1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania unasaidia watoto yatima

Balozi Wolfgang Ringe aahidi ubalozi utaangalia namna ya kutatua tatizo la maji

Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania hivi majuzi ulitembelea vituo vya kulelea watoto yatima jijini Dar es salaam, ili kuangalia namna ya kuvisaidia na kuboresha maisha ya watoto hao.

Katika ziara hiyo Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Bwana Wolfgang Ringe alitoa ahadi kuwa nchi yake itasaidia kutatua tatizo kubwa linalokikabili kituo hicho la ukosefu wa maji.

Ahadi hii hasa inakihusu kijiji cha SOS ambacho ni kituo kikubwa kabisa cha kulelea watoto yatima kilichojengwa jijini Dar es salaam chenye uwezo wa kulea watoto takliban 130 kwa wakati mmoja.

Balozi Ringe alitoa ahadi hii kutokana na ombi lililotolewa na mmoja wa wadhamini wa kituo hicho Bwana Hilary Biduga wakati akimkaribisha balozi. Katika risala yake Biduga alisema kuwa kijiji hicho kilikuwa kikikabiliwa na tatizo la mfumo wa maji, na eneo la watoto kuchezea.

Mwakilishi huyo wa Ujerumani nchini Tanzania alisema kuwa ijapokuwa tatizo la eneo la watoto kuchezea halipaswi kupuuzwa lakini tatizo la maji lazima lipewe kipaumbele.

Kwa hiyo akawaahidi wadhamini na wafanyakazi wa kituo hicho kuwa maadhali ubalozi wake una uwezo wa kutoa msaada wa hadi Euro elfu nane ambazo ni sawa na wastani wa shilingi milioni 12 pesa za kitanzania, basi kituo hicho kilete maombi rasmi kwenye ubalozi.

“Tutaangalia mazingira hapo. Na ninaweza kukuahidini kwamba tutaangalia ikiwa ninaweza kusema hivyo, maombi mliyonayo na tayari nimewaambia katika ubalozi, tanasubiri maombi yenu ya awali”, akasisitiza Balozi Ringe.

Hiki ni kituo cha kwanza kujengwa na Shirika hili la SOS nchini Tanzania. Cha kwanza kilijengwa visiwani Zanzibar mwaka 1991. Mwaka 2000 mwezi wa May shirika hilo likajenga kituo kingine mkoani Arusha.

Kituo hiki cha Dar es salaam kilichoanza kazi mwanzoni mwa mwaka huu tayari kimekusanya watoto yatima 28.

Akiulizwa na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho hapa Tanzania Bwana Nassor Hemed juu ya utaratibu unaotumika kuwapata watoto hawa alisema “ zaidi tunatumia habari tunazozipata kutoka viongozi wa serikali za mitaa na vitongoji lakini nasisi tunafanya upelelezi wetu”. Anasema na kuongeza kuwa inachukuliwa tahadhari kubwa wakati wa kuwachagua watoto hawa ili wasije kuletwa kituoni hapo watoto wasiokusudiwa mfano ambao wana wazazi lakini wakalazimika kuletwa kituoni hapo kutokana na ukali wa maisha.

Akizungumzia manufaa ambayo yamepatikana tangu kuanzisha kituo cha SOS visiwani Zanzibar, Bwana Nasor alisema watoto waliolelewa na kituo hicho sasa hivi ni watu wazima baadhi wameoa na wengine kuolewa ilhali wengi wakiendelea kimasomo katika ngazi mbalimbali.

“ wengine wame-advance academically, mmoja ameisha maliza marekani, kwa mambo ya mathematics mmoja yupo South Africa, kuna wengine hapa wapo hapa University of Dar es salaam, mwingine alimaliza business administration hapo, na kuna mwingine anachukua mambo ya computer, alimuradi mambo mbalimbali ya kuwafanya watoto wajitegemee”.

Kwa mujibu wa Bwana Biduga Shirika hili la SOS linatarajia kujenga vituo vingine viwili hapa Tanzania kataka kipindi cha miaka 4 kuanzia sasa.

Mojawapo ya vituo hivyo vipya na kinachotarajiwa kuanza hivi karibuni kinakusudiwa kujengwa mjini Bagamoyo umbali wa kilomita zipatazo 70 kutoka mjini Dar es salaam.

Mwisho.

 • Tarehe 24.04.2007
 • Mwandishi Christopher Buke
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHl8
 • Tarehe 24.04.2007
 • Mwandishi Christopher Buke
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHl8