1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunisia yajipatia serikali mpya

18 Januari 2011

Vyama vitatu vya upinzani vinawakilishwa katika serikali ya mpito ambayo wizara nne muhimu wamekabidhiwa wafuasi wa chama tawala cha zamani.Watunisia wanajiuliza eti hiki ni kiini macho?

https://p.dw.com/p/zz5k
Waziri mkuu Mohammed GhannouchiPicha: AP

Siku tatu baada ya kutimuliwa madarakani Zine El Abidine Ben Ali, serikali ya mpito imeshaundwa nchini Tunisia na mihimili ya kiimla kuanza kung'olewa. Waziri mkuu wa zamani na mpya, Mohammed Ghannouchi, ametangaza serikali ya umoja wa taifa, wakishiriki pia wanasiasa wa upande wa upinzani.

Kumeanza kupambazuka nchini Tunisia licha ya hali ya hatari-katika maduka mengi picha kubwa kubwa za rais aliyetimuliwa madarakani Ben Ali zimeshaondolewa ukutani na kutupwa jaani.

Mapambazuko ya kisiasa ndio kipa umbele cha serikali ya waziri mkuu Ghannouchi na serikali yake ya umoja wa taifa iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa.

Vyama vitatu vya zamani vya upinzani vinawakilishwa katika baraza hili la kwanza la mawaziri lililoundwa baada ya kung'oka madarakani Ben Ali- akiwemo Najib Chebbi, mpinzani mashuhuri kabisa nchini Tunisia aliyekabidhiwa wizara ya maendeleo ya kimkoa.

Tunesien Alltag Obst Gemüse Geschäft einkaufen
Watu wameanza kwenda madukani TunisPicha: DW

Waziri mkuu Mohammed Ghannouchi anajaribu kusawazisha hali ya mambo, ameivunja wizara ya mawasiliano iliyokuwa ikichukiwa mno na wananchi, amerejesha uhuru wa vyombo vya habari na kutangaza msamaha kwa wafungwa wote wa kisiasa.

Wadadisi wanajiuliza kama kuingizwa serikalini upande wa upinzani ni mbinu tuu za kisiasa au la. Kiongozi mmojawapo wa upinzani, Moncef Marzouki, anaepanga kutetea wadhifa wa rais uchaguzi utakapoitishwa, anasema serikali hii mpya si chochote isipokuwa kiini macho tu. Hata Hammam Hammami hakubaliani na uamuzi wa kukabidhiwa wafuasi wa chama tawala cha zamani wizara muhimu za mambo ya nchi za nje, mambo ya ndani, ulinzi na fedha. Chama cha kikoministi cha Hammami kilipigwa marufuku wakati wa utawala wa Zine al Abidine, na hata katika serikali ya sasa ya umoja wa taifa hakiwakilishwi ,sawa na wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiiislam.

Kuna wanaopinga kujumuishwa wafuasi wa chama tawala cha RCD, mfano wa huyu anaesema:

"Hatutoitambua serikali hii-ni sawa na serikali ya Ben Ali bila ya Ben Ali, imepambwa kidogo kidemokrasia."

NO FLASH Bürgerwehr in Tunesien
Raia walinda usalama mitaaniPicha: picture alliance / dpa

Waziri mkuu Mohammed Ghannouchi amewatetea mawaziri wa chama cha RCD, akisema mikono yao haijanona damu ya utawala wa Zine Al Abidine Ben Ali. Ameahidi wote waliosababisha watu kuuliwa watafikishwa mahakamani.

Mwandishi:Göbel,Alexander(HR)Rabat/Hamidou

Mpitiaji:Miraji Othman