1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuimarisha kampeni ya kijeshi Afghanistan

Yusra Buwayhid
22 Agosti 2017

Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza mkakati mpya wa kijeshi kuhusu Afghanistan na eneo la Asia ya Kusini, unaorudi nyuma katika kulijenga taifa hilo na badala yake kipaumbele kitakuwa kuwasaka na kuwaua magaidi.

https://p.dw.com/p/2icKz
USA Fort Myer Trump Rede Afghanistan Strategie
Picha: Getty Images/M. Wilson

Mkakati huo mpya umetangazwa katika wakati ambapo wanamgambo wa kundi la Taliban wanaongeza mashambulizi yao katika wilaya za maeneo kadhaa ya nchi, na huku Marekani ikiwa inaelekea kutimiza miaka 17 ya kuwepo kijeshi nchini Afganistan.

Trump amesema malengo makuu ya mkakati huo ni kuliharibu kundi linalojiita Dola la Kiislam IS, kulisagasaga kundi la al-Qaeda na kulizuia kundi la Taliban kuidhiti Afghanistan.

"Hatujengi tena taifa. Tunawaua magaidi. Hatua inayofuata ya mkakati wetu mpya ni kubadili mbinu na jinsi ya kukabiliana na Pakistan. Hatuwezi tena kukaa kimya kuhusu namna  Pakistan inavyoyapa usalama mashirika ya kigaidi, Taliban, na makundi mengine ambayo yamekuwa tishio kwa kanda nzima na zaidi ya hapo. Pakistan itafaidika kwa kushirikiana na jitihada za Marekani huko nchini Afghanistan," amesema rais wa Marekani, Donald Trump.

Muda mchache baada ya hotuba hiyo ya Trump iliyorushwa katika televisheni akiwa mbele ya wanajeshi wa kambi ya Fort Myer kaunti ya Arlington, huko Virginia, kundi la Talibal lilitoa tamko la kuendeleza mapigano hadi pumzi yao ya mwisho na kuonya iwapo Marekani haitaondoka Afghanistan basi nchi hiyo itageuka kuwa eneo la makaburi ya wanajeshi wa Kimarekani.

Afghanistan US-Marines in Helmand
Wanajeshi wa Kimarekani wakipandisha bendera ya Marekani, jimbo la Helmand AfghanistanPicha: Getty Images/AFP/W. Kohsar

Afghanistan hata hivyo imeipokea hotuba ya Trump kwa mitazamo tafauti. Baadhi ya raia wa kawaida wamefurahia maneno makali ya Rais Donald Trump dhidi ya Pakistan alipoishutumu nchi hiyo kwa kuwahifadhi magaidi huku wakiwaua wanajeshi wa Kimarekani katika nchi jirani ya Afganistan.

Lakini wachambuzi wa Pakistan wanaonya kutengwa kwa nchi hiyo kama mkosa pekee kutasababisha kuongezeka kwa ushawishi wa nchi kama Urusi, China na hata Iran nchini humo.

Waafghani wengi waliohojiwa na shirika la habari la AP katika mji mkuu wa Kabul, wameelezea hofu zao juu ya hali kuwa mbaya zaidi nchini, wakisikitikia rushwa,  kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira na mauwaji mabaya yanayotokana na  mashambulizi.

Kwa upande wa nchi za magharibi, Uingereza leo imekubaliana na uamuzi wa Rais Trump wa kuongeza kasi katika kampeni ya kijeshi dhidi ya waasi wa kundi la Taliban nchini Afghanista.

Uingereza na washirika wengine wa nchi za Ulaya wameahidi kutoa wanajeshi zaidi kulisaidia jeshi la Afghanistan mwezi Juni, huku Waziri wa Ulinzi wa Marekani Jim Mattis akisema kwa wakati huo kwamba idadi ya wanjeshi nchini humo ilikuwa ikipungua haraka mno.

Kwa sasa Marekani ina wanajeshi wapatao 8,500 nchini Afghanistan wanaopigana vita ambavyo Marekani ilijitumbukiza ndani yale baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, mwaka 2001.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae/ap/rtre

Mhariri: Caro Robi