1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Senegal waelekea duru ya pili

Admin.WagnerD28 Februari 2012

Zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa Jumapili nchini Senegal linaendelea. Takribani nusu ya kura zote zilizopigwa imekwishahesabiwa, na kuna kila dalili kuwa hakuna mshindi wa dhahiri kuepusha duru ya pili.

https://p.dw.com/p/14BCu
Zoezi la kuhesabu kura laendelea Senegal
Zoezi la kuhesabu kura laendelea SenegalPicha: Reuters

Baada ya siku nyingi za kujigamba kwamba atapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi huu, Rais mkongwe wa Senegal Abdoulaye Wade hatimaye amekiri kuwa mwendo si mtelemko kama alivyofikiria. Wade ambaye uamuzi wake kusimama tena kama mgombea umesababisha mzozo wa kisiasa, amesema kuwa baada ya nusu ya kura zote kuhesabiwa anaongoza kwa kuwa na asilimia 32.17, huku mpinzani wake wa karibu Macky Sall akimpumlia kisogoni na asilimia 25.24.

Akizungumza katika mkutano wa kwanza na waandishi wa habari tangu zoezi la uchaguzi kuanza, Rais Wade alionekana kukosa msisimko wake wa kawaida. Hata hivyo aliwaambia wafuasi wake kwamba huu sio wakati wa kukataa tamaa, kwani bado yote yanawezekana; kushinda moja kwa moja, au kushinda kupitia duru ya pili ya kura. Ili kuepusha duru hiyo ya pili inambidi kupata asilimia 50 ya kura zote.

Rais Abdoulaye Wade amekiri uwezekano wa kushinda moja kwa moja ni mfinyu
Rais Abdoulaye Wade amekiri uwezekano wa kushinda moja kwa moja ni mfinyuPicha: picture alliance / dpa

Baadhi ya wapiga kura wanamlaumu Abdoulaye Wade kwa hali ngumu ya maisha katika kipindi cha miaka 12 ya uongozi wake, na wangependa kuona mabadiliko.

''Ni matumaini yangu kuwa Abdoulaye Wade atashindwa. Mimi sikumpigia kura yeye. Amezeeka sana na tumemchoka, wakati wa utawala wake bei ya chakula imepanda na kuwa mara tatu ya alivyoikuta. Hili ni jambo baya sana.'' Alisema mpiga kura mmoja.

Uchaguzi huu unawashirikisha wagombea 14
Uchaguzi huu unawashirikisha wagombea 14Picha: Reuters

Zaidi ya nusu ya kura zimehesabiwa

Matokeo kutoka wilaya 282 kati ya 551 za Senegal yamekwishahesabiwa. Wachambuzi wanasema nafasi pekee ya Abdoulaye Wade kushinda uchaguzi huu ni iwapo atapita moja kwa moja bila kulazimika kuingia duru nyingine, ambapo upinzani uliogawanyika sasa utakuwa umeungana nyuma ya mgombea mmoja.

Senegal yenye wakazi milioni 12, imekuwa ikichukuliwa kama nuru ya demokrasia barani Afrika, lakini hadhi hiyo ilichafuliwa na hatua ya Rais Abdoulaye Wade kukataa kuondoka baada ya mihula miwili ya uongozi kama inavyoeleza katiba ya nchi hiyo. Wachambuzi wanasema ghasia zilizojitokeza wakati wa maandamano ya kupinga hatua hiyo ya Rais Wade, zinaweza kuongezeka iwapo atatangazwa mshindi katika uchaguzi huu.

Kipindi cha kampeni ya uchaguzi kiligubikwa na ghasia
Kipindi cha kampeni ya uchaguzi kiligubikwa na ghasiaPicha: Reuters

Hatua nyuma kwa Wade?

Alipomaliza kupiga kura yake Jumapili, Wade aliwakasirisha watu alipojitapa atapata ushindi bila kulazimika kuingia mzunguko wa pili wa kura, na alizomewa na watu waliokuwepo.

Mwenendo wa Wade unachukuliwa na wengi kama hatua nyuma, ikizingatiwa namna alivyoingia madarakani kwa kushangiliwa. Ushindi wake mwaka 2000 dhidi ya rais aliyekuwepo wakati huo, Abdou Diouf, ambaye kwa uungwana mkubwa alimpigia simu Wade akimpongeza na kukubali kushindwa, ulionyesha kukomaa kisiasa na kidemokrasia kwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Wade anasisitiza kuwa hakukiuka katiba wakati alipogombea mhula wa tatu, na amesema nchi yake bado haijaacha njia ya demokrasia. Pia amewaomba wananchi kubakia watulivu wakati wakisubiri matokeo rasmi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu