1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa bunge waingia duru ya mwisho Ufaransa

18 Juni 2017

Wapiga kura wa Ufaransa Jumapili (18.06.2017) wameingia duru ya pili na ya mwisho ya uchaguzi wa bunge unaotazamiwa kutowa ushindi mkubwa kwa chama cha Rais Emmanuel Macron.

https://p.dw.com/p/2etKk
Frankreich Wahlen Stimmabgabe Macron
Picha: Reuters/C.Archambault

Wapiga kura wa Ufaransa Jumapili (18.06.2017) wameingia duru ya pili na ya mwisho ya uchaguzi wa bunge unaotazamiwa kutowa ushindi mkubwa kwa chama cha Rais Emmanuel Macron ambao utakamilisha ushindi wake wa mageuzi ya siasa za kitaifa nchini humo.

Uchunguzi wa maoni umetabiri chama cha sera za wastani cha Macron cha Le Republique en Marche (The Republique on the Move ,LREM) kinapaswa kunyakuwa sio chini ya viti 400 katika bunge la taifa lenye viti 577 kwa kuzingatia uchaguzi wa bunge wa duru ya kwanza Jumapili iliopita.

Lakini idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura kufikia mchana iliotolewa na wizara ya mambo ya ndani imedokeza kwamba uchaguzi huu wa marudio yumkini pia ukawa na wapiga kura wachache zaidi kuliko hata duru ya kwanza ambapo uliweka rekodi ndogo ya wapiga kura.

Ni asilimia 17.8 tu ya waliojiandikisha kupiga kura walikuwa wamepiga kura zao kufikia mchana hiyo ikiwa ni chini kwa asilimia 19.2 ikilinganishwa na duru ya kwanza wakati kama huo ambapo idadi ya waliojitokeza ilikuwa asilimia 48.7 baada ya vituo kufungwa.

Macron anahitaji kuwa na wingi wa viti katika bunge la taifa ili serikali yake iweze kuidhinishwa inayoongozwa na Waziri Mkuu Edouard Philippe na kupitisha mageuzi ya kiliberali ambayo tayari yanapingwa vikali na chama cha sera za mrengo wa kushoto na kile cha sera kali za mrengo wa kulia cha National Front.

Ushindi kuimarisha mamlaka ya mageuzi

Frankreich  Wahlen Macron
Rais Emmanuel Macron akiondoka nyumbani kwake kwenda kupiga kura yake.Picha: picture alliance/AP Photo/T.Camus

Ushindi wa wazi pia utaimarisha madai ya rais ya kuwa na mamlaka kwa mpango wake wa mageuzi.Amekiri kwamba wengi wa wapiga kura asilimia 64 waliomchaguwa katika duru ya pili ya uchaguzi hapo mwezi wa Mei walifanya hivyo kumzuwiya mpinzani wake kiongozi wa chama cha National Front Marine Le Pen kuingia madarakani.

Lakini anataraji kujitokeza kwa idadi ndogo ya wapiga kura kutapunguza taathira ya hata matokeo ya ushindi wa kishindo.

Macron yeye mwenyewe amepiga kura yake katika mji wa kitalii wa Touquet ambako ana nyumba yake binafsi. Tofauti na ilivyokuwa katika duru ya kwanza safari hii hakuandamana na mke wake Brigitte.

Baada ya kupiga kura alielekea katika ngome ya Mont-Valerein magharibi ya Paris ambapo ameshiriki katika maadhimisho ya kila mwaka ya wito wa Generali Charles de Gaulle wa kuwepo upinzani dhidi ya Ujerumani kuikalia Ufaransa wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Vikosi vya Ujerumani viliitumia ngome hiyo kama sehemu ya kuwanyongea zaidi ya wapiganaji 1,000 wa Ufaransa waliokuwa wakipinga kukaliwa na Ujerumani na mateka wakati wa vita.

Le Pen amepiga kura yake katika mji unaoongozwa na chama cha National Front wa kaskazini wa Henin-Beaumont ambao anajaribu kwa mara ya tatu kushinda kiti katika bunge la taifa.

Chama cha Macron na washirika wake wanajiandaa kunyakuwa wingi wa viti bungeni kwa kujizolea viti 449 kati ya 573 vinavyogombaniwa katika marudio haya ya uchaguzi wa bunge.

Upigaji kura utaendelea hadi saa kumi na mbili jioni nchini kote Ufaransa na hadi saa mbili usiku katika miji mikubwa ya Ufaransa ambapo vituo vya kupigia kura vikitarajiwa kutowa makadirio yao muda mfupi baada ya kufungwa kwa upigaji kura.

Matokeo rasmi yatakuwa yanatolewa hatua kwa hatua wakati mahesabu yakiendelea kushughulikiwa usiku kucha.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/AFP

Mhariri : John Juma