1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atishia kuiondoa Marekani kutoka WHO

Amina Mjahid
19 Mei 2020

Rais wa Marekani, Donald Trump ametishia kuiondoa Marekani katika Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO akiishutumu kwa kutolishughulikia ipasavyo janga la virusi vya corona na kuielezea WHO kama kibaraka cha China.

https://p.dw.com/p/3cSi1
US Präsident Trump in Washington
Picha: Reuters/L. Millis

Kiongozi huyo wa Marekani amekuwa akizozana na China akiishutumu kwa kutokuwa wazi juu ya mripuko wa virusi vya corona, vilivyotokea kwa mara ya kwanza mjini Wuhan, kabla ya virusi hivyo kusababisha vifo na kuuyumbisha uchumi wa dunia.

Akizungumza katika ikulu ya White House, Trump amesema WHO imekuwa ikitoa ushauri mbaya huku akiishutumu kuwa kibaraka cha China

Trump amesema njia pekee ya kusonga mbele ni pale WHO itakapoonyesha ina mawazo yake binafsi bila ya kuiegemea China. Baada ya kumuandikia barua mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, Trump amelipa shirika hilo siku 30 kuboresha shughuli zake au ikose kabisa kufadhiliwa na Marekani.  

Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Getty Images/Afp/F. Coffrini

Kabla ya kitisho hicho shirika la afya ulimwenguni tayari liliahidi kufanya uchunguzi huru juu ya majibu yake ya kukabiliana na virusi vya corona.

China kwa upande wake imeendelea kukanusha madai ya Marekani kwamba ilidanganya kuhusu kiwango cha kitisho cha virusi vya corona. Rais Xi Jinping ameiambia WHO kuwa taifa lake lilikuwa wazi katika kipindi kizima cha mgogoro wa virusi hivyo.

Zaidi ya watu 317,000 wamefariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19 huku wengine takriban milioni 4.8 wameambukizwa virusi hivyo duniani. Mataifa mbalimbali yako mbioni kutafuta tiba kamili ya virusi hivyo huku wakitafuta njia mbadala za kupiga jeki uchumi wao. 

Trump atangaza kunywa dawa ya hydroxyl-chloroquine kujikinga na virusi vya corona

Wakati mzozo huo kati ya Marekani, WHO na China ukiendelea Rais Trump ametangaza kunywa dawa ya Malaria ya hydroxyl-chloroquine ili ajikinge dhidi ya virusi vya corona licha ya mamlaka za afya kuonya kuwa hatua hiyo sio salama. Trump amesema anatumia dawa hiyo maana amesikia taarifa nzuri kuihusu.

USA Präsident Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump Picha: picture-alliance/CNP/S. Reynolds

Huku hayo yakiarifiwa watengenezaji wa magari wa Marekani wameanza kurejea kazini na Ulaya inaendelea kulegeza masharti yake dhidi ya mapambano ya virusi vya corona. Lakini huku visa hivyo vikiripotiwa kupungua katika mataifa mengi Urusi, Brazil Mexico na India idadi ya walioambukizwa inazidi kupanda.

Urusi imeripoti visa 300,000 hii leo wakati serikali ikiorodhesha maambukizi mengine 9,000 mapya. Waziri Mkuu, Mikhail Mishustin ameonya kuwa hali nchini humo inaendelea kuwa ngumu.

Iran iliripoti kupungua kwa visa vya corona mwezi Aprili lakini ikatoa tena taarifa ya kuongezeka kwa idadi ya walioambukizwa mwezi Mei.

Vyanzo: reuters,afp, ap