1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Twiga wako hatarini kutoweka barani Afrika

8 Desemba 2016

Idadi ya twiga imepungua kwa karibu asilimia 40 barani Afrika tangu miaka ya 1980 katika kile kinachoelezwa kama ''kutoweka kimya kimya'' kunakosababishwa na uwindaji haramu na kuongezeka kwa maeneo ya kufanyia kilimo.

https://p.dw.com/p/2Twa2
Niger Giraffen aus dem Kouré Giraffe Reserve
Picha: Getty Images/AFP/B. Hama

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Red List, shirika linalofanya utafiti kuhusu wanyama walio katika kitisho cha kuangamia.Twiga, mnyama mrefu zaidi duniani, yuko katika hatari.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Mazingira, IUCN, idadi ya wanyama hao duniani imepungua na kufikia karibu 98,000 kutoka idadi ya twiga kati ya 152,000 na 163,000 iliyokuwepo mwaka 1985.

Ripoti ya shirika hilo  inawaweka twiga katika hatari kubwa ya kutoweka kwa kuzingatia mienendo ya sasa ukilinganisha na ilivyokuwa awali. Kushuka kwa idadi ya twiga ambako hutokea sana katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara kunatokea kwa sehemu kubwa bila kutambuliwa.

Wakati watalii wanapenda kuwaona twiga katika maeneo ya hifadhi, katika vyombo vya habari na katika maeneo ya hifadhi, watu wa kawaida pamoja na wahifadhi hawafahamu kuwa wanyama hao wenye fahari wako katika kipindi cha hatari ya kuangamia kimya kimya anasema Julian Fennesy mtaalamu wa masuala yahusuyo twiga kutoka shirika la IUCN.

Fennesy anaongeza  kuwa ujangili, magonjwa pamoja na watu kuhamia katika maneo wanakoishi twiga hasa katika nchi za Afrika ya kati na Mashariki kuwa ni kati ya sababu ambazo zimechangia kupungua kwa idadi ya twiga.

Shughuli mbalimbali za kibinadamu zimechangia

Twiga wako katika hatari pia kutokana na kuongezeka kwa maeneo ya kuendeshea shughuli za kilimo ili kuweza kutosholeza mahitaji ya chakula kwa idadi ya watu ambayo inazidi kuongezeka, na pia kutokana na kuwauwa ili watu waweze kupata nyama, hii hutokea sana katika maeneo ambayo yana migogoro kama vile Sudan Kusini.

BdT Giraffen im Zoo
Twiga wakiwa katika moja ya maeneo ya hifadhiPicha: AP

Alex Motoko ni muelimishaji wa uhifadhi katika kituo cha twiga nchini Kenya anathibitisha kwa kusema ni kweli wanyama hao wako katika hatari kwa sababu ya kupotea kwa maeneo asili ya kuishi, watu wameanza kuendesha shughuli za kilimo katika maeneo hayo na katika mchakato huo twiga wameanza kufa kutokana na kupungua kwa chakula, na pia wakulima wamekuwa wakiwauwa pale wanapoingia katika mashamba yao.

Craig Hilton ni kiongozi wa shirika hilo, akiongeza na shirika la habari la Reuters amesema

"Watu wanapigania rasilimali chache zilizopo na wanyama wanakuwa katika hali mbaya zaidi hasa katika maeneo yenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe" na kutaja kuwa mabadiliko ya hali ya hewa pia  kuwa jambo jingine linalochangia.

Utafiti huo pia umebaini kuwa asilimia 11 ya aina nyingine ya ndege 700 ambao wamefanyiwa tathimini wako katika hatari ya kutoweka. Umoja wa mataifa unasema kuwa vitisho vinavyotokana na shughuli mbalimbali za binadamu kumesababisha kupotea kwa makaazi asili.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/Reuters/AP

Mhariri:Gakuba Daniel