1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera ya nje ya Trump yasababisha wasi wasi

Admin.WagnerD28 Aprili 2016

Anaewania tiketi ya kukiwakilisha chama cha Republican katika uchaguzi wa rais nchini Marekani, Donald Trump amesema, akichaguliwa, atayaweka maslahi ya Marekani mbele

https://p.dw.com/p/1Ieb7
Anaewania tiketi ya kukiwakilisha chama cha Republican katika uchaguzi wa rais nchini Marekani, Donald Trump
Anaewania tiketi ya kukiwakilisha chama cha Republican katika uchaguzi wa rais nchini Marekani, Donald TrumpPicha: picture-alliance/AP/E.Vucci

Akifafanua sera ya nje anayokusudia kuitekeleza endapo ataingia Ikulu, Trump pia amesema atawataka washirika wa Marekani wabebe wenyewe gharama za ulinzi ikiwa hawatachangia katika gharama zinazobebwa na Marekani kwa ajili ya kuwalinda washirika hao. Trump ametamka kuwa Marekani haitakuwa na njia nyingine.

Amesema Marekani imetumia Matrilioni ya dola kwa ajili ya ndege, manowari na zana zingine, kulijenga jeshi ili kuwalinda washirika wa Marekani katika mabara ya Ulaya na Asia. Trump atazitaka nchi nazo zilipe kwa ajili ya ulinzi huo la sivyo Marekani iwe tayari kuziacha zijilinde zenyewe.Ametamka kuwa hakuna njia nyingine.

Akihutubia kwenye hoteli ya Mayflower mjini Washington DC Donald Trump aliwaambia Wamarekani na dunia nzima kwamba sera yake ya nje itakuwamo katika msingi wa kuyazingatia maslahi ya Marekani. Amesema atayaweka maslahi ya Marekani mbele.

Ameahidi kuandaa mikutano miwili ya jumuiya ya kijeshi ya NATO na washirika wa barani Asia kujadili njia za kuijenga upya mifungumano yao ili kuipunguzia Marekani mzigo wa gharama.

Amkosoa Obama kwa kuiendekeza Iran

Katika hotuba yake mjumbe huyo wa chama cha Republican pia amemkosoa Rais Obama kwa alichosema kuionyesha Iran upendo na kuifanya nchi hiyo liwe taifa kubwa. Trump amesema badala yake Obama hakuwa rafiki wa Israel.

Bwana Trump pia alitahadharisha juu ya hatari ya watu wenye itikadi kali.Amesema lazima kukomesha kuwaingiza watu wenye itikadi kali nchini kutokana na sera ya uhamiaji isiyokuwa ya busara.Hatujui watu hawa wanatoka wapi.Ameitaka Marekani iwe macho na ikumbuke yaliyotukia kwenye kituo cha Biashara ya Dunia na yaliyotukia tarehe 11 mwezi Septemba.

Bwana Trump anaewania tiketi ya kukiwakilisha chama chake cha Republican katika uchaguzi wa Rais pia aliwakosoa marais wa hapo awali wa vyama vyote viwili kwa kuiingiza Marekani katika migogoro ya kijeshi katika nchi za nje.

Lakini ameeleza kuwa Marekani huenda ikalazimika kutumia nguvu za kijeshi ili kuwakabili magaidi wanaojiita Dola la Kiislamu.Trump ametoa ujumbe kwa magaidi wa Dola la Kiislamu kwa kusema kwamba siku zao zinakaribia mwisho. Mwanasiasa huyo amesema hatawaambia wapi na lini Marekani itashambulia.

Juu ya China ameeleza kuwa anataka kujenga uhusiano na nchi hiyo lakini kutokea katika msingi wa nguvu. Pia amesisitiza juu ya kuziimarisha nguvu za kijeshi za Marekani.Na amemkebehi Obama kwa kusema, wakati jeshi la Marekani limedhoofika majenerali na viongozi wa jeshi hilo wanaambiwa walitilie maanani suala la kuongezeka kwa joto duniani.

Hotuba ya Trump ni uzuri wa mkakasi

Juu ya hotuba ya Trump msemaji wa sera za nje wa chama cha Social Demokratik nchini Ujerumani Niels Annen ameeleza kuwa kauli za Trump zimesababisha wasi wasi miongoni mwa washirika wa Marekani. Aliekuwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Madeleine Albright amesema hotuba ya Trump ilijaa vidokezo sahili na mikingamo

Mwandishi:Mtullya Abdu.rtre,afp

Mhariri:Iddi Ssessanga