Uchaguzi mpya Uturuki na kikao cha waislamu Ujerumani | Magazetini | DW | 03.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Uchaguzi mpya Uturuki na kikao cha waislamu Ujerumani

Uchaguzi mpya wa Bunge umeitishwa Uturuki kuikomboa kutoka mvutano wa hivi sasa wa kuamua nani angestahiki kugombea wadhifa wa urais.Huko Berlin waislamu walikutana kuanza utaratibu wa kupata msemaji wao na serikali.

Mada 2 zimechambuliwa kwa mapana na marefu na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo:Moja ni mkutano wapili kati ya Ujerumani na jumuiya za waislamu humu nchini na pili, hali nchini Uturuki baada ya Mahkama Kuu kubatilisha uchaguzi wa rais .

LEIPZIGER VOLKSZEITUNG juu ya mkutano wa jana huko Berlin na waislamu laandika:

“Waziri wa ndani wa Ujerumani Bw.Schäuble amefaulu kuwakusanya mbele ya meza moja wakakamavu,wepesi,watetezi wa haki za wanawake,watetezi wa mfumo wa kutenganisha dini na serikali,waumini wa madhehebu ya Alawit,wale wa kishia na wa madhehebu ya sunni.

Huo ni mchanganyiko wa nadharia tofauti,lakini hakukua na njia nyengine kufuata katika utaratibu huu mgumu .Walioshiriki wanapaswa kukiangalia kikao hicho kama fursa ya kuupa uislamu humu nchini sura ya kimambo-leo…..

Ama gazeti la TAGESSPIEGEL linlotokla Berlin linaona:

“Ni kweli alichosema waziri wa ndani Bw.Schäuble:Uislamu hauwezi tena kupanguswa usiwepo nchini Ujerumani.Na hivyo amesukuma usoni zaidi mazungumzo kati ya serikali na wajumbe wa kiislamu wa madhehebu mbali mbali-mbali zaidi kuliko hatua zote zilizochukuliwa hivi sasa chini ya jukwaa la kuleta pamoja mila na tamaduni mbali mbali lililopaliliwa na chama cha KIJANI cha walinzi wa mazingira….

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linazungumzia dai la Baraza kuu la waislamu kuwa msemaji wa waislamu humu nchini:

“jumuiya zilizojikusanya pamoja chini ya paa za Baraza hilo la waislamu linataka kujumuishwa katika kundi la jumuiya zinazosikizwa maoni yao katika kutunga sheria,kuwa na muwakilishi wao katika halmashauri zinazosimamia idhaa mbali mbali na kuwa na sauti hadharani kama kanisa na vyama vya wafanyikazi.Dai lao hilo limepata nguvu kwa hamu ya serikali ya kuwa na muakilishi anaewasemea waislamu humu nchini…”

Gazeti la LANDSHUTER ZEITUNG linakumbusha hali ya mambo ilivyo hata baada ya kikao cha jana huko Berlin.Laandika:

“Uhusiano kati ya wengi nchini upande mmoja na waislamu wachache upande wa pil, unabakia kuwa mgumu…na mkutano wa jana wa Berlin umethibitisha hayo.

Waziri wa ndani Bw.Schäuble alijaribu kueneza matumaini mema.Kuwa mazungumzo yanasonga mbele.Lakini kama hapo kabla kuna tofauti za kimsingi.Kwahivyo mambo hayatasonga mbele amedai mwenyekiti wa Baraza Kuu la waislamu nchini Ujerumani Ayuyub Köhler.

Wakati anapendekeza kufanywa jaribio jengine la kukutana,hakujibu swali la kimsingi kabisa na muhimu kuliko yote:Je, waislamu humu nchini wako tayari kuweka nyuma Qoran na kuitanguliza mbele katiba ya Ujerumani ?

Likitugeuzia mada, gazeti la kibiashara HANDELSBLATT linalotoka Düsseldorf linauchambua uamuzi wa waziri mkuu wa Uturuki Erdogan kuitisha uchaguzi mkuu mpya baada ya mahkama kubatilisha uchaguzi wa rais kwa jinsi ulivyokwenda bungeni.

Gazeti laandika:

”Ingawa kinyan’ganyiro cha madaraka kiliendeshwa katika hali ya kutatanisha siku chache zilizopita,matokeo yake ni ya busara.Uturuki sasa inakabiliwa na uchaguzi mpya wa Bunge.Uchaguzi huo utafafanua nguvu za madaraka ya kila upande.Kwani hata baada ya kupita miaka 85 tangu kuasisiwa Jamhuri hii ya uturuki,bado inasaka utambulisho wake kati ya mila na desturi za kiislamu na mfumo unaotenganisha dola na dini.”