1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsvangirai amshinda Mugabe katika duru ya kwanza lakini duru ya pili inahitajika

Kalyango, Siraj2 Mei 2008

Upinzani unakataa duru ya pili

https://p.dw.com/p/DsHS
Vtoile Silaigwana, katikati, naibu mkuu wa tume ya uchaguzi ya Zimbabwe ya (ZEC), akisoma matokeo ya uchaguzi wa baraza la wawakilishi Harare, Zimbabwe, April 3, 2008. Matokeo ya uchaguzi wa urais yanaonyesha kuwa Tsvangirai alimpiku Mugabe katika duru ya kwanza lakini analazimika kumshinda katika duru ya pili ili awe kiongozi kamili.Lakini chama chake kinapinga hilo.Picha: picture-alliance/ dpa

Zoezi la kuhakiki matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi Machi nchini Zimbabwe leo Ijumaa umeingia siku yake ya pili katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Harare.

Zoezi lilianza jana alhamisi ambapo tume ya uchaguzi iliwaambia wajumbe wa vyama vya kisiasa kuwa kiongozi wa upinzani wa MDC Morgan Tsvangira alishinda kwa asili mia 48 huku rais Mugabe kujinyakulia asili mia 43.Hata hivyo chama cha MDC kinashuku matokeo hayo kikidai kuwa kiongozi wao alipata asili mia 50.3.

Mazunguzo ya vyama vyote vya kisiasa nchini Zimbabwe ambayo yanafanywa na tume ya uchaguzi nchini humo yaliyoanza jana leo yameingia siku ya pili.

Hata hivyo yamegubikwa na mvutano wa kiasi gani cha ushindi wa upande unaotazamiwa kuwa umeshinda.

Msemaji wa chama cha upinzani George Sibotshiwe amesema leo mjini Harare kuwa hesabu za tume ya uchaguzi za matokeo ya urais ambazo ,zinampa ushindi Morgan Tsvangirai wa asili mia isiozidi 48. Huku Mugabe akiwa amepata 43 asili mia.

Ikiwa hayo ndio matokeo ya kweli ina maana kuwa duru ya pili itahitajika kwa sababu hakuna aliepata kiwango kinachohitajika kuepuka duru hiyo.Na waziri wa mashauri ya kigeni wa Senegal, Chikh Tidiane Gadio, amesema kuwa Bw Mugabe yuko tayari kushiriki katika duru ya pili.Waziri huyo alikutana na Mugabe jana alhamisi mjini Harare.

Lakini upande wa upinzani unapinga kuwepo kwa duru ya pili ukidai kuwa kiongozi wao alipataasili mia 50.3 ya kura zote kwa mujibu wa hesabu zao.Chama hicho kinatoa hoja kuwa kutokan na matokeo walionayo hakuna haja ya kufanyika kwa duru ya pili.Mjumbe wa Tsvangirai katika mazungumzo hayo,Chris Mbanga,kabla ya kuingia katika chumba cha mkutano leo asubuhi mjini Harare, amesema hakubaliani na idadi inayotolewa na tume ya uchaguzi.Ameongeza kuwa tume ya uchaguzi italazimika kuwapa ushahidi wa kutosha unaoonyesha kuwa idadi walio nayo si ya ukweli.

Tsvangirai mwenyewe,ambae kwa sasa yuko Afrika Kusini anasema nini kuhusu ushindi aliopewa ambao hesabu ni kasoro ya kiwango cha kumpa ushindi wa bayana,'Unaweza kusema kuwa hayo ni makosa ya kihisabati tu.Tulipotangaza matokeo ya asili mia 50.35 tulisema kuwa kuna makosa ya asili mia 0.5,lakini kwa kweli taarifa zaidi zinaonyesha kuwa tuko juu zaidi ya asili mia 50. Hali ya duru ya pili inabuniwa tu na Mugabe pamoja na chama chake cha ZANU PF', asema Tsvangirai.

Duru ya pili sio tu inakataliwa na upande wa upinzani lakini pia na makundi yanayotetea haki za binadamu.Makundi hayo yanatoa hoja tofauti na za wanasiasa.Mfano Tiseke Kasambala kutoka kwa kundi la Human Rights Watch,ambae alikwenda Zimbabwe kisiri kwa ziara ya kikazi,'Tunaamini kuwa duru ya pili haifai wakati huu kutokana na aina ya ghasia ambayo inashudiwa ikiwa inaendelea. Jamii ya kimataifa,Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ni lazima zikariri kuwa duru ya pili haiwezi kufanyika katika mazingira kama hayo.Na vilevile wakariri kuwa ni hadi pale ghasia zimekomeshwa na kuwa amani imetanda ndio wafikirie uwezekano wa kufanyika kwa duru ya pili',amesema Kasambala.

Huku hali hiyo ikiwa inaweza kusababisha tena kutoelewana lakini upande wa Mugabe waonekana hauna wasiwasi yoyote. waziri mmoja Emmerson Mnangagwa amesema kuwa zoezi lilikuwa sawa.