1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trumpa akataa suluhisho la kidiplomasia Korea Kaskazini

Grace Kabogo
31 Agosti 2017

Rais wa Marekani, Donald Trump na waziri wake wa ulinzi wametoa kauli zinazotofautiana kuhusu Korea Kaskazini, huku Trump akisema mazungumzo sio jibu la kuondoa wasiwasi uliopo wa makombora yanayorushwa na nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2j8Mf
USA Donald Trump und James Mattis
Picha: Reuters/J. Ernst

Mkanganyiko wa viongozi hao wawili umezusha maswali kuhusu kama Marekani inapanga kukabiliana na mzozo huo. Trump ameyatoa matamshi hayo siku moja baada ya Korea Kaskazini kurusha kombora lililopita katika anga ya Japan, kitendo kilichokosolewa vikali na jumuia ya kimataifa.

Trump ambaye wiki iliyopita alimsifia kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un kwamba ameanza kuiheshimu Marekani, ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba ''Marekani imekuwa ikizungumza na Korea Kaskazini na kuilipa fedha za kutuhujumu kwa miaka 25 na kwamba mazungumzo sio jibu!''

Trump alikuwa akimaanisha kiasi che Dola bilioni moja kilichotolewa kwa Korea Kaskazini kati ya mwaka 1995 na 2009 kwa ajili ya chakula na mafuta. Msaada huo ulikuwa sehemu ya mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini ambao ulikiukwa. Nchi hizo mbili hazijawahi kufanya mazungumzo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini tangu mwaka 2012.

Nordkorea Raketenstart
Moja ya makombora ya Korea KaskaziniPicha: Reuters/KCNA

Trump amesema anapinga hatua ya kufanya mazungumzo na Korea Kaskazini kuhusu mpango wake wa makombora ya nyuklia. Kauli hiyo ya Trump inaonyeshaya kutoa kitisho cha kuongeza vikwazo zaidi kwa Korea Kaskazini au hata kufanya maandalizi ya operesheni za kijeshi.

Matamshi hayo yanatofautiana na waziri wake wa ulinzi, Jim Mattis, ambaye saa chache baadae alipoulizwa na waandishi habari iwapo Marekani ilikuwa inajiondoa katika suluhisho la kidiplomasia na Korea Kaskazini, Mattis alijibu ''hapana.'' Mattis ameyatoa matamshi hayo, kabla ya kukutana na waziri mwenzake kutoka Korea Kusini mjini Washington.

Hatuna nia ya kujiondoa

''Kamwe hatujajiondoa katika suluhisho la kidiplomasia. Tunaendelea kushirikiana pamoja na mimi na waziri tuna jukumu la kuyalinda mataifa yetu, watu wetu na maslahi yetu, masuala ambayo tuko hapa kuyajadili na kuangalia maeneo yote ambayo tunaweza kushirikiana,'' alisema Mattis.

Mattis amesema tayari wana ushirikiano imara na kamwe hawajawahi kulalamika. Katika wiki za hivi karibuni, Korea Kaskazini imetishia kufanyika majaribio zaidi ya makombora kuelekea katika kisiwa cha Guam kinachomilikiwa na Marekani kwenye Bahari ya Pasifiki.

Russland Moskau Rex Tillerson und Sergei Lawrow
Rex Tillerson akiwa na Sergei LavrovPicha: picture-alliance/dpa/TASS/S. Krasilnikov

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo tayari limeiwekea Korea Kaskazini aina saba ya vikwazo, limesema vitendo vya uchokozi vinavyofanywa na nchi hiyo, sio kitisho tu katika Rasi ya Korea, bali kwa mataifa yote wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov ameisihi Marekani kujizuia na vitendo vyovyote vile vya kijeshi katika Rasi ya Korea, ambavyo vinaweza kusababisha madhara ambayo hayakutarajiwa. Katika mazungumzo ya simu kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson, Lavrov amesema Urusi pia inaamini kuwa suala la kuongeza shinikizo la vikwazo zaidi, huenda lisifanikiwe.

Maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Marekani, akiwemo Tillerson, Mattis pamoja na Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa majeshi ya Marekani, Jenerali Joseph Dunford na Mkurugenzi wa shirika la ujasusi, Dan Coats watakuwa na vikao na wawakilishi wa baraza la Congress Septemba 6.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, Reuters
Mhariri: Bruce Amani