1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ndio chaguo la Marekani

Sylvia Mwehozi
9 Novemba 2016

Wamarekani wameamua,na Trump ndie chaguo lao.Rais huyo mteule wa Marekani Donald Trump amesema atakuwa "rais wa wamarekani wote".

https://p.dw.com/p/2SOhW
US-Präsidentschaftswahl 2016 - Sieg & Rede Donald Trump
Picha: Getty Images/S. Platt

Donald Trump anaahidi kuyatibu majeraha ya nchi huku akimsifu mpinzani wake Hillary Clinton kwa utumishi wake kwa umma kwa muda mrefu katika hotuba yake ya ushindi aliyoitoa katika jiji la New York. 

Donald Trump, rais mteule atakayekuwa wa 45 katika hesabu za marais wa Marekani akiieleza hadhira ya wafuasi wake baada ya kupata ushindi katika uchaguzi uliofanyika hapo jana Jumatano. Ushindi wa Trump dhidi ya mpinzani wake Hillary Clinton umewashangaza watu wengi duniani na unahitimisha utawala wa miaka nane wa chama cha Democrats na kuipeleka Marekani katika njia wengi wakiseman isiyojulikana.

Wafuasi wa Republican wakifurahia ushindi wa Donald Trump
Wafuasi wa Republican wakifurahia ushindi wa Donald TrumpPicha: Reuters/J. Roberts

Akiongozana na familia yake mbele ya wafuasi waliojawa na furaha , Trump kwanza amemsifu mpinzani wake bi Clinton kwa utumishi wake wa muda mrefu na akasema kwamba amepokea simu kutoka kwa mpinzani wake huyo ya kumpongeza baada ya matokeo ya Pennysylvania ambalo limekuwa likipiga kura kwa ajili ya Democratic tangu mwaka 1992. Trump amesema kwamba "nimepokea simu kutoka kwa Clinton. Ametupongeza, ni kwa ajili yetu, kwa ajili ya ushindi wetu na ninampongeza yeyena familia yake kwa namna alivyopambana katika kampeni. Amepambana kweli. Hillary amefanya kazi kwa bidii na kwa muda mrefu na tuna deni kubwa kwake kwa mchango wake katika nchi yetu".

Mfanyabiashara huyo ameahidi kufanya kazi kwa usawa na kila mmoja yakiwemo mataifa yote ambayo yatakuwa tayari kufanya kazi naye, akiongeza kwamba Marekani itakuwa na mahusiano mazuri. Rais huyo mteule sasa anacho kibarua cha kuwaunganisha wamarekani waliogawanyika baada ya kumalizika kwa uchaguzi. "Sasa ni wakati wa Marekani kutibu majeraha ya mgawanyiko uliotokea, tunahitaji kushirikiana . Kwa republicani wote, wanademocratis wote na wale walio wasio na upande wowote nasema ni muda sasa kwetu kuungana pamoja kama wamarekani. Ni muda sasa", amesema Trump.

Joey Marzinsky mfuasi wa Hillary Clinton akishikwa na mshangao wakati wa matokeo
Joey Marzinsky mfuasi wa Hillary Clinton akishikwa na mshangao wakati wa matokeoPicha: Reuters/D. Becker

Kwa mujibu wa makadirio ya kituo cha habari cha Fox na shirika la habari la Associated Press Trump alijikusanyia kura za kutosha kati ya kura 270 za wajumbe zilizokuwa zikitajika yeye kushinda muhula wa miaka minne. Pamoja na hilo vituo vingi pia vimetabiri kwamba warepublican watadhibiti baraza la wawakilishi la Marekani pamoja na baraza la seneti. Trump amefanikiwa kushinda katika majimbo yaliyokuwa yakingombaniwa  yakiwemo Florida, na Ohio .

Akiingia Ikulu pasipo kuwa na uzoefu wowote wa uongozi, Trump atakuwa mwenye miaka 70 atakuwa ni rais mwenye umri mkubwa kuwahi kuliongoza taifa hilo.

Kwa upande mwingine Bi Hillary Clinton alitarajiwa zaidi kuwa mwanamke wa kwanza kuliongoza taifa hilo na baada ya matokeo haya ndoto zake zimeyeyuka na amekataa kutoa hotuba ya baada ya matokeo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters

Mhariri: Saumu Yusuf