1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Mashambulizi ya Syria yalitimiza lengo

Caro Robi
14 Aprili 2018

Rais wa Marekani Donald Trump amesifu mashambulizi ya anga yaliyofanywa leo alfajiri dhidi ya utawala wa Syria yaliyotekelezwa kwa pamoja na Marekani, Uingereza na Ufaransa akisema lengo lao lilifanikiwa.

https://p.dw.com/p/2w3QK
USA - Trump ordnet Militärschlag auf Syrien an
Picha: picture-alliance/dpa/AP/S. Walsh

Maafisa wa nchi za magharibi wamesema mfululizo wa mabomu na makombora ya kutokea angani kwenda ardhini yameshambulia maeneo yanayohusishwa na uzalishaji wa silaha za kemikali, katika kulipiza kisasi cha shambulizi la gesi ya sumu wiki moja iliyopita kwenye eneo la mji unaoshikiliwa na waasi wa Douma, katika kitongoji cha Damascus.

Trump kama kawaida yake alitumia ukurasa wake wa Twitter kupongeza mashambulizi hayo na kuzisifu Uingereza na Ufaransa kwa hekima na nguvu ya jeshi lake na kuongeza kuwa lengo limetimia. Waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis ameyaita mashambulizi hayo kuwa ya wakati mmoja na hakuna hatua zaidi za kijeshi zilizopangwa kwa hivi sasa

Syria yasema haitetereki

Rais wa Syria Bashar al Assad amesema mashambulizi hayo dhidi ya utawala wake, yanawapa nguvu ya kupambana zaidi dhidi ya ugaidi katika kila kona ya Syria na kuongeza nchi za magharibi zimefanya mashambulizi hayo baada ya kuona zimeshindwa kuwa na ushawishi na kuidhibiti mzozo wa Syria.

Zypern Britischer Kampfjet vor Einsatz
Ndege za kijeshi za Uingereza zikielekea kuishambulia SyriaPicha: picture-alliance/AP Photo/L. Matthews

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema anaunga mkono mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani, Ufaransa na Uingereza nchini Syria akiyataja muhimu na yanayostahili. Merkel amesema mashambulizi hayo ya angani yaliyofanywa leo asubuhi yanapaswa kuwa onyo kwa utawala wa Syria kutoendelea kutumia silaha za sumu.

Wiki hii Kansela huyo wa Ujerumani alisema nchi yake haitashiriki katika hatua ya kijeshi Syria lakini itaunga mkono hatua za kijeshi zitakazochukuliwa na nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana leo kwa ombi la Urusi ili kujadili mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani, Ufaransa na Uingereza nchini Syria ili kukabiliana na shambulizi linaloshukiwa kuwa la kemikali.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye atalihutubia baraza hilo, hapo awali alisema kwamba nchi zote zinapaswa kujizuia katika mazingira haya magumu na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea na kufanya hali ya raia wa Syria wanaoteseka kuwa mbaya zaidi.

Ni kipi kitafuata?

Urusi ilionya kwamba hatua zozote za kijeshi dhidi ya Syria itakuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa kwakuwa zimetekelezwa bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Syrien Damaskus Proteste nach Militärschlag
Wanajeshi na raia wa Syrian wakiandamana kupinga mashambuliziPicha: Reuters/O. Sanadiki

Katika kikao cha baraza hilo siku ya Ijumaa, Marekani, Uingereza na Ufaransa zilitetea hoja ya hatua za kijeshi zikidai kuwa majeshi ya rais Bashar al-Assad yametumia gesi za sumu mara kadhaa na kukiuka sheria za kimataifa.

Shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya silaha za sumu OPCW limesema linaendelea na uchunguzi wa kutathmini matumizi ya silaha za sumu Syria.

Naye kiongozi wa kidini mwenye ushawishi mkubwa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameyalaani vikali mashambulizi hayo ya angani na kuzitaja Marekani, Ufaransa na Uingereza 'wahalifu'. Uongozi wa Palestina pia umelaani mashambulizi hayo na kuyataja ukiukaji wa uhuru wa kujitawala wa Syria.

Umoja wa Ulaya umezitolea wito Iran na Urusi kusaidia katika kuzuia matumizi zaidi ya silaha za sumu Syria ukionya kuwa utaziwekea nchi hizo vikwazo zaidi vya kiuchumi. Katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema anaunga mkono mashambulizi dhidi ya utawala wa Syria kwani utapunguza uwezo wa Syria kuwashambulia watu wake kwa silaha za sumu. Saudi Arabia pia imeyaunga mkono.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Sylvia Mwehozi