1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na spika wa baraza la wawakilishi wanazidi kuzozana

Yusra Buwayhid
18 Januari 2019

Uhasama kati ya rais Donald Trump na spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi umezidi kupamba moto baada ya Trump kumzuia Pelosi kutumia ndege ya kijeshi kwa safari yake ya kikazi ya kwenda Afghanistan.

https://p.dw.com/p/3Bl8P
Kombobild Pelosi vs Trump

 

Mzozo baina ya viongozi hao wa Marekani umezidi makali baada ya Nancy Pelosi ambaye ni spika wa Baraza la Wawakilishi, kupendekeza kwamba Rais Donald Trump aahirishe hotuba yake ya hali ya taifa, ambayo ilikuwa ifanyike January 29, kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha za maandalizi. Trump alimjibu Pelosi kwa barua, na kumwambia kuwa naye hana ruhusa ya kutumia ndege ya serikali kwa safari yake ya kwenda Afghanistan.

Trump amesema safari ya hiyo ni shughuli inayohusu mahusiano ya umma- licha ya kwamba hata yeye binafsi alifanya ziara ya aina hiyo katika eneo lenye vita. Trump amesema itakuwa vyema kwa Bi Pelosi kubaki Marekani na kujadili suala la kufungua tena shughuli za serikali.

Kumnyima mbunge wa ngazi ya juu ndege ya kijeshi, achia mbali spika wa Baraza la Wawakilishi ambae ni wa pili kwa cheo katika serikali ya Marekani, ambaye anataka kutembelea eneo la vita- ni kitu cha nadra sana. Wabunge walishangazwa na uamuzi huo.

Msemaji wa Pelosi Drew Hammill amesema spika huyo alipanga kwenda Afghanistan na Brussels kuwashukuru wanajeshi kwa huduma yao, na kupokea taarifa kutoka kwa wanajeshi walio huko juu ya usalama wa taifa na taarifa nyingine za upelelezi.

Hammill amekumbusha kwamba Trump alisafiri kwenda Iraq wakati tayari shughuli za serikali zikiwa zimeshafungwa.

USA Arlington Präsident Trump Ankündigung zur Raketenabwehr
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/K. Lamarque

Trump pia aahirisha safari ya Davos

Trump amesema shughuli za serikali zitaendelea kufungwa hadi Baraza la Congress limpatie dola bilioni 5 ili ajenge ukuta katika mpaka wa Mexico na Marekani.

Nancy Pelosi amesema yuko tayari kujadili suala la fedha za kuimarisha usalama katika mpaka wa Marekani na Mexico mara baada ya shughuli za serikali kufunguliwa tena, lakini amesema wabunge wa chama Democratic wamesema bado wanapinga mpango wa Trump wa kujenga ukuta.

Kutokana na kwamba kuna watumishi wa serikali 800,000 ambao hawakupokea mishara yao, Ikulu ya Marekani pia imeripoti kwamba Trump amefuta safari yake na ujumbe wake ya kwenda katika Kongamano la Kimataifa la Uchumi huko Davos, Uswisi. Trump alikuwa afungue mkutano wa mwkaa huu.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap/afp

Mhariri: Gakuba, Daniel