1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Indonesia

Halima Nyanza9 Julai 2009

matokeo ya awali ya Uchaguzi wa Rais nchini Indonesia, yanaonesha kuwa Rais anayetetea nafasi yake Susilo Bambang Yudhoyono ameshinda uchaguzi huo. Lakini hata hivyo upinzani unayapinga matokeo hayo.

https://p.dw.com/p/Ik9U
Rais anayetetea nafasi yake wa Indonesia Susilo Bambang Yudhoyono, akionesha kura yake, akiwa pamoja na mkewe kabla ya kupiga kura, nje ya mji wa Jakarta.Picha: AP

Upinzani nchini humo wamekataa kupokea taarifa za kushindwa katika uchaguzi huo wa Rais, na kusema kuwa uchaguzi huo, haukuwa wa kidemokrasia.

Rais wa zamani wa nchi hiyo, ambaye pia alishiriki katika kinyang'nyiro hicho ambapo matokeo ya awali yanaonesha kuwa ameshika nafasi ya pili kwa kupata asilimia kupata asilimia 28.6 ya kura zote zilizopigwa, Megawati Sukarnoputri leo amesisitiza kuwa chama cha Demokrasia cha kinachoongozwa na Rais Yudhoyono kilifanya udanganyifu wakati wa uchaguzi.


Kwa upande wake mgombea mwingine katika uchaguzi huo, Makamu wa Rais Yusuf Kalla, ambaye ameshika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 9.8 ya kura zote zilizopigwa, amekubali kushindwa.

Matokeo yasiyo rasmi yaliyotolewa kwa haraka na Taasisi tatu kuhusu uchaguzi huo wa Rais uliofanyika jana, Jumatano yanaonesha kwamba Rais Susilo Bambang Yudhoyono anaongoza kwa asilimia 60 ya kura zilizopigwa.


Aidha matokeo ya awali yaliyotolewa leo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo yanaonesha kwamba Rais Yudhoyono anaongoza kwa asilimia 61.7 kutoka katika kura milioni 19, zilizohesabiwa hadi leo asubuhi.


Matokeo hayo ya awali, yanampa nafasi nzuri Rais huyo, kupata zaidi ya asilimia 50, itakayomwezesha kukwepa kufanyika tena kwa duru ya pili ya uchaguzi mwezi Septemba.


Awali akizungumza baada ya kupiga kura, jana huku akiwa na matumaini ya kushinda tena Rais Yudhoyono aliwashukuru wote waliofanikisha uchaguzi huo.


Lakini hata hivyo mpinzani wa Rais huyo, bila ya kuonesha vithibitisho, amekilaumu chama chake cha Demokrasia kwa udanganyifu wakati wa uchaguzi, kwa kuhoji uhalali wa kuhesabiwa kura kwa haraka na kutishia kupinga matokeo ya mwisho, hali ambayo inaongeza wasiwasi wa kutokea kwa mvutano wa kisiasa.


Hata hivyo Waangalizi wa Uchaguzi nchini Indonesia wanasema kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki, wakati matokeo hayo ya awali yakimuonesha Rais Yudhiyono kuwa mshindi.


Matokeo Rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo tarehe 25 ya mwezi huu wa Julai.


Licha ya kukosolewa mara kwa mara kwamba ni mtu asiyekuwa na maamuzi, Rais Yudhoyono amekuwa akiheshimiwa kwa baadhi ya mafanikio yaliyopatikana wakati wa awamu yake ya kwanza ya uongozi madarakani, ikiwemo kuimarisha uchumi na kuleta amani.


Alishinda uchaguzi wa kipindi chake cha awamu ya kwanza madarakani mwaka 2004 ambapo aliahidi kupambana na rushwa, umasikini na kuinua uchumi wa nchi hiyo.


Waangalizi wa Uchaguzi wanasema kuwa zaidi ya watu milioni 176 kati ya Waindonesia milioni 230 wenye uwezo wa kupiga kura walipiga kura zao katika vituo laki nne na 50, katika zoezi hilo lililofanyika kwa amani katika taifa hilo lenye visiwa vipatavyo elfu 17.


Mwandishi: Halima Nyanza(AP)

Mhariri Mohamed Abdul-Rahman