1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Clinton waongoza, Rubio ajitoa

Mohammed Khelef16 Machi 2016

Donald Trump wa Republican amembwaga Marco Rubio katika jimbo la Florida lakini ameshindwa na mgombea asiye maarufu Ohio, huku Hillary Clinton wa Democratic akiendelea kuwa mbele ya Bernie Sanders.

https://p.dw.com/p/1IDte
John Kasich mshindi wa kura za maoni jimbo la Ohio kwa tiketi ya Republican.
John Kasich mshindi wa kura za maoni jimbo la Ohio kwa tiketi ya Republican.Picha: Reuters/A. Josefczyk

Licha ya ushindi wa Trump wa Jumanne ya jana kuzidi kumuhakikishia nafasi yake ya kuwa mgombea wa Republican, Gavana John Kasich wa Ohio alifanikiwa kumzuwia bilionea huyo mwenye kauli za kutatanisha kuwika kwenye jimbo lake.

Wapiga kura vijana kwenye jimbo hilo muhimu waliamua kumkataa Trump, ambaye amekuwa akijizolea umashuhuri kwa kauli zake dhidi ya wale anaowaita wageni, Waislamu na wahamiaji.

"Imekuwa dhamira yangu kuwafanya vijana wa nchi hii kumuangalia mtu na kuingia kwenye siasa, ingawa muda mrefu watu walinipuuza. Watu wa Ohio walikuwa wakisema: "Kwa nini hawamuiti?" Tunafahamu hayo, lakini tunapiga hatua moja baada ya nyengine na leo nawahakikishieni kuwa sitarudi nyuma kuelekea safari ya ofisi hii kubwa kabisa katika nchi," gavana huyo aliwaambia wafuasi wake.

Ushindi wa Kasich ni wa kwanza kwake tangu kura hizi za mchujo za jimbo kwa jimbo kuanza wiki sita zilizopita. Hata hivyo, sio tu kuwa Trump alishinda kwenye majimbo ya North Carolina na Illinois, bali pia Florida, jimbo la mpinzani wake, Rubio, ambaye sasa amelazimika kujiengua moja kwa moja kwenye kinyang'anyiro hicho, hivyo kuwaweka Trump na Seneta Ted Cruz kuwa washika bendera.

'Tsunami ya Kisiasa'

Akiyaaga mashindano hayo, Rubio alisema alikuwa amejaribu kujenga daraja katika nchi na katika chama baada ya kutekwa nyara na kupasuliwa na kampeni za uasi za Trump, ambaye anamlaumu kwa kuiletea Marekani kile alichokiita "tsunami ya kisiasa."

Kwa upande wa Democratic, Hillary Clinton ameshinda pia kwenye majimbo yote manne: Florida, North Carolina, Illinios na Ohio, na kumuwacha mbali hasimu wake, Bernie Sanders.

"Usiku huu ni wazi kabisa kwamba ni moja ya kampeni zenye mafanikio makubwa kabisa maishani mwetu. Rais ajaye ataingia Ikulu mwezi Januari, akae kwenye kiti chake na kuanza kufanya maamuzi ambayo yataathiri maisha ya kila mmoja wetu kwenye nchi hii, na hakika kwenye dunia nzima."

Ushindi wa jana wa Clinton ulikuwa mkubwa, huku kwenye jimbo kama Florida akijizolea asilimia 65 dhidi ya 33 za Sanders, na ni katika jimbo la Illinois tu ambako Sanders alishindwa kwa asilimia moja.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman