1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Twaendelea kutomtambua Museveni" - Upinzani Uganda

Admin.WagnerD28 Oktoba 2011

Upinzani nchini Uganda umesisitiza kuwa hawaitambui serikali ya Rais Yoweri Museveni na wataendelea kushiriki kwenye maandamano ya aina mbali mbali ili kuipinga serikali ambayo imekuwa madarakani kwa miaka 25 sasa.

https://p.dw.com/p/131EU
Kiongozi wa upinzani wa Uganda, Dk. Kiza Besigye.
Kiongozi wa upinzani wa Uganda, Dk. Kiza Besigye.Picha: AP

Miezi saba baada ya uchaguzi nchini Uganda, upinzani unasema kwa kipindi ambacho Rais Museveni amekuwa mamlakani wametambua hana mpango wa kubadilisha sera zake za uongozi ili kuyabadilisha maisha ya raia wa Uganda ambao wanazidi kuwa maskini kila kukicha ilhali baadhi ya watu walio serikalini wanazidi kutajirika.

Marais wa vyama vyote vitano vya upinzani nchini Uganda kwa pamoja wangali wanashikilia msimamo wao wa hapo awali kuwa chama tawala kiliiba kura kwa hivyo serikali ya Rais Museveni si halali.

Akizungumza kwa niaba ya marais wengine, Rais wa chama cha DP Norbert Mao amesema maisha ya raia wa Uganda yanazidi kuwa mabaya kila kukicha kwa sababu ya udororaji wa uchumu lakini serikali ya Uganda inawadanganya wananchi wake kuwa uchumi unazidi kuwa bora na ndio sababu wameamua.

"Ikiwa huwezi kuzibadilisha sera za serikali, basi lengo lako linafaa kuwa kuibadilisha serikali yenyewe. Hatuogopi kutangaza kuwa kuibadilisha serikali ni lengo ambalo tunalifuata."

Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda.Picha: DW/Schlindwein

Marais hao watano wa vyama vya upinzani leo waliunda kamati iitwayo "Joint Political Action Committee" ambayo itahakikisha kuwa inawaelimisha wananchi upungufu ulioko serikalini na mbinu zisizoambatana na sheria ambazo zinatumiwa na serikali kuwakandamiza ili wasizungumzie kutoridhika kwao na jambo lolote lile.

Upinzani unasema wakati umefika wa Uganda kukumbatia demokrasia ambayo inasisitiza mfumo wa vyama vingi.

"Hatuamini tuna demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa. Uganda imo chini ya utawala wa chama kimoja... hata idadi kubwa ya wabunge wa chama tawala walioko bungeni ni ishara kuwa tumo chini ya utawala wa chama kimoja na si ishara kuwa NRM ni chama kilicho na nguvu." Amesema Norbert Mao, akiongeza kuwa wataendelea na maandamano yao.

"Tumeamua kuendelea na kampeni za kuipinga serikali. NRM inadhani ikitufunga kwa tuhuma za uhaini inawaogopesha watu wengine wasishiriki kwenye maandamano yoyote ya kuipinga. Ukweli wa mambo ni kwamba raia wa Uganda hawamwogopi Rais Museveni tena. Hata wabunge wa chama chake hawamwogopi na ndio sababu wanampinga. Tunataka kuiambia serikali hatuogopi kuzivunja sheria sizizo za haki kama kumfungia mtu nyumbani mwake ili asitembee kwenda kazini. Tutaendelea na maandamano ya kutembea kwenda kazini kwa sababu hakuna sheria tunayoivunja tukitembea kwenda kazini."

Naye rais wa chama cha FDC, Dk. Kiiza Besigye, ambaye amezingirwa na polisi nyumbani kwake kwa wiki nzima kumzuia asishiriki kwenye maandamano ya kutembea kwenda kazini, anasema lazima atatembea Jumatatu ijayo.

Maandamano ya kutembea yalianza Aprili 2011 kama malalamiko dhidi ya ongezeko la bei ya chakula na petroli.

Mwandishi: Leylah Ndinda

Mhariri: Josephat Charo