Ubadilishanaji wafungwa Israel-Hamas waanza rasmi | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.10.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ubadilishanaji wafungwa Israel-Hamas waanza rasmi

Mapema leo (18.10.2011), kundi la Hamas limemuwachia huru mwanajeshi wa Israel, Gilad Shalit, huku Wapalestina 477 wakiwa njiani kuelekea nyumbani baada ya kuachiwa huru kutoka jela za Israel.

Gilad Shalit katika mahojiano ya kwanza na Nile TV ya Misri.

Gilad Shalit katika mahojiano ya kwanza na Nile TV ya Misri.

Kiasi ya saa 5.00 asubuhi kwa saa za Mashariki ya Kati, kituo cha televisheni cha Nile cha Misri kimemuonesha kijana wa miaka 25 sasa, mwembamba, mwenye rangi iliyopauka lakini mwenye afya, akifanya mahojiano yake ya kwanza. Alikuwa ni Gilad Shalit akiwa katika hatua ya kwanza ya uhuru wake baada ya miaka mitano mikononi mwa Hamas.

Chanzo kimoja cha habari kutoka jeshi la Israel, kimeliambia Shirika la Habari la AFP, kwamba Shalit alipelekwa Misri na Hamas wenyewe.

Taarifa hizi pia zimethibitishwa na kundi la Ezzedine al-Qassam lililo karibu na tawi la kijeshi la Hamas. Msemaji wa kundi hilo, amesema kuwa licha ya Shalit kukabidhiwa kwa mamlaka za Misri, "asingelipelekwa Israel mpaka wafungwa wote wa Kipalestina wawe huru".

Mama wa Kipalestina anayemsubiri kijana wake kutoka jela za Israel.

Mama wa Kipalestina anayemsubiri kijana wake kutoka jela za Israel.

Hadi wakati Shalit anafanya mahojiano na televisheni ya Nile, hakukuwa na kauli yoyote kutoka upande wa Israel, lakini tayari ilishafahamika kuwa wafungwa 477 wa Kipalestina walishaanza kusafirishwa kwenye mabasi kuelekea Misri.

Huko Gaza na Ukingo wa Magharibi, wafungwa hao walikuwa wanasubiriwa kupatiwa mapokezi ya kishujaa. Miongoni mwa waliokuwa wakisubiriwa kwa hamu ni Irena Sarahna, mwanamke wa Kipalestina mwenye asili ya Ukraine, ambaye kwa mwaka wa kumi amekuwa kwenye jela za Israel. Binti yake, Ghazaleh Sarahna, hajawahi kumuona mama yake.

"Nilikuwa na miezi minane tu mama yangu alipokamatwa. Simjui mama yangu. Sasa ni msichana mzima tayari ndiyo yeye anaachiwa huru. Kwa hakika nina furaha sana." Amesema Ghazaleh.

Ikiwa kila jambo litakwenda kama ilivyokubaliwa, Israel inatakiwa kuwaachia wafungwa 1,027 kwa kumpata Shalit mmoja. Hii itakuwa ni mara ya kwanza ndani ya miaka 26 iliyopita kwa mwanajeshi wa Israel kurudishwa kwao akiwa hai.

Mwanamke wa Kipalestina akipita mbele ya mchoro wa picha ya Gilad Shalit, Gaza

Mwanamke wa Kipalestina akipita mbele ya mchoro wa picha ya Gilad Shalit, Gaza

Kiasi ya saa 7.00 mchana kwa saa Mashariki ya Kati, wafungwa 297 wameingia Gaza, kupitia Kerem Shalom, kisha Misri kupitia mpaka wa Rafah, ambako baadaye wanapokewa na viongozi wa ngazi za juu wa Hamas, akiwamo Khaled Meshaal na Waziri Mkuu, Ismail Haniyeh.

Wafungwa wengine 40 wanasafirishwa kwenye nchi nyengine, zikiwemo Qatar, Uturuki na Syria. Hamas imesema itampa kila mfungwa anayerejea nyumbani, fedha na kazi ya kujikimu kimaisha.

Mpatanihsi mkuu wa ujumbe wa Palestina katika mazungumzo ya amani na Israel kutokea chama cha Fatah, Saeb Erakat, amesifu hatua hii ya mabadilishano ya wafungwa, lakini akasema kwamba haitoshi kuleta amani baina ya pande hizo mbili.

"Ukaliaji wa Israel kwenye ardhi ya Wapalestina lazima umalizike. Ni wakati wa kumaliza ukaliwaji huu, ni wakati wa amani. Kwa bahati mbaya sana, wakati Waziri Mkuu wa Israel anatangaza kuachiwa kwa wafungwa 1,000 wa Kipalestina katika mpango wa mabadilishano, anatangazapia ujenzi wa nyumba 3,000 katika Jerusalem ya Mashariki." Amesema Erakat.

Kukamatwa kwa Shalit akiwa na cheo cha ukoplo hapo mwaka 2006, kulizifanya pande zote husika kulipa gharama kubwa sana kwa minajili ya mtu mmoja tu.

Siku tatu baada ya kukamatwa kwake, Israel ilianzisha operesheni ya kijeshi ya miezi mitano kujaribu kumuokoa, bila ya mafanikio. Operesheni hiyo ilimalizika kwa vifo vya zaidi ya Wapalestina 400.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA
Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

 • Tarehe 18.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12uAb
 • Tarehe 18.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12uAb

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com