1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa bunge wakamilika nchini Pakistan

18 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D9KE

Uchaguzi wa bunge nchini Pakistan uliofanyika leo umekamilika.

Vituo vya kupigia kura vimefungwa huku kukiripotiwa idadi ndogo ya wapigaji kura waliojitokeza kuwachagua viongozi watakaowawakilisha bungeni.

Wapakistan wamepiga kura kulichagua bunge jipya katika hatua muhimu kuelekea demokrasia baada ya miaka minane ya utawala wa kijeshi ulioongozwa na rais Pervez Musharraf.

Licha ya usalama kuimarishwa kote nchini watu tisa wameuwawa kwa kupigwa risasi sita katika jimbo la Punjab na wengine wawili katika jimbo la kusini la Sindh na mmoja jimboni Karak kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Maafisa wa usalama wa Pakistan wamesema watu wengine wasiopungua 100 wamejeruhiwa kwenye machafuko yaliyotokea leo katika maeneo mbalimbali ya Pakistan.

Lakini afisa wa wizara ya mambo ya ndani ya Pakistan amesema licha ya machafuko ya hapa na pale uchaguzi wa leo umefanyika kwa amani na utulivu.