1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi katika jimbo la Hesse

A Mtullya28 Januari 2008

Chama cha CDU chapata pigo wakati chama cha mlengo wa shoto "Die Linke" kimeingia bungeni kwa mara ya kwanza.

https://p.dw.com/p/CyjW
Waziri Mkuu wa Hessen Roland Koch na mgombea wa chama cha SPD Andrea YpsilantiPicha: picture-alliance/ dpa


Chama cha CDU cha Kansela Angela Merkel kimepata pigo la uso katika uchaguzi muhimu uliofanyika kwenye majimbo mawili ya Ujerumani mwishoni mwa wiki iliyopita.

Uchaguzi huo unaotathmiwa a kama kipimo cha hali ya kisiasa nchini Ujerumani kote, ulifanyika katika majimbo ya Hesse na Lower Saxony.

Katika jimbo la Hesse lícha ya kushinda, chama cha CDU kikiongozwa na waziri mkuu Roland Koch,kilipata asilimia 36.nukta 8. Kiwango hicho kinawakilisha anguko kutoka asilimia 49 ya kura kilichopata katika uchaguzi wa mwaka wa 2003.

Katika kampeni yake waziri mkuu Koch aliweka mkazo juu ya suala la uhalifu wa vijana wahamiaji na hivyo kuwagawanya wapiga kura . Lakini pia alijaribu kusisitiza suala la utengemavu wa kiuchumi katika kampeni hiyo.

Mshindani wake mkuu katika uchaguzi huo bibi Andrea Ypsilanti wa chama cha Social Demokratik alipata asilimia 36 nukta 7. Kampeni yake ilikuwa juu ya kuleta elimu bora,kuwajumuisha wahamiaji katika jamii na pia alitetea pendekezo la utaratibu wa mshahara wa kima chini.

Baada ya matokea ya uchaguzi kutangazwa bibi Ypsilanti alisema kuwa chama cha SPD sasa kimerudi tena.

Kutokana na tofauti finyu katika matokeo hayo hakuna chama kinachoweza kuunda serikali peke yake katika bunge lenye viti 110.

Akitangaza matokeo yauchaguzi huo, afisa wa uchaguzi aliwaambia waandishi habari .

Katika uchaguzi wa jimbo hilo la Hesse,chama cha waliberali FDP kilipata asilimia 9 nukta 4 na chama cha kijani asilimia 7 nukta 5.

Lakini kwa mara ya kwanza chama cha mlengo wa kushoto kimefanikiwa kuingia katika bunge la jimbo hilo tokea nchi mbili za Ujerumani ziungane tena.

Chama hicho ni mchanganyiko wa warithi wa wakomunisti wa Ujerumani Mashariki na watu waliojitoa kwenye chama cha SPD.

Katika uchaguzi wa jimbo jingine ,Lower Saxony waziri mkuu Christian Wullf wa chama cha CDU amefanikiwa kutetea kiti chake kwa kupata asilimia 43 ya kura.

Lakini kiwanggo hicho ni pungufu ya kura ambazo chama hicho kilipata katika uchaguzi wa mwaka 2003 ambapo kilifikia asilimia 48. Hatahivyo kiwango hicho kinamwezesha waziri mkuu Wullf kuunda serikali ya mseto na chama cha waliberali-FDP.

Katika jimbo hilo pia chama cha mlengo wa kushoto pia kilifanikiwa kuingia bungeni.

Wadadisi wamesema matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Hesse yanaashiria pigo kwa chama cha CDU nchini kote.

Watu wapatao milioni 10 na laki tano wanastahiki kupiga kura katika majimbo hayo mawili.

Asilimia 64 walijitokeza katika jimbo la Hesse na asilimia 57 katika jimbo la Lower Saxony.

Uchaguzi mkuu ujao nchini Ujerumani unatarajiwa kufanyika mwezi septemba mwaka ujao.