1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aikosoa China kusafirisha mafuta Korea Kaskazini

Isaac Gamba
29 Desemba 2017

Rais wa Marekani Donald Trump ameikosoa China  kufuatia taarifa kuwa meli za China zimetumika kuhamishia mafuta katika meli za Korea Kaskazini na hivyo kukiuka  vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi   ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2q5e0
USA Präsident Donald Trump
Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Rais Trump ameandika katika ukurasa wake wa twitter kuwa China imeshuhudiwa ikiruhusu mafuta kusafirishwa kwenda Korea Kaskazini na kusema amekatishwa tamaa na hatua hiyo na kuongeza kuwa hakutakuwa na suluhisho la kirafiki kuhusiana na Korea Kaskazini iwapo vitendo hivyo vya China vitaendelea.

Trump ambaye mara kadhaa amekuwa akisifu juhudi za China katika kuweka mbinyo dhidi ya Korea Kaskazini hakugusia hatua za kijeshi kutatua mzozo huo wa Korea Kaskazini lakini hivi karibuni alitishia kuisambaratisha Korea Kaskazini iwapo vita itatokea.

China ambayo  ni mshirika muhimu wa kibiashara  na Korea Kaskazini wiki mbili zilizopita ilisifiwa na rais Donald Trump kwa msaada wake katika juhudi zinazooongozwa na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini ikiwa ni pamoja na kuunga mkono vikwazo vya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya taifa hilo lililotengwa.

Hata hivyo Jumanne wiki hii gazeti moja la Korea Kusini likiwanukuu maafisa  kadhaa wa Korea Kusini liliripoti kuwa satelaite za Marekani zilishuhudia meli za China zikihamishia mafuta katika meli za Korea Kaskazini  karibu mara 30 mwezi Oktoba  katika eneo la bahari upande wa China taarifa ambazo pia  ziliandikwa na vyombo vya habari vya Marekani ikiwa ni pamoja na shirika la habari la Fox.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani  imesema  Marekani inataarifa kuwa baadhi ya meli zimekuwa zikihusika na  shughuli zilizopigwa marufuku na Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa shehena ya mafuta yaliyosafishwa pamoja na kusafirisha makaa ya mawe kutoka Korea Kaskazini.

Kim Jong Un
Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un Picha: picture-alliance/AP Photo

 Afisa mmoja wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alisema wanaushahidi kuwa baadhi ya meli zinazohusika na usafirishaji mafuta zina milikiwa na makampuni ya nchi kadhaa yakiwemo kutoka China.

Marekani imesema inalaani kitendo hicho na kuwa ina tumaini nchi yeyote mwanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo China  itatoa ushirikiano wa karibu kuzuia usafirishaji wa aina hiyo.

 

China yakanusha taarifa hizo

Wizara ya mambo ya nje ya China kupitia kwa msemaji wake imesema inatekeleza ipasavyo vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini na kuongeza kuwa hana taarifa  za hivi karibuni nyingine tofauti na hivyo.

Usafirishaji wa bidha kwa njia ya meli unaoihusisha Korea Kaskazini ni  suala lililozuiwa kupitia vikwazo vilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa Septemba 11 pamoja  na vikwazo vilivyotangazwa  hivi karibuni  kufuatia Korea Kaskazini kufanya  jaribio la kombora lenye uwezo wa kutoka bara moja kwenda jingine.

Mwezi uliopita idara ya fedha ya Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya makampuni sita ya Korea Kaskazini pamoja na meli 20 na  Oktoba 19 kuchapisha picha ilizodai ni meli za Korea Kaskazini ambazo huenda zilikuwa zikihamisha  mafuta ili kukwepa vikwazo dhidi yake.

China Kongress der Kommunistischen Partei Xi Jinping
Rais wa China Xi JinpingPicha: Reuters/J. Lee

Hata hivyo taarifa hiyo haikufafanua iwapo meli za China zilihusika katika kuhamisha mafuta hayo.

Azimio  la Umoja wa Mataifa lililoandaliwa na Marekani linapiga marufuku usafirishaji wa bidhaa zitokanazo na mafuta yaliyosafishwa kwenda Korea Kaskazini kwa kiwango cha asilimia 75 , kuweka kikomo kuhusiana na biashara ya makaa ya mawe pamoja na kuagiza raia wa Korea Kasakzini wanaofanya kazi nje ya nchi  hiyo warejeshwe ifikapo mwishoni mwa mwaka 2019.

Mwandishi: Isaac Gamba/afpe/ape

Mhariri       :Gakuba, Daniel