1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsvangirai afika mahakamani mjini Harare

Oummilkheir13 Machi 2007

Walimwengu walaani matumizi ya nguvu ya polisi wa Zimbabwe dhidi ya "maandamano ya amani."

https://p.dw.com/p/CHIG
Rais Robert MUgabe wa Zimbabwe
Rais Robert MUgabe wa ZimbabwePicha: dpa

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kinawalaumu polisi kwa kumpiga vibaya sana kiongozi wao Morgan Tsvangirai anaeshikiliwa jela na kuahidi kuzidisha vishindo hadi rais Robert Mugabe anang’oka madarakani.

„Tsvangirai anashikiliwa katika kituo cha polisi cha Borrowdale,akiwa katika hali mahtuti baada ya kupigwa vibaya sana“ amesema Thokozani Khupe,ambae ni makamo mwenyekiti wa chama klinachopigania mageuzi ya kidemokrasi MDC.“Amezimia mara tatu akiwa kizuwizini-„ ameongeza kusema bwana Khupe.

Mashirika ya haki za binaadam yanalalamika pia kwamba mkuu huyo wa MDC na watu wengineo waliokamatwa wameteswa wakiwa kizuwizini.

Shirika la Amnesty International lenye makao yake makuu mjini London limezungumzia wasi wasi na hofu kufuatia matumizi ya nguvu yaliyogharimu maisha ya mtu mmoja nchini Zimbabwe.

Jumuia ya kimataifa imelaani matumizi hayo ya nguvu.Ujerumani ambayo ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya ichapisha taarifa inayolaani tunanukuu“kukandamizwa kila wakati nchini Zimbabwe uhuru wa mtu kutoa maoni yake,watu kukutana na haki nyenginezo za kimsingi.“Mwisho wa kunukuu taarifa ya umoja wa ulaya iliyotangazwa leo mjini Berlin.

Mawakili wa mwenyekiti huyo wa chama kikuu cha upinzani Morgan Tsvangirai hawakuwaruhusu kumuona mteja wao na watu wengine mashuhuri wa MDC waliokamatwa jumapili iliyopita.

Alec Muchadehama,mmojawapo wa mawakili hao amesema polisi wamedharau amri iliopitishwa jana usiku na korti kuu ya Zimbabwe,inayotaka mawakili waruhusiwe haraka kuwatembelea wanasiasa hao na kupatiwa pia matibabu.

Wanaharakati wa kongamano la „Save Zimbabwe“- wakiwemo wafuasi wa upande wa upinzani,haki za binaadam,na wachamngu wamepania kuendeleza shinikizo lao mpaka rais Mugabe anang’oka madarakani.

Morgan Tsavingari alitarajiwa kufika mahakamani hii leo asubuhi.Jaji Chinemberi Bhunu wa mahakama kuu mjini Harare ameamuru mwenyekiti huyo wa MDC na dazeni kadhaa ya wafuasi wake waliokamatwa jumapili wafikishwe mahakamani haraka,la sivyo waachiliwe huru.

Mmojawapo wa mawakili wa Morgan Tsavingirai,Alec Muchadehama amewaambia maripota wa shirika la habari la Ufaransa AFP ,wanaelekea mahakamani kuwasubiri wateja wao,baada ya kukataliwa kuwaona jana usiku.