1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Toure mchezaji bora Afrika kwa mara ya nne

9 Januari 2015

Yaya Toure ametangazwa kuwa mchezaji bora barani Afrika kwa mara ya nne na kuifikia rekodi iliyowekwa na mshambuliaji wa zamani wa Cameroon Samuel Eto'o. Toure amewabwaga Aubameyang na Enyeama

https://p.dw.com/p/1EHvE
Afrikas Fußballer des Jahres 2014 Yaya Toure
Picha: Pius Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

Kiungo huyo wa Cote d'Ivoire na Manchester City pia ndiye mchezaji wa kwanza kushidna tuzo hiyo mfululizo. Tangazo hilo lilitolewa katika sherehe iliyoandaliwa mjini Lagos. Toure alishinda Taji la Ligi ya Premier ya England na Taji la League Cup mwaka jana na akachaguliwa kama mmoja wa wachezaji wa timu bora ya ligi ya mwaka jana. Amesema "Kusema tu ukweli – mambo ya kandanda hayajulikani. Kila mara ninataka kushinda mataji muhimu. Lakini nilijua itakuwa vigumu, kwa sababu wachezaji wapya wanainuka kwa kasi. Tuna wachezaji bora chipukizi wanaoinukia sasa, na wachezaji hao wanafanya vyema sana katika vilabu wanavyochezea"

Bildergalerie Afrikanische Fußballspieler Yaya Toure
Yaya Toure ni nguzo muhimu katika klabu ya Manchester City ya EnglandPicha: Getty Images/A. Livesey

Japokuwa hakupata mafanikio makubwa katiak Kombe la Dunia nchini Brazil huku Cote d'Ivoire ikiondolewa katika hatua ya makundi, mchezo wa Toure katika klabu yake ya City ulikuwa wa hali ya juu. Toure ataiwakilisha nchi yake katika dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Guinea ya Ikweza kuanzia mwishoni mwa wiki hii. Toure aliongeza kuwa "nadhani kawaida huwa ni uamuzi mgumu. Unastahili kuchezea nchi yako na kuiacha klabu yako katika miezi hiyo muhimu. Ligi ya Premier kawaida huwa ngumu. Lakini City ina wachezaji wazuri wanaoweza kufanya vyema bila mimi kuwepo. Ni vigumu kuchagua, lakini kitu cha kwanza siku zote huwa nchi. Hivyo natumai ninaweza kwenda huko, nicheze vyema na kuipa fahari nchi yangu".

Mshambuliaji wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang na mlinda lango wa Nigeria Vincent Enyeama ni wachezaji wengine waliokuwa katika orodha ya wagombea watatu wa mwisho. Algeria ilishinda tuzo ya timu bora ya mwaka baada ya kudhihirisha umahiri wake kama timu inayorodheshwa ya kwanza Afrika katika viwango vya FIFA, ikafika katika duru ya pili ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza na ikafuzu kwa urahisi katika Kombe la Mataifa ya Afrika.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reueters/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga