1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tymoshenko aanza mgomo wa kula

26 Novemba 2013

Kiongozi wa upinzani nchini Ukraine, Julia Tymoshenko leo ameanza mgomo wa kula chakula, akiwaunga mkono maelfu ya watu wanaopinga uamuzi wa serikali hiyo kuubatilisha mkataba baina ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1AOgg
Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine, Julia Tymoshenko
Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine, Julia TymoshenkoPicha: picture-alliance/dpa

Tymoshenko, kiongozi mwenza wa muungano uliofanya mapinduzi yaliyopewa jina la chungwa, mwaka 2004, unaounga mkono mataifa ya Magharibi, alitangaza kuanza mgomo huo katika barua yake aliyowaandikia wafuasi wapatao 20,000 jana Jumatatu (25.11.2013) wanaounga mkono mkataba wa ushirikiano kati ya Ukraine na Umoja wa Ulaya, ambao wanaandamana mjini Kiev kwa siku ya pili mfululizo.

Tymoshenko aliyekuwa waziri mkuu wa Ukraine, amesema ataendelea kugoma hadi hapo Rais Viktor Yanukovych atakaposaini mkataba huo kuhusu ushirikiano na biashara huru na Umoja wa Ulaya. Ameongeza kusema kuwa iwapo Yanukovych hatosaini mkataba huo tarehe 29 ya mwezi huu wa Novemba, atolewe katika uongozi wa Ukraine kwa njia ya amani na kikatiba, pamoja na wasaidizi wake wa kisiasa na wala rushwa.

Polisi wakipambana na waandamanaji mjini Kiev
Polisi wakipambana na waandamanaji mjini KievPicha: GENYA SAVILOV/AFP/Getty Images

Taifa hilo la watu milioni 45, linajikuta katika mzozo mpya wa kisiasa uliosababishwa na uamuzi wa ghafla wa serikali wa kuubatilisha mkataba wa kihistoria na Umoja wa Ulaya katika mkutano wake utakaofanyika Vilnius, mji mkuu wa Lithuania baadaye wiki hii. Uamuzi huo umepitishwa baada ya Yanukovych kufanya mazungumzo ya siri na Rais wa Urusi, Vladmir Putin mjini Moscow. Mazungumzo hayo yalikuwa yanasadikiwa kuelezea vikwazo vikali ambavyo Urusi ingeviweka dhidi ya Ukraine, iwapo ingeusaini mkataba huo na Umoja wa Ulaya.

Mkataba huo unaiweka wapi Ukraine?

Mkataba huo wa ushirikiano ungeiweka Ukraine katika nafasi nzuri ya kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya hapo baadaye na kuiondoa nchi hiyo kuwa mhimili wa kihistoria wa Urusi. Hata hivyo, Rais Putin anaiona Ukraine kama mwanachama muhimu mpinzani wa kiuchumi katika umoja unaojulikana kama Umoja wa Forodha wa nchi za Ulaya na Asia, ambao tayari unazijumuisha Kazakhstan na Belarus.

Jana jioni, Rais Yanukovych aliwataka wananchi wake kuwa watulivu na kuutetea uamuzi huo kwamba ulizingatia hatari za kiuchumi ambazo nchi hiyo ingezipata iwapo ingevuja uhusiano wake wa kibiashara na Urusi. Uamuzi huo umetolewa baada ya bunge kushindwa kwa mara nyingine kuupitisha muswada wa sheria utakaoruhusu kuachiwa huru kwa Tymoshenko, sharti kuu lililotolewa na Umoja wa Ulaya ili nchi hiyo iweze kusaini mkataba huo. Tymoshenko anatumikia kifungo cha miaka saba gerezani baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka.

Rais Viktor Yanukovych na Rais Vladmir Putin
Rais Viktor Yanukovych na Rais Vladmir PutinPicha: picture-alliance/dpa

Jana Jumatatu, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatanya zaidi ya waandamanaji 100,000 wanaoupinga uamuzi huo wa serikali waliokusanyika mjini Kiev. Umati huo wa watu unaelezwa kuwa mkubwa zaidi kutokea tangu mapinduzi ya chungwa na baadae Viktor Yushchenko kutoka muungano unaounga mkono mataifa ya Magharibi, kushinda katika uchaguzi wa urais mwaka 2007.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo,AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman