1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsipras na Merkel kukutana kutafuta kuboresha uhusiano

Admin.WagnerD23 Machi 2015

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras anaizuru Ujerumani hii leo kwa mara ya kwanza tangu kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu kwa mazungumzo na mwenyeji wake Kansela Angela Merkel yanayotarajiwa kuboresha uhusiano kati yao.

https://p.dw.com/p/1EvRz
Picha: picture-alliance/AA

Mazungumzo kati ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na kiongozi huyo wa Ugiriki wa chama cha mrengo wa kushoto mjini Berlin yanatarajiwa kutuwama katika suala la mgogoro wa kiuchumi unaoikumba Ugiriki ambayo inazongwa na madeni.

Katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya wiki iliopita, Merkel na viongozi wengine wa nchi wanachama wa umoja huo, walimtaka Tsipras kuwasilisha katika siku chache zijazo hatua za jinsi serikali yake ambayo iliingia madarakani kwa ahadi za kusitisha mpango wa kubana matumzi, itakavyopunguza bajeti yake na kuongeza kodi ili iweze kupewa mkopo zaidi wa uokozi.

Ugiriki yaelezwa itabidi ikaze mkwiji

Serikali hiyo mpya ya Ugiriki imejikuta katika uhusiano tete na nchi nyingi za umoja wa Ulaya hasa Ujerumani kutokana na msimamo wa utawala wa Tsipras kutaka kulegezewa masharti na wakopeshaji wake ya kupokea na kulipa madeni jambo ambalo Ujerumani ambayo ni mojawapo ya wakopeshaji wakuu imesisitiza Ugiriki haina namna nyingine ila kuchukua mkondo mgumu wa kubana matumizi na kufanya mageuzi ya kiuchumi.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakikutana Brussels kuijadili Ugiriki
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakikutana Brussels kuijadili UgirikiPicha: Reuters/E. Dunand

Naibu Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel amekiambia kituo cha televisheni cha Ujerumani ARD kuwa anatumai mkutano huo kati ya Merkel na Tsipras utaashira mwanzo mpya wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Tsipras amemuonya Merkel katika barua aliyomuandikia kabla ya ziara ya leo kuwa Ugiriki haitaweza kuyalipa madeni yake bila ya kupata usaidizi wa kifedha kutoka Umoja wa Ulaya na kumtaka kiongozi huyo wa Ujerumani kutoruhusu matatizo aliyoyataja madogo ya kifedha kuiathiri zaidi Ugiriki na bara Ulaya kwa jumla.

Ugiriki yahitaji msaada wa kifedha

Hata hivyo Rais huyo wa Ugiriki amesema anatumai mkutano huo wa leo utakuwa fursa nzuri kwake na Merkel kuzungumza bila ya shinikizo ya kufikia makubaliano ya mageuzi ya kiuchumi na ni muhimu kuweza kuzungumzia masuala mbali mbali yanayoiathiri bara Ulaya na jinsi ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/F. Bensch

Maafisa wa Ujerumani wamekuwa wakilalamika kuwa wenzao wa Ugriki wamekuwa wakionyesha dhamira ya kutekeleza masharti yaliyopo kuhusu suala la mikopo lakini baadaye wanakwenda kinyume ya makubaliano hayo hadharani na kuzusha shaka iwapo nchi hiyo ina nia kweli ya kuyaheshimu masharti ya wakopeshaji au la.

Serikali ya Ujerumani imesisitiza suala la ulipaji fidia kutokana na kukaliwa kwa Ugiriki na wanazi wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia halitakuwa katika ajenda ya mazungumzo ya leo ambayo yanatarajiwa kuanza rasmi saa kumi na moja jioni saa za Ulaya ya Kati.

Mwandishi:Caro Robi/Ap/Afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman