Uchaguzi wa Ireland Kaskazini. | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Uchaguzi wa Ireland Kaskazini.

Hatua inayosubiriwa sasa ni kugawana madaraka Wakatoliki na Waprotestanti.

Chama cha wahafidhina cha Waprotestanti Democratic Unionist na chama kikuu cha jamii ya Wakatoliki, Sinn Fein, vimetokeza kuwa washindi wakubwa katika uchaguzi wa Ireland Kaskazini, huku matokeo yakikaribia kukamilika hii leo. Uchaguzi huo unatarajiwa kufungua njia ya kugawana madaraka kwa pande zinazowakilisha jamii hizo mbili.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali ni kwamba chama cha kihafidhina cha Democratic Unionist-DUP kinachoongozwa na Kasisi Ian Paisley, kimenyakua 30.1 asili mia ya kura, wakati Sinn Fein kimepata 26.1 asili mia. Paislaey na kiongozi wa Sinn Fein Gerry Adams wameshinda kirahisi viti vyao. Wakati matokeo ya viti 72 kati ya 108 vikiwa yameshajulikana, DUP kina viti 25 kijiongeza viti 2 na Sin Fein viti 24 nyongeza ya viti wili pia. Matokeo kamili yanatarajiwa baadae leo.

Bunge la awali lilisimamishwa kwa zaidi ya miaka 4 baada ya kuzuka hali ya kutoaminiana , kati ya vyama vinavyowakilisha jamii mbili za wakatoliki na waprotestanti, baada ya kupatikana mkataba wa amani wa kihistoria 1998, ambao kwa sehemu kubwa umemaliza umwagaji damu uliodumu miaka 30 katika jimbo hilo la Uingereza.

Waziri mkuu wa Uingereaza Tony Blair na mwenzake wa Jamhuri ya Ireland Bertie Ahern, ambao ndiyo waandalizi wa mpango wa kugawana madaraka baina ya wakatoliki na Waprotestanti katika Jimbo la Ireland ya kaskazini, wanatazamiwa kukutana baadae leo jinni Brussels kuzungumzia matokeo ya uchaguzi huo. Katika uchaguzi huo kwa mara ya kwanza Anna Lo mwenye umri wa miaka 56 na mwanamke mwenye asili ya Hong Kong, amekua mtu wa kwanza kutoka jamii ya wachache kuchaguliwa mbunge. Bibi Loo mwenye uraia wa Uingereza ameishi Belfast kwa miaka 32 .

Hivi sasa pande hizo mbili za Waprotestanti na Wakatoliki zimepewa muda hadi tarehe 26 ya mwezi huu wa Machi, kuunda baraza la utawala, ikiwa ni serikali ya mseto itakayoliongoza jimbo hilo, la si hivyo Ireland ya kaskazini itatawaliwa moja kwa moja kutoka serikali kuu ya Uingereza mjini London ikishiriki pia Jamhuri ya Ireland na bunge la Ireland kaskazini kuvunjwa kabisa.

Sinn Fein ya wakatoliki imekua ikipigania jimbo hilo lijiunge na Jamhuri ya Ireland na DUP ya waprotestanti inataka libakie kuwa sehemu ya Uingereza.

Bado haijafahamika iwapo pande hizo zitafikia makubaliano ya kuunda utawala wa pamoja, ambapo kama makubaliano yatapatikana, basi kiongozi wa DUP Paisley mwenye umri wa miaka 80 anatarajiwa kuwa Waziri Kiongozi wakati Sinn Fein itashika wadhifa wa Naibu waziri Kiongozi akitarajiwa kuwa ni Martin McGuiness. Hata hivyo Kasisi Paisley ameonyesha shaka shaka juu ya kufanya kazi pamoja na mpinzani wake, kwa kutamka,“Siyo kwa wakati huu kwa sababu Bw Mc Guiness hawezi kuunga mkono hatua anazopaswa kuziunga mkono na kuwa mdemokrasi. Anapaswa kugeuzwa kuwa mdemokrasi.”

Lakini wakati Paisley ana onyesha shaka shaka juu ya kuundwa utawala wa pamoja , Bw McGuiness ana matumaini akisema, “Nafikiri sote, mimi na yeye tutaelewa umuhimu wa uchaguzi huu na zaidi kutambua mahitaji ya waliotuchagaua.”

Wadadisi wanaashiria kwamba licha ya matamshi yanayopingana pande hizo mbili kuu za jamii ya Ireland kaskazini hatimae zitaunda utawala wa pamoja ifikapo tarehe 26 Machi , muda uliowekwa kufikia hatua hiyo.

 • Tarehe 09.03.2007
 • Mwandishi Moahammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHIa
 • Tarehe 09.03.2007
 • Mwandishi Moahammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHIa

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com