1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya Uchaguzi Tanzania: Magufuli ndiye mshindi wa urais

31 Oktoba 2020

Tume ya uchaguzi Tanzania imemtangaza John Pombe Magufuli kama rais kwa muhula wa pili. Magufuli amepata ushindi mkubwa uliopingwa na upinzani kutokana na tuhuma kubwa za udanganyifu.

https://p.dw.com/p/3kgNR
Tansania Wahlen | Präsident John Magufuli
Picha: Ericky Boniphace/AFP

Kulingana na mwenyekiti wa tume hiyo Semistocles Koijage rais huyo ambaye atahudumu kwa kipindi chengine cha miaka mitano, amejizolea kura milioni 12.5 hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 84 akiwa amemshinda hasimu wake mkuu Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kwa zaidi ya kura milioni kumi. Tume ya uchaguzi imesema Lissu amepata kura milioni 1.9. Awali Lissu alikuwa amesema kwamba hatokubali matokeo hayo.

Naibu waziri wa ulinzi wa Marekani kuhusu masuala ya Afrika Tibor Nagy amesema wanaendelea kuwa na wasiwasi kuhusiana na kuvurugwa kwa demokrasia ya nchi hiyo. Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho chama tawala Tanzania tayari kilikuwa kimeshatangazwa kupata ushindi katika kisiwa cha Zanzibar kilicho na utawala wa ndani ambapo Hussein Mwinyi alitangazwa kuwa rais kwa kupata asilimia 76 ya kura.

Ubalozi wa Marekani unasema demokrasia imebinywa Tanzania

Maafisa kadhaa na wanachama wa vyama vya upinzani walikamatwa kisiwani Zanzibar Alhamis na mmoja anadaiwa kuwa hospitali akiwa na majeraha mabaya baada ya kudaiwa kupigwa na maafisa wa polisi ambao hawajatoa tamko lolote kuhusiana na tukio hilo.

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa taarifa kupitia ukurasa wake wa mtandao kijamii wa Twitter ukisema "udanganyifu na tofauti kubwa ya ushindi ni mambo yanayozua shauku kuhusiana na matokeo yaliyotangazwa."

Tansania Singida | Wahlen | Tundu Antiphas Lissu
Tundu Lissu aliyekuwa mgombea wa urais kupitia CHADEMAPicha: Said Khamis/DW

Ubalozi huo vile vile umesema uchaguzi huo ulikumbwa na visa vya wagombea na waandamanaji kukamatwa, mawakala wa vyama kutoruhusiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura, watu kupiga kura mara zaidi ya moja, kura zilizopigwa hata kabla uchaguzi kuanza na kufungwa kwa mitandao ya kijamii.

Maafisa wa tume ya uchaguzi hawakupatikana kuzungumzia madai hayo kwa wakati ila Jumatano tume hiyo iliklanusha kuwepo kwa kura bandia ikisema madai hayo si rasmi na hayana thibitisho.

Viongozi wa upinzani wameshindwa na wagombea wa chama tawala katika ngome zao

Kiongozi wa chama cha upinzani ACT Wazalendo Zitto Kabwe na kiongozi wa CHADEMA Freeman Mbowe ni miongoni mwa wagombea wengi wa upinzani waliopoteza viti vyao vya ubunge kwa wabunge wa chama tawala Chama Cha Mapinduzi CCM katika maeneo waliyokuwa wanagombea.

Afrika Tansania Dar es Salaam Wahlen
Mpigaji kura akishiriki zoezi hilo Dar es SalaamPicha: Emmanuel Herman/REUTERS

Magufuli ambaye anasifiwa na wafuasi wake kutokana na mtindo wake wa uongozi aliingia uongozini akiahidi kupambana na ufisadi na miradi yake ya miundo mbinu. Lakini makundi ya kutetea haki za binadamu yamekosoa hatua yake ya kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na pia jinsi anavyolishughulikia janga la virusi vya corona nchini humo ambapo amesema mara kadhaa kwamba maombi yameisaidia nchi hiyo kuviangamiza virusi hivyo.