1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kusaini amri kuu za kiutendaji

Grace Kabogo
25 Januari 2017

Rais wa Marekani, Donald Trump leo atasaini amri kuu za kiutendaji za kupiga marufuku wahamiaji kuingia nchini humo, kusimamishwa kutolewa visa kwa wananchi wa Syria pamoja na mataifa sita ya Mashariki ya Kati na Afrika.

https://p.dw.com/p/2WMIO
US Präsident Donald Trump spricht zur Vereidigung weiterer Minister
Picha: Picture-Alliance/dpa/A. Harnik

Taarifa mbalimbali zimeeleza kuwa Trump ambaye aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba leo itakuwa ''siku kubwa'' iliyopangwa kwa usalama wa kitaifa, anatarajiwa kupiga marufuku kwa miezi kadhaa wakimbizi kuingia Marekani, isipokuwa kwa waumini wachache wa dini wanaokimbia mateso.

Wasaidizi wa Trump pamoja na wataalamu wamesema amri nyingine itazuia utoaji wa visa kwa mtu yeyote anayetokea nchini Syria, Iraq, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen. Stephen Legomsky, aliyekuwa mshauri mkuu wa Idara ya Uraia wa Marekani na Uhamiaji katika utawala wa Rais Barack Obama, amesema rais ana mamlaka ya kudhibiti wakimbizi kuingia na kuzuia kutoa visa kwa nchi maalum, kama utawala utaamua kufanya hivyo kwa maslahi ya umma.

Grenze USA - Mexiko
Doria ikiendelea kwenye mpaka wa Marekani na MexicoPicha: Getty Images/AFP/S. Huffaker

Wakati wa kampeni za kuwania urais, Trump aliahidi kuyafanyia mageuzi masuala ya uhamiaji nchini Marekani. Pia aligusia ujenzi wa ukuta kati ya Mexico na Marekani ili kuimarisha usalama katika mpaka huo na kuzuia wahamiaji haramu kuingia nchini humo kama sehemu ya kupiga vita ugaidi.

Amri ya kujenga ukuta kati ya Mexico na Marekani pia itasainiwa

Trump ambaye anatarajiwa kuzuru wizara ya usalama wa ndani baadae leo, pia atasaini pendekezo lake la kujenga ukuta katika mpaka wa Mexico na Marekani. Wizara hiyo inahusika na masuala mbalimbali ikiwemo uhamiaji na usalama wa mipakani. Sera ya Trump ni kujenga ukuta wenye urefu wa kilomita 3,200 katika mpaka wa mataifa hayo mawili.

Mapema jana Trump alisaini memorandam ya urais kuidhinisha ujenzi wa mradi wenye utata wa bomba la mafuta ghafi kutoka Canada kwenda Marekani pamoja na bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka kwenye visima vya ndani kwa watumiaji wa Marekani unaojulikana kama Dakota Pipeline. Ujenzi wa mabomba yote hayo ulizuiwa na mtangulizi wake, Barack Obama, kutokana na wasiwasi wa kimazingira.

USA TPP Protest
Wanaharakati wakiandamana kuupinga mkataba wa TPPPicha: Getty Images/AFP/

Siku ya Jumatatu, Trump alisaini agizo la serikali la kuiondoa rasmi Marekani kwenye Mtakaba wa ushirikiano wa biashara huria katika eneo la Bahari ya Pasifiki, TPP. Pia alizionya kampuni za Marekani zitachukuliwa adhabu kama zitahamisha shughuli za uzalishaji nje ya Marekani. Mkataba wa TPP ulijadiliwa chini ya utawala wa Obama, lakini haukuridhiwa na bunge.

Trump pia ameliamuru Shirika la Ulinzi wa Mazingira la Marekani, EPA, kusitisha kwa muda mikataba yote pamoja na kuacha mawasiliano na vyombo vya habari. EPA, hutoa na kusimamia ruzuku za mabilioni ya Dola kila mwaka, ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa mazingira, usafishaji na utafiti. Agizo hilo limetolewa baada ya Trump kutoa amri ya rais inayopiga marufuku kwa muda serikali kuwaajiri wafanyakazi, isipokuwa tu jeshini.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, Reuters, DPA, AP, DW http://bit.ly/2jY5A7y
Mhariri: Josephat Charo