Machi 2016

Chama cha,AfD,kimejikingia si chini ya asili mia kumi katika chaguzi za mabaraza ya miji katika jimbo la Hessen. AfD kinatishia kugeuka nguvu ya 3 ya kisiasa,wiki moja kabla ya uchaguzi wa majimbo 3 ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1I8QV
Matokeo ya uchaguzi wa mabaraza ya miji HessenPicha: picture-alliance/dpa/A. Arnold

Kwa mujibu wa matokeo ya awali,chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia,kimegeuka nguvu ya tatu muhimu ya kisiasa kufuatia uchaguzi huo wa mabaraza ya miji katika jimbo la Hessen. Kwa mujibu wa idara ya takwimu ya jimbo la Hessen,AfD kimejikingia jumla ya asili mia 13.2,kikipitwa kidogo tu na chama cha Christian Democratic Union kilichojipatia asili mia 28,nukta mbili,kura ambazo takriban ni sawa na zile za chama cha SPD kilichojipatia asili mia 28 .

Vyama hivyo viwili vikuu vimelishwa hasara ikilinganishwa na matokeo ya uchaguzi kama huo miaka mitano iliyopita. Wakati ule,CDU walijikingia asili mia 33.7 na SPD asili mia 31.5. Pigo kubwa zaidi wamepata walinzi wa mazingira;wamepoteza asili mia 6.7 na kuondoka na asili mia 11.6 tu,ikilinganishwa na matokeo ya uchaguzi kama huo mwaka 2011.

FDP wamefanikiwa kujipatia asili mia 6.3,ikilinganishwa na asili mia 3.9 mwaka 2011

Katika jiji la Frankfurt,chama cha "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani"-AfD kimejipatia asili mia 10.3. Katika mji huo mkubwa kabisa wa jimbo la Hessen,mji mkuu wa kiuchumi wa Ujerumani yadhihirika kana kwamba serikali ya muunganao ya chama cha Christian Democratic Union na walinzi wa mazingira die Grüne inakaribia mwisho wake baada ya miaka kumi ya uongozi katika baraza la mji.

Deutschland Mitglied der Partei AfD in Mainz
Wanachama wa AfD katika mkutano wao mjini MainzPicha: picture-alliance/dpa/F. von Erichsen

Katika mji wa Wiesbaden chama cha AfD kimejikingia asili mia 15.3 ya kura na kugeuka kuwa nguvu ya tatu katika baraza la mji baada ya SPD na CDU. Na katika mji wa Bad Karlshafen chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia kimejipatia asili mia 22.3 na kukipita chama cha Social Democratic-SPD kilichojipatia asili mia 22.1 na CDU kilichojikusanyia asili mia 17.2.

Katika mji wa Darmstad,walinzi wa mazingira ndio wanaoongoza kwa asili mia 31wakiwaapita CDU na SPD.AfD wamejikingia asili mia 12.2.

Matokeo ya Hessen yawatia hofu baadhi ya viongozi wa vyama vikuu

Ushindi wa kishindo wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD unawatia wasi wasi viongozi wa vyama vikuu,wiki moja kabla ya uchaguzi katika majimbo ya Baden-Württemberg ,Rheinland-Pfalz na Sachsen-Anhalt. Hata hivyo kuna wanaohisi matokeo ya uchaguzi katika daraja ya miji hayawezi kulinganishwa na daraja ya majimbo au shirikisho.

Deutschland Winfried
Waziri mkuu wa jimbo la kusini la Baden-Württemberg-Winfried KretschmannPicha: Getty Images/T. Lohnes

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa/

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman