1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Twiga hatarini kutoweka

Admin.WagnerD27 Februari 2015

Ni wanyama wachache sana wanaotambulishwa zaidi na bara la Afrika kama alivyo Twiga. Lakini sasa mnyama huyo anakabiliwa na kitisho cha kutoweka kutokana na imani kwamba uboho wake unatibu ukimwi.

https://p.dw.com/p/1Eioq
Serengeti Nationalpark in Tansania
Twiga wakiwa katika mbuga ya Seregeti.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Elshamy

Twiga ni mnyama maarufu katika ukanda wa Savannah kama walivyo Kangaruu kwa nchi ya Australia. Kwa urefu wa shingo yake wa hadi mita mbili Twiga ndiyo mnyama mrefu zaidi duniani na amekuwa akivinjari katika ukanda wa Savannah wa bara la Afrika tangu enzi. Nchini Tanzania Twiga ni mnyama wa taifa, lakini pamoja na hadhi yake hiyo, mnyama huyo anakabiliwa na kitisho kikubwa cha kutoweka.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, idadi ya Twiga imepungua kwa kiwango cha kustusha, anasema Marlies Gabriel, raia wa Namibia mwenye asili ya Ujerumani, ambaye pamoja na mume wake wanaendesha biashara ya nyumba ya wageni katika mbuga ya wanyama ya Arusha, na wanajishughulisha na utunzaji wa mazingira ya asili katika mkoa huo. Hadi miaka michache iliyopita, wanyama hao walikuwa wanakutikana kwa wingi katika maeneo yanayozunzunguka mlima Meru, lakini leo hii wageni katika mbuga hiyo wanapaswa kutafuta muda mrefu hadi kumuona Twiga.

Twiga wa Uganda katika bustani y awanyamapori nchini Ujerumani.
Twiga wa Uganda katika bustani y awanyamapori nchini Ujerumani.Picha: Tierpark Berlin

Sababu kuu ni ujangili

Sababu za kupungua kwa wanyama hao ni zile za siku zote - ujangili. Twiga wanaweza kuuawa kwa wepesi mno kwa kutumia risasi moja tu au waya, unasema mtandao wa taasisi ya uhifadhi wa Twiga GCF, ambayo ndiyo taasisi pekee duniani inayojishughulisha na uhifadhi wa wanyama hao, iliyoanzishwa mwaka 2009.

Watu zaidi na zaidi wanazidi kuamini kuwa uboho wa mifupa ya Twiga unaponya magonjwa yanayohusiana na ukimwi, alisema Peter, muongozaji wa wageni, ambaye ameshuhudia kupungua kwa idadi ya Twiga katika maeneo ya Mlima Meru, Kilimanjaro na mfumo wa ekolojia wa Ambosile kwenye mpaka kati ya Tanzania na Kenya.

Wataalamu kutoka taasisi ya GFC wanasema kilo moja ya uboho wa Twiga inaweza kuingiza hadi dola za Marekani 120. Hii siyo mara ya kwanza kwa wababaishaji kuuwa wanyama kwa visingizio vya kuwa viuongo vyao ni tiba ya maradhi, kuongeza nguvu za kiume na haiba ya mtu. Uwindaji wa tembo na faru kwa ajili ya pembe zao umewapelekea wanyama hao kwenye kingo za kutoweka kabisaa.

Punguzo la asilimia 40

Twiga, ambao wanapatikana katika mataifa 21 wamebainishwa kwenye orodha nyekundu ya shirika la uhifadhi wa mazingira asili IUCN kama wanyama wasio hatarini. Lakini kupungua kwa wanyama hao kwa asilimia 40 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, kunabainisha kwamba hatua za ulinzi zinahitajika hivi sasa kuliko huko nyuma.

Mwaka 1998 idadi ya Twiga ilikadiriwa kuwa 140,000, lakini kwa mujibu wa GFC, idadi hiyo ilikuwa imeshuka chini ya 80,000 kufikia mwaka 2012. Katika baadhi ya maeneo ambayo yanachukuliwa kama makaazi ya asili ya Twiga, idadi ya wanayama hao imepungua kwa hadi asimilia 65. Ikiwa Twiga watatoweka, dunia itapoteza moja ya spishi maarufu zaidi.

Watalii wakimlisha Twiga katika mbuga ya wanyama ya Seregeti.
Watalii wakimlisha Twiga katika mbuga ya wanyama ya Seregeti.Picha: Medizinische Hochschule Hannover

Shughuli za binaadamu

Pamoja na ujangili, wanyama hao wanakabiliwa pia na kitisho cha kutanuka kwa makaazi ya wanaadamu. Marlies Gabriel, anasema mashuhuda waliripoti juu ya kuchinjwa kwa wanyama hao na raia, na pia katika mbuga ya wanyama ya Serengeti, wageni waliripoti kukutana na mizoga ya Twiga.

Licha ya kupiga hatua kadhaa za kimaendeleo, Tanzania bado inaendelea kuwa miongoni mwa mataifa maskini zaidi duniani, na hivyo raia wengi wanapendelea kujihusisha zaidi na kilimo na ufugaji kuliko uhifadhi wa mazingira. Hilo limaanisha janga kwa wanyamapori wa eneo hilo.

Chini ya utawala wa rais wa kwanza Julius Nyerere katika miaka ya 1960 na 1970, adhabu ya kuwinda Twiga ilikuwa kifo, anasema Gabriel na kuongeza kuwa inatisha zaidi hivi sasa kuona kwamba wanyama hao wanatoweka taratibu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef